Morrison, Mugalu Wapewa Jukumu Zito DR Congo

KUTOKANA na uzoefu wake alionao wa kuwahi kucheza soka Kinshasa, DR Congo, benchi la ufundi la Simba limempa jukumu zito kiungo wake mshambuliaji, Mghana Bernard Morrison la kuwamaliza wapinzani wao AS Vita.

 

Timu hizo zinatarajiwa kuvaana leo Ijumaa katika mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaopigwa saa moja kamili kwenye Uwanja wa Martyrs jijini Kinshasa.

Simba katika msimu wa mwaka juzi wakiwa wanashiriki michuano hiyo ya kimataifa, walichapwa mabao 5-0 katika uwanja huo na wapinzani hao wa leo Akizungumza na Championi Ijumaa, Kocha Mkuu wa Simba, Mfaransa, Didier Gomes alisema kiungo wake huyo ana uzoefu wa kucheza ligi ya DR Congo kama ilivyo kwa Mkongomani, Chris Mugalu.

 

Gomes alisema kuwa uzuri zaidi waliwahi kuutumia uwanja huo wa Martyrs utakaotumika kuchezea mchezo huo, hivyo amewataka kuutumia uzoefu wao huo katika kupata matokeo mazuri.

“Mchezo uliopita wa ligi dhidi ya Azam FC tulifanya makosa ya kizembe hasa safu ya ushambuliaji ambayo ilishindwa kutumia nafasi nyingi walizokuwa wanazipata za kufunga mabao.“Hivyo, sitaki kuliona hilo likitokea tena, ninataka kuona tunatumia vema kila nafasi tutakayoipata, ni vema tukaitumia kufunga mabao ili kupunguza presha ya timu,” alisema Gomes

Stori: Wilbert Molandi, Dar es Salaam

Toa comment