Mondi Ashtua Tena na Saa ya milioni 500

DAR : Achana na kufuru nyingine alizowahi kuzifanya huko nyuma, mkali wao kwenye Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ ameshtua tena kwa kutinga saa inayocheza kwenye shilingi milioni 500 na kuendelea, Gazeti la IJUMAA linakushushia ripoti kamili.

 

Hii si mara ya kwanza kwa Diamond au Mondi kutinga saa ya mamilioni ya shilingi kwani amewahi kuushangaza ulimwengu wa showbiz (burudani) ndani na nje ya Bongo kwa kuonekana na saa ya shilingi milioni 290.

 

TUICHEKI HIYO MPYA

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, hivi karibuni Mondi alitupia picha yake akiwa ametinga mavazi ya kijani kuanzia juu mpaka chini huku mkononi akiwa ametupia saa hiyo mpya ambayo taarifa zilibainisha kuwa inaitwa Richard Millie 011 Red Demon.

 

GUMZO KAMA LOTE

Mara baada ya kuweka picha hiyo, gumzo kubwa mitandaoni likawa ni uwezo wa Mondi kumiliki saa ya aina hiyo ambayo inatajwa kuwa miongoni mwa saa ghali zaidi duniani.

 

Wengi waliochangia maoni yao mitandaoni walionekana kupinga kwamba haiwezekani Mondi kumiliki saa hiyo na wengine walikwenda mbali zaidi kwa kusema huwenda itakuwa ni feki kwa sababu ‘original’ yake haishikiki Kibongobongo.

 

“Wewe unafanya mchezo nini, Mondi anaweza kuvaa Richard Mille? Hebu tuache masihara na haya mambo serious, labda uniambie ni feki, hapo nitakubaliana na wewe, lakini original yake si kazi rahisi Mondi kuimiliki,” aliandika mdau mmoja kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram.

IJUMAA MZIGONI

Gazeti la IJUMAA liliingia mzigoni kusaka bei ya saa hiyo kupitia vyanzo mbalimbali ambapo lilibaini saa hiyo bei yake inaanzia kucheza kwenye Dola za Kimarekani 110, 000 (zaidi ya shilingi milioni 254) na kuendelea kulingana na madini au vionjo mbalimbali vilivyonakshiwa kwenye saa husika.

 

Kuna nyingine zinacheza kwenye Dola za Kimarekani 216,133 (zaidi ya shilingi milioni 500) ambayo inaonekana kufanana na ile ya Mondi, lakini zipo pia za zaidi ya hapo ambazo uchunguzi wa Gazeti la IJUMAA umebaini zinavaliwa na mastaa wakubwa duniani akiwemo msukuma kabumbu anayekipiga kwenye Klabu ya Juventus ya Italia, Cristiano Ronaldo ‘CR7’ na Rapa Aubrey Graham Drake.

 

Wawili hao kwa nyakati tofauti wamewahi kuposti saa hiyo toleo la Richard Mille RM 69 ambayo thamani yake ni Dola za Kimarekani 750,000 (zaidi ya shilingi bilioni 1.7) ambapo kwa hali ya kawaida, Mondi hawezi kufikia levo hizo.

KUFURU ZA MONDI

Licha ya kwamba saa ya Mondi haijafika kwenye levo hizo za akina Ronaldo na Drake, lakini siku za hivi karibuni staa huyo wa Wimbo wa Jeje amefanya kufuru za aina yake ambapo amenunua hoteli ya maana iliyopo maeneo ya Mikocheni B jijini Dar.

 

Lakini kama hiyo haitoshi, pia amenunua gari la kifahari aina Rolls Royce ambalo inatajwa kuwa miongoni mwa magari ya kifahari duniani. Usisahau pia kuna kijiji kinachodaiwa anakijenga kikitajwa kuwa maeneo ya Kigamboni jijini Dar.

Disemba mwaka jana, Mondi aliibua gumzo la aina yake kwa kununua saa aina ya Patek Philipe Rose Gold ambayo gharama yake kwa fedha za madafu inafika shilingi milioni 290.

Stori: ERICK EVARIST, Ijumaa

Toa comment