Moto Wateketeza Mali za Mamilioni Sokoni

 

WAFANYABIASHARA wanahesabu hasara baada ya mali ya thamani isiyojulikana kuteketea kwa moto usiku wa kuamkia leo (Jummane) alfajiri katika soko la Toi jijini Nairobi, Kenya. Moto huo umezuka mnamo saa tisa  usiku.

Toi ni soko maarufu linalofahamika kwa uuzaji wa bidhaa kukuu zikiwemo nguo za mtumba, lakini pia bidhaa nyingine kama mbao na vifaa vya elektroniki.

 

Muuzaji mmoja, Charlie Chaplin, ameliarifu shirika la utangazaji la Uingereza (BBC) kwamba aliamshwa alfajiri kwa simu akiarifiwa kwamba moto umezuka na alilazimika kukimbia kwenda katika soko hilo. Kwa sasa anasema anakadiria kupatwa na hasara ya mamilioni ya shilingi za Kenya.

 

Mwandishi habari aliyefika katika eneo hilo Oliver Koech, anasema baadhi ya watu wamelalamika kuhusu kuchelewa kwa zimazoto kukabiliana na moto huo kwa wakati na kuudhibiti kabla ya kusambaa kama ulivyosambaa na kuiharibu sehemu kubwa ya soko hilo.   Hiyo si mara ya kwanza magari ya zimamoto kushutumiwa nchini kwa kushindwa kudhibiti mikasa ya moto kwa muda muafaka licha ya kuwa na vifaa vipya.

 

 

Hata hivyo, makazi yasiyo rasmi  yanakuwa hayana mpangilio mzuri, kwani nyumba husongamana sana na hakuna njia za katikati, hivyo magari ya zimamoto hushindwa kuingia ndani zaidi. Hadi kufikia saa moja asubuhi ya leo, baadhi ya wauzaji walikuwa wakijaribu kukusanya masalio ya mali zao katika eneo hilo la Toi.

 

 

Wauzaji wengi wamekumbwa na hasara ya thamani ya mali za mamilioni katika soko hilo lililo karibu na mtaa mkubwa wa mabanda wa Kibera mjini Nairobi. Wanasema ni pigo kubwa, na hawajui la kufanya kutokana na kwamba walitegemea biashara katika soko hilo katika kujikimu maisha.

 

CHANZO: BBC SWAHILI

Loading...

Toa comment