The House of Favourite Newspapers

Morrison Hana Bahati na Yanga

0

UNAAMBIWA gonga jiwe usikie mlio wake, basi ukimgonga mzee wa kuchetua ndani ya kikosi cha Simba, Bernard Morrison utakutana na mambo matatu ambayo yamemfanya akae jukwaani wakati timu yake ikicheza na mabosi zake wa zamani Yanga.

 

Nyota huyo raia wa Ghana aliibuka ndani ya Simba akitokea Yanga ambao waliweka wazi kuwa bado ni mchezaji wao kwa kuwa alisaini huko akiwa na mkataba hivyo kesi yao ipo Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo (CAS).

 

Weka kando masuala ya kuvutana na mabosi wake ila ukweli ni kwamba hana bahati ya kukutana na Yanga kwenye mechi nyingi za ushindani kutokana na sababu mbalimbali.

 

Kuelekea kwenye Kariakoo Dabi inayotarajiwa kuchezwa Septemba 25, Uwanja wa Mkapa ikiwa ni Ngao ya Jamii pia hatakuwepo, hapa ni sababu zilizofanya nyota huyo akakosa baadhi ya mechi dhidi ya Yanga:-

 

UGONJWA

Mchezo wa Fainali ya Kombe la Mapinduzi kule visiwani Zanzibar ilikuwa ni Simba Vs Yanga jamaa hakuwa na bahati ya kucheza kwenye mchezo huo.

 

Ilikuwa ni Januari 13, 2021, visiwani Zanzibar, Simba walikutana na Yanga ambapo ushindi ulikuwa mikononi mwa Yanga ambayo ilishinda kwa mikwaju ya penalti 4-3 kwa kuwa dk 90 ngoma ilikuwa Yanga 0-0 Simba.

 

Kwenye mchezo huo uliokuwa na mashabiki wa kutosha waliishia kumuona Morrison akipasha tu kwa muda kisha akarejea benchi kuendelea na mambo mengine kwa kuwa hakupewa nafasi ya kuingia.

 

Sababu iliyotajwa nyota huyo kushindwa kucheza mchezo huo ilikuwa ni kwamba bado hajawa fiti kwa kuwa alikuwa anaumwa.

 

Kwa mujibu kwa Kocha Msaidizi wa Simba, Seleman Matola aliliambia Championi Jumatano namna hii: “Kwenye mchezo wetu wa fainali wa Kombe la Mapinduzi, Morrison aliomba apewe dakika 10 ili aweze kuonyesha makeke yake kwenye mchezo huo ila ilishindikana kwa sababu presha ilikuwa kubwa.

 

“Pia sababu nyingine ni kwamba bado alikuwa hayupo fiti kwa kuwa alikuwa anaumwa ila ugonjwa wake hilo ni suala ambalo linapaswa kuzungumziwa na wataalamu, hilo lilipita na tunaangalia mambo mengine.”

 

NGUMI MKONONI

Ngumi ya mshikaji Morrison ni nyepesi akiwa uwanjani hasa pale anapodhani kwamba jambo alilofanyiwa sio sawa na mpinzani wake.

 

Ilikuwa ni Oktoba 26, Uwanja wa Uhuru wakati ubao uliposoma Simba 0-1 Ruvu Shooting, Morrison alionekana akimpiga beki wa Ruvu Shooting, Juma Nyosso.

 

Ilikuwa hivi, Nyosso alionekana akimkanyaga Morrison aliyekuwa nyuma yake naye BM3 hakukubali alimpiga ngumi ya kichwa Nyosso.

 

Kutokana na sakata hilo mzee wa kukera alikutana na rungu la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kufungiwa kucheza mechi tatu za ligi.

 

Miongoni mwa mechi ambazo alizokosa jumlajumla ilikuwa ni ile ya Oktoba 31, Simba 5-0 Mwadui FC, Uwanja wa Uhuru, Novemba 4, Simba 2-0 Kagera Sugar, Uwanja wa Uhuru na aliwakosa mabosi zake wa zamani, Yanga.

 

Dabi hiyo ya kibabe ilichezwa Uwanja wa Mkapa ilikuwa ni Novemba 7 na ubao ulisoma Yanga 1-1 Simba na watupiaji walikuwa ni Michael Sarpong kwa upande wa Yanga na Joash Onyango.

 

BUKTA PIA KIKWAZO

Jamaa haishiwi maneno wala vituko, ilikuwa ni kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho, mchezo uliochezwa Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma. Morrison baada ya timu yake ya Simba kushinda kwa bao 1-0 dhidi ya Yanga alionekana akishangilia kwa nguvu kubwa na aliweka bukta yake kichwani akiendelea na mishe nyingine.

 

Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi alimfuata na kumuelekeza kuwa avae bukta hiyo ila aligomea na kuendelea kushangilia ushindi wa kutwaa Kombe la Shirikisho.

 

Kutokana na ishu hiyo, TFF walimshushia rungu kwa kumfungia mechi tatu za kucheza na picha ya kwanza inaanza kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga unaotarajiwa kuchezwa Septemba 25.

 

Mechi yake ya pili kukaa jukwaani itakuwa dhidi ya Biashara United ambayo inatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Karume, Mara na huu utakuwa ni mchezo wa kwanza wa ligi pamoja na mchezo wa tatu itakuwa dhidi ya Dodoma Jiji, Oktoba Mosi, Uwanja wa Jamhuri.

 

NENO LA MORISSON

Baada ya kurejea kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho, Morrison aliweka wazi kuwa ilikuwa ni furaha na alikuwa amevaa nguo nyingine jambo ambalo hakuona ajabu.

 

Kuhusu kuikosa Yanga, Morrison alisema: “Watu wengi wamesahau kama mimi sitakuwa sehemu ya mchezo huo wa Ngao ya Jamii, kutokana na kutumikia adhabu ila kungekuwa na uwezo wa kuomba adhabu isogezwe mbele ningeomba ili niwalambishe juisi Yanga, jambo ambalo halitawezekana tena japo tutashinda.”

LUNYAMADZO MLYUKA, Dar es Salaam

 

Leave A Reply