Moses Phiri: Yanga ni Timu Kubwa, Fei Toto ni Bonge la Mchezaji

UNAPOLITAJA jina la Moses Phiri, basi linakuwa sio geni tena kwa mashabiki wa soka nchini ambao wanafuatilia kwa karibu zile tetesi za usajili katika dirisha dogo la usajili ambalo linaendelea kwa sasa mpaka litakapofungwa rasmi Januari 16.

 

Moses Phiri, mwenye uraia wa Zambia, kwa sasa anakipiga katika Klabu ya Zanaco ya nchini Zambia ambapo moja ya rekodi yake kubwa ni kufanikiwa kuibuka kuwa mfungaji bora wa ligi hiyo msimu uliopita kwa kufunga mabao 17.

Phiri kwa sasa anahusishwa kukamilisha usajili wake wa awali wa kujiunga na Yanga kwa kusaini mkataba wa awali wa miaka 2 na Yanga jambo ambalo Championi Jumatatu, limeamua kumtafuta mshambuliaji huyo na kufunguka haya yafuatayo…

 

UNAJISIKIAJE KUWA MCHEZAJI WA ZANACO?

“Namshukuru Mungu kuwa katika sehemu ya hii timu ambayo kwangu imenipatia nafasi nzuri ya kufanya makubwa katika ligi ya Zambia ambapo sikuwahi kuipata katika timu yoyote licha ya kucheza baadhi ya timu kutoka huku Zambia.

 

KWA NINI ZANACO NA SIYO TIMU NYINGINE?

“Hata kabla ya kuwa hapa Zanaco, nilipita katika baadhi ya timu ambapo kwa sasa sipo na nipo Zanaco, ukiachana na hilo kuna wachezaji nilikuwa nao Zanaco lakini kwa sasa hawapo, haya ndiyo maisha yetu wachezaji, siyo Zambia tu ni duniani kote.

 

MALENGO YAKO YAPOJE KWA SASA?

“Malengo yangu ni kuhakikisha nafanikiwa kucheza soka la kiwango kikubwa nje ya Zambia, malengo yangu ya kucheza Ulaya yalifanikiwa kwa asilimia 50 kwa kuwa nilicheza katika Ligi Daraja la Pili nchini Ureno.

“Natamani kuona narejea Ulaya nikiwa nacheza katika ligi kuu katika zile nchi 5 bora yaani England, Hispania, Ufaransa, Italia na Ujerumani, hayo ndio malengo yangu makubwa ambayo nimekuwa nikiyaishi, japo muda ni kama unazidi kusogea.

 

NI KWELI UMESAINI MKATABA WA AWALI NA YANGA?

“Hilo lipo nje ya uwezo wangu kwa sasa kulizungumzia kwa kuwa lipo chini ya uongozi wangu na uongozi wa klabu, hawa wanaweza kuzungumza yote na wakayafafanua vizuri zaidi yangu.

 

WEWE UPO TAYARI KUCHEZA NDANI YA YANGA?

“Mpira ni biashara siku zote, kuna maisha baada ya mpira, wachezaji tuna familia zetu lakini tuna ndugu na majamaa ambao wanatutegemea zaidi katika kuwasaidia, hivyo kama Yanga wana ofa nzuri kwa nini nisikubali kucheza Yanga?

“Lakini kuna ofa nyingi ambazo zipo mezani kutoka Tanzania na naamini mwezi Juni, mwaka huu nitakuja Tanzania lakini kama kutakuwa na mabadiliko basi sitakuja huko tena.

 

UNAIZUNGUMZIAJE YANGA KWA UNAVYOIFAHAMU?

“Yanga ni timu kubwa ambayo inahitaji kufanya makubwa, wakati tunacheza nao katika mchezo ule wa utambulisho wa wachezaji wao, nilishangaa sana, kwangu lile jambo litabaki katika kumbukumbu zangu ikiwa moja ya matukio makubwa ya soka.

“Wingi wa mashabiki wao na jinsi ambavyo wanaipenda timu yao nilishangaa, wanapenda sana mpira na naamini huko mbeleni watakuja kuwa timu kubwa sana hapa Afrika.

 

MCHEZAJI GANI ALIKUVUTIA KATIKA MCHEZO WENU NA YANGA?

“Kuna yule mchezaji ambaye anavaa jezi namba 6 kama sikosei anaitwa Feisal, ni mchezaji mzuri sana, nakumbuka kabla hatujaja kucheza naye, nilimuona katika michuano ya CHAN walipocheza na Zambia.

“Katika mchezo huo nilikuwa nipo benchi lakini kila alipokuwa akishika mpira, nilikuwa nahofia ataleta madhara, hata katika mchezo dhidi yetu alitusumbua sana katika eneo la kiungo, naamini atafika mbali zaidi.

 

UNAFAHAMU NINI KUHUSU SOKA LA TANZANIA?

“Nafahamu kwa machache kwa kuwa nimefika na kuna baadhi ya vitu naviona, kwanza kuna mashabiki ambao wanapenda mpira lakini pili ni ligi ambayo ni bora na ina wachezaji wengi wazuri.

\“Nakumbuka kuna wakati Clatous Chama na Rally Bwalya wote walikuwa wakicheza huko ndani ya Simba lakini Obrey Chirwa naye akiwa huko tulipata nafasi ya kuona vitu vyao kuhusu ligi ya Tanzania jambo ambalo limesababisha baadhi ya wakazi wa Zambia kuwa mashabiki wa timu za Tanzania.

 

UKIACHANA NA FEISAL NI WACHEZAJI GANI UNAWAFAHAMU NA UNAWAKUBALI KUTOKA TANZANIA?

“Mbwana Samatta namfahamu ambaye amecheza hadi Ulaya lakini wapo wachezaji wengine ambao nawafahamu kwa sura ila majina yao siyafahamu vizuri bila kumsahau Rally Bwalya, Obrey Chirwa, Wawa na kipa wa Simba, Aishi Manula,” anasema mshambuliaji huyo.

MARCO MZUMBE, Dar es Salaam3473
SWALI LA LEO

Kupanda Kwa Bei ya Mafuta Nchini, Nini Kifanyike Kupunguza Bei?
Toa comment