Morrison Amvurugia Mo Dewji Kwa Shonga GSM
HESABU za mabosi wa Simba wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya timu hiyo, Mohammed Dewji ‘Mo’ ni kumshusha straika raia wa Zambia, Justine Shonga anayekipiga Orlando Pirates ya nchini Afrika Kusini katika usajili wa msimu ujao kwa ajili ya kuongeza nguvu kikosini hapo.
Lakini kabla ya dili hilo kukamilika, kiungo mshambuliaji wa Yanga, Bernard Morrison amelivuruga, hiyo ni baada ya kuwaambia viongozi wake kwamba wampe fedha za kutosha kwa ajili ya kumleta Mzambia huyo klabuni hapo.
Shonga amekuwa akihusishwa na Simba tangu msimu uliopita wakati kikosi hicho kilipoenda kuweka kambi nchini Sauz, ambapo kwa sasa wana asilimia kubwa ya kumtwaa kutokana na straika huyo kukosa nafasi mara kwa mara ya kucheza ndani ya kikosi cha Orlando Pirates.
Ikumbukwe kwamba kabla ya kuja Yanga, Morrison mwenye mabao matatu katika Ligi Kuu Bara, aliwahi kuichezea Orlando Pirates.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Morrison amesema kuwa anamfahamu Shonga ambaye dau lake ni Sh mil 800, ni mchezaji mzuri na kama akitua Bongo ana uwezo mkubwa wa kupafomu katika ligi ya hapa.
Morrison ameongeza kwamba ana uwezo wa kuzungumza moja kwa moja na Shonga na kumleta Bongo lakini mabosi wa Yanga wampe fedha nyingi kwa ajili ya kumvuta.
“Nani wanataka kumnunua Shonga? Ni mchezaji mzuri ndivyo ninavyoweza kusema kwa ujumla wake na ana uwezo mkubwa, anaweza kuja hapa na kupafomu vizuri tu bila tatizo.
“Ninaweza kufanya naye mazungumzo kuja Yanga, lakini viongozi wa Yanga wanatakiwa kunipa fedha nyingi za kumfanya atue hapa,” alisema Morrison.