The House of Favourite Newspapers

Mpambano wa Juma Nkamia na John Heche Ngoma ni Nzito!

0
Juma Nkamia.

MBUNGE wa Chemba (CCM), Juma Nkamia na John Heche wa Tarime Vijijini (Chadema), wanatarajia kupambana bungeni wakati kila mmoja atakapowasilisha mswada binafsi kuhusu ukomo wa urais.

Hivi karibuni kupitia mitandao kijamii, Nkamia alikaririwa kuwa anakusudia kuwasilisha bungeni mswada wa marekebisho wa Katiba utakaomwezesha muhula wa urais madarakani kuwa wa miaka saba baada ya mitano ya sasa.

Vivyo hivyo kwa Heche kupitia mitandao ya kijamii na yeye aliibuka, ingawa alikuwa tofauti kidogo na Nkamia lakini amesema anakusudia pia kuwasilisha bungeni hoja binafsi ya kupunguza muda wa kukaa madarakani kwa urais, wabunge na madiwani kutoka miaka mitano hadi minne.

Hatua hiyo ya Nkamia, ilikoselewa na wasomi mbalimbali akiwamo Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Ruaha, Profesa Gaudence Mpangala aliyeshangazwa na mbunge huyo huku akieleza kuwa hiyo ni mbinu ya kumuongezea muda rais aliye madarakani.

Hali ya kukoselewa imemkumba pia Heche ambaye anashambuliwa na watu mbalimbali huku wengine wakimwambia kwamba amemuiga Nkamia huku akifahamu wazi kwamba mswada huo hautafika popote kutokana na wingi wa chama tawala.

Wakati Nkamia na Heche wakikukusudia kupekeleka hoja hizo, kwa mujibu wa Katiba, Rais wa Tanzania anapochaguliwa huongoza kwa muhula wa miaka mitano na baada ya hapo anaweza kuchaguliwa tena kwa muhula mwingine wa muda kama huo.

Lakini Nkamia alisema kufanya uchaguzi kila baada ya miaka mitano ni gharama kwa nchi maskini kama Tanzania, kwani katika kipindi hicho nchi inakuwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa miaka miwili kabla ya uchaguzi mkuu na hivyo kufanya gharama ya uchaguzi kuwa kubwa.

“Badala ya Serikali kushughulikia kero za wananchi imekuwa ikishughulika kutafuta fedha za maandalizi ya uchaguzi kwa muda mrefu,” inasema sehemu ya ujumbe wa Nkamia aliotuma kwenye kundi la WhatsApp la viongozi.

John Heche.

 

Mwananchi ilipomuuliza kuhusu ujumbe huo kama ni wa kwake na ni lini atawasilisha mswada huo, mbali na kukiri kuwa ni wake, Nkamia alisema tayari ameshapeleka hoja yake ambayo wakati wowote itawasilishwa bungeni.

Akizungumza na mwananchi leo, Jumanne kutoka jijini Nairobi, Kenya, Heche amesema hajafuata mkumbo wa Nkamia na kamwe hawezi kumuiga  kwa sababu mbunge huyo wa Chemba anaiga  nchi ya … ambayo hakuna ukomo wa uongozi kwa rais, wakati yeye mimi anataka kuiga nchi ya kidemokrasia zaidi duniani, ili kuwapa wananchi uwezo mkubwa na mda mfupi kupata nafasi kufanya uamuzi.

“Nataka watu wafanye uamuzi kuhusu usimamizi wa nchi yao, kwa mujibu wa Katiba yetu Ibara ya 8 wananchi ndio wenye mamlaka na uendeshaji wa nchi. Kwa hiyo lazima wapate muda wa kuamua, kwenye hoja hiyo pia nitaweka kipengele cha viongozi wote kupimwa afya ya akili kila mara,” amesema Heche.

Alipoulizwa  hoja anayowasilisha itaungwa mkono na wabunge wote kutokana na uchachewa wabunge wa upinzani Heche alijibu;

“Mwisho wa siku wananchi walio wengi ndio wenye uamuzi wa kuipinga hoja ya msingi inayoungwa mkono na wananchi,  lazima watakuadhibu  kwa hiyo wataoipinga watakutana na Mahakama ya wananchi huku nje kwenye uchaguzi,” anasema.

Hata hivyo, Heche ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), hakuwa tayari kusema ni kikao gani ataiwasilisha hoja hiyo zaidi ya kusema hivi kwa sasa macho yake yapo katika matibabu ya Tundu Lissu na kwamba akirudi nchini atatoa taarifa za kina.

“Nikirudi nitasema lakini kwa sasa nguvu na jitihada zetu zote ni kuhakikisha tunamsaidia Mh Lissu kupona,” anasema.

 

LEMA: Mwigulu na Sirro Mnataka Tufanye Nini Juu ya Lissu??

Leave A Reply