The House of Favourite Newspapers

Morrison Awatibulia Simba, Wachezaji Wapiga ‘stop’ Kuongea

0

UNAWEZA ukasema mzimu wa kiungo wa Yanga, Bernard Morrison, bado unaitafuta Simba, hiyo ni mara baada ya uongozi wa klabu hiyo kuwapiga ‘stop’ wachezaji kuzungumza na chombo kingine chochote cha habari zaidi ya Simba TV.

 

Inaelezwa kuwa uongozi umefikia hatua hiyo mara baada ya baadhi ya wachezaji wa Simba kumtaja na kumsifia Morrison katika moja ya mahojiano waliyofanya hivi karibuni, huku wengine wakisifia bao la faulo alilolifunga kiungo huyo katika dabi ya watani wa jadi, Machi 8, Simba wakifa 1-0.

 

Uamuzi huo ulitolewa jana Jumanne na uongozi wa juu wa klabu hiyo katika kikao cha viongozi na wachezaji

kilichodumu kwa muda wa zaidi ya saa tatu.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya uongozi wa Simba, ambacho kiliomba hifadhi ya jina lake, kililiambia Championi Jumatano kuwa: “Itakuwa ngumu kwa sasa wachezaji kuzungumza na chombo chochote cha habari ambacho hakimilikiwi na Simba, mara baada ya hivi karibuni baadhi ya wachezaji kufanya mahojiano na vyombo mbalimbali vya habari na kuzungumza baadhi ya mambo ambayo hayakuipendeza klabu.

 

“Hivyo, ruhusa imetolewa kwa wachezaji hao kufanya mahojiano na Simba TV pekee, ambayo inamilikiwa na klabu hiyo, maamuzi hayo yameamuliwa leo(jana), katika kikao kilichofanyika kati ya sisi viongozi na wachezaji.”

 

Gazeti hili lilijaribu kumtafuta meneja wa klabu hiyo, Patrick Rweyemamu ili kujua ukweli wa taarifa hizo, simu yake iliita bila kupokelewa.

 

Alipotafutwa mmoja wa wachezaji wa kikosi cha kwanza cha timu hiyo alikiri kwa kusema:

“Ni kweli haturuhusiwi kuongea na chombo chochote cha habari zaidi ya Simba TV, kama mwandishi ukiwa na shida mcheki meneja.”

Stori: Issa Liponda, Championi Jumatano

Leave A Reply