Mpango Haramu Tanasha, Mobeto Kuvuruga Ndoa ya Mondi

Baada ya hivi karibuni Mwanamama anayefanya poa kwenye gemu la muziki nchini Kenya na mzazi mwenza wa mwanamuziki mkubwa wa Afro-Pop, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Tanasha Donna Oketch, kutangaza kukutana na mwanamitindo, mwanamuziki na mjasiriamali wa Bongo, Hamisa Mobeto na watoto wao, imeelezwa nyuma yake kuna mpango haramu.

 

Imeelezwa kuwa, mpango huo unalenga kuvuruga ndoa ya Diamond au Mondi, ambaye ni mzazi mwenzao, inayotarajiwa kufungwa Oktoba 2, mwaka huu. Mara baada ya taarifa hizo kutoka kwa Tanasha, mashabiki wao wameonesha kulijadili suala hilo mitandaoni, kwa kusema kuwa, ukaribu wa wawili hao, unalenga kupindua ndoa ya Mondi kwa kuweka shughuli yao siku hiyohiyo.

 

“Unajua siku zote wanawake ni viumbe wa ajabu sana, hawa wazazi wenza wa Mondi waliposikia tu jamaa anafunga ndoa mwaka huu, tena mwezi wa kumi, nao wakapanga mpango wa kukutana siku hiyohiyo na kufanya jambo lao,’’ anasema shabiki mmoja.

Tanasha ambaye amezaa mtoto mmoja na Mondi, amekiambia kituo kimoja cha televisheni jijini Nairobi, Kenya kuwa, ana mpango wa kuwakutanisha mwanaye Naseeb Junior na Abdul Nasibu ‘Dyllan’ ambaye ni mtoto mwingine wa jamaa huyo aliyezaa na Mobeto.

 

Tanasha amesema kuwa, jambo hilo atalifanya siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa (birthday) ya mwanaye Naseeb ambayo ni Oktoba 2, mwaka huu, siku ambayo Mondi ametangaza kufunga ndoa.

 

Akimzungumzia Mobeto ambaye naye ni mzazi mwenza wa Mondi, Tanasha alikuwa na haya ya kusema; “Hamisa (Mobeto) amekuwa ni mtu ambaye ninakubali kazi zake, maana ni mchapakazi na ana upendo. Hivyo nimepanga kuwakutanisha watoto wetu, maana wao ni ndugu wa baba mmoja.

 

“Watoto wetu wamekuwa wakizungumza kwenye video call mara nyingi tu,’’ amesema Tanasha ambaye alitengana na Mondi mapema mwaka huu. Tanasha alipoulizwa kuhusiana na kukutana na Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ ambaye naye amezaa watoto wawili na Mondi, Tiffah Dangote na Nillan, alisema yeye si mtu wa kuhifadhi vinyongo.

 

“Kuhusiana na kukutana na Zari, ni muda tu ukifika na yeye akiwa tayari nitafanya hivyo, najua ni jambo muhimu na hakuna sababu ya sisi kuchukiana kwa kuwa wote tumezaa na mwanaume mmoja (Mondi). Ni muhimu kwa mwanangu kukutana na ndugu zake, maana inaweza kufika siku akaniuliza.

 

“Sijali sana kuhusu kuweka vinyongo, napenda kutafuta amani maana kikubwa ni kuwakutanisha watoto, kwa sababu mimi huwa ninamtanguliza mtoto mbele, mambo yangu baadaye,’’ alisema Tanasha.

 

Tanasha, Zari na Mobeto ni wazazi wenza wa Mondi na wamemzalia mwanamuziki huyo watoto wanne ambao ni; Tiffah Dangote, Nillan, Dyllan na Naseeb Junior.

 

Mbali na hilo, Tanasha amekuwa karibu mno na Mobeto, kwani wamekuwa wakishirikiana kwenye kazi zao za kisanaa na hata kuwasiliana na kupostiana kwenye mitandao ya kijamii.

Stori: Happyness Masunga, Dar

Toa comment