The House of Favourite Newspapers

Mondi, Zari Ndoa Yanukia

0

CHINI ya kapeti kuna mambo matamu! Msanii Nasibu Abdul ‘Mondi’ na mzazi mwenziye Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ ndoa yao inanukia.

Chanzo kutoka ndani ya familia kimeliambia RISASI kwamba, sintofahamu iliyokuwepo kati ya wawili hao imezikwa kitambo.

Vurugu za kupostiana kwenye mitandao ya kijamii kati ya Zari, watoto wake na familia ya Mondi zinazoendelea zimetajwa kubeba siri ya wawili hao kufungua ukurasa mpya wa maisha.

 

CHANZO WATOTO

Mtoa habari wetu ambaye anatoka ndani ya familia hiyo alisema:

“Asikuambie mtu, familia ya Diamond (Mondi) hasa mama yake mzazi (Sanura Kassim ‘Mama D’) anawapenda sana wajukuu zake.

 

“Hana furaha ya kuishi nao mbali, nadhani unaona mwenyewe, baada ya tofauti kati ya mwanaye na Zari kuisha amekuwa akimshawishi mwanaye amuoe Zari ili walee watoto wasije wakapotea.

“Kwa kuwa Mondi hapindui kwa mama yake amemwambia hawezi kupingana na mtazamo wake,” chanzo chetu kilisema.

Yote haya yanakuja siku chache baada ya Mondi kutamka kuwa kwa sasa hahitaji tena maisha ya kurukaruka na wanawake na kwamba jamii ikimsikia basi atakuwa ameoa.

 

SHINIKIZO MITANDAONI

Katika hali inayoonesha kuwa mashabiki wa Mondi wanaipenda ‘kapo’ yake na Zari, mara kadhaa wamekuwa wakishabikia kufufuka kwa uhusiano wao ambao ulikufa miaka miwili iliyopita.

Siku chache baada ya gazeti dada la hili la IJUMAA WIKIENDA kuripoti kuwa Zari na Mondi wamerudiana na baadaye kuthibitika, shangwe lilikuwa kama lote mitandaoni kwa upande wa mashabiki wa Zari na Mondi.

 

“Mungu ni mwema jamani yaani nilikuwa naumwa hawa watu kuachana.”

“Mondi vuta chuma hicho kimejileta.”

“Wachawi sijui wataweka wapi sura zao.”

Hizo ni baadhi ya komenti ambazo zilipostiwa kwenye mtandao wa Instagram kwenye kurasa za watu tofautitofauti walioripoti wawili hao kumaliza tofauti zao.

 

FAMILIA YA MONDI KICHEKO

Aidha, gazeti hili lilipofanya mahojiano na mmoja kati ya ndugu wa Mondi (jina linafichwa) na kumuuliza kuhusu kinachoendelea kwa wawili hao alisema:

“Familia nzima tumefurahi na hata hilo la ndoa yao unalosema likitokea tutalipokea kwa mikono miwili.”

 

MUME WA MAMA D SASA…

Mume wa Mama D, Maisara Abdul ‘Uncle Shamte’ ambaye ni baba wa kambo wa Mondi hivi karibuni alionesha furaha yake kwa Zari na mwanaye Tiffah kupitia ukurasa wake wa Instagram kwa kuposti picha zao.

Baadaye akaweka komenti iliyosomeka: “Mama Tee, mke huyo (Tiffah ambaye ni mwijukuu wake) namfuata mwenyewe.”

Mama D naye kuonesha kuwa ana mahaba na Zari na watoto wake aliweka video kwenye akaunti yake ya Instagram, ikimuonesha Tiffah akiwa anamsifia baba yake na kuwafanya wenye maneno yao kujiachia watakavyo kwa komenti.

 

ZARI KUTUA BONGO KARIBUNI

Habari za chini ya kapeti zililinyetishia RISASI kuwa Zari anatarajiwa kutua Bongo hivi karibuni endapo kikwazo cha Karantini ya Corona kilichowekwa nchini Afrika Kusini anakoishi kwa sasa na watoto aliozaa na Mondi, Tiffah na Nillan, kitaondolewa.

 

Chanzo chetu kilisema, Karantini ndiyo iliyokwaza mpango wa Zari kuja nchini akiambatana na watoto wake kwa lengo la kuja kujumuika na familia ya mzazi mwenzake.

Awali, taarifa zilisema kuwa Mondi na familia yake walikuwa wameandaa mapokezi ya kufa mtu ya Zari na wanaye ili kuionesha jamii kuwa ukurasa mpya umefunguliwa na kwamba yaliyopita si ndwele ya kugangwa ni yajayo.

 

KUMBUKUMBU

Zari na Mondi walimwagana kufuatia bibie huyo kudai kwamba Mondi anamdhalilisha kwa kuwa na michepuko.

Baada ya kuachana, Mondi aliangukiwa kwa mwanamke mwingine raia wa Kenya, Tanasha Donnah ambaye alizaa naye pia mtoto na kisha kummwaga.

 

Zari naye aliingia kwenye uhusiano usioeleweka na mwanaume aliyekuwa akimtaja kwa jina la King Bae ambaye hakupata kumuonesha sura yake kwenye mitandao ya kijamii.

Kwa takriban miaka miwili Zari na Mondi walifungiana vioo huku wakipigana vijembe lakini siku za hivi karibuni penzi lao lilifufuka kwa wawili hao kuanza kuwasiliana kupitia mitandao ya kijamii ambapo kwa sasa ishu ya ndoa yao inatajwa kunukia.

STORI | Happyness Masunga, Risasi

Leave A Reply