Morocco Anukia Geita Gold FC
Siku chache baada ya klabu ya soka ya Geita Gold ya mkoani Geita kutangaza kuachana na aliyekuwa kocha wake mkuu Fred Felix Minziro ‘Baba Isaya’ taarifa za ndani kutoka ndani ya klabu hiyo zinaeleza kuwa kwa sasa uongozi wa klabu hiyo uko katika hatua za mwisho kumpata Kocha msaidizi wa Taifa stars na kocha mkuu wa timu ya Zanzibar Heros Hemed Morocco kwaajili ya kukinoa kikosi hicho kuelekea msimu ujao wa ligi.
Morocco ambaye amewahi kuvinoa vilabu vya Mbao fc, pamoja na Namungo fc anawindwa vikali na wachimba dhahabu hao wa Geita ambapo mtoa taarifa huyo ameiambia Global Publishers kuwa ” ni kweli Viongozi walikua katika harakati za kutafuta kocha wa kuchukua nafasi ya Minziro lakini kwa dalili zilizopo ni kuwa wanakaribia kumalizana na Morocco ambaye kwa sasa hana timu ukiachilia mbali majukumu yake ya timu za taifa” alisema
Geita Gold ikiwa chini ya kocha Fred Felix Minziro ilifanikiwa kumaliza ligi ikiwa ndani ya nafasi sita za juu ambapo kwa msimu wa mwaka 2021/2022 walimaliza ligi wakiwa nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi kuu huku msimu wa mwaka 2022/2023 wakimaliza nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi kuu ambapo huu utakua msimu wao wa tatu kucheza ligi kuu tangu walipopanda daraja kucheza ligi kuu mwaka 2020.