The House of Favourite Newspapers

‘Mpemba wa Magufuli’ Aandika Barua Kukiri kwa DPP

MFANYABIASHARA Yusufu Ally, maarufu kwa jina la Mpemba wa Magufuli na wenzake,wanaokabiliwa na mashitaka ya uhujumu uchumi ikiwemo kujihusisha na biashara ya meno ya tembo, wameandika barua kwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) kuomba kukiri mashitaka yao hayo.

 

Katika kesi hiyo, mbali ya Mpemba,  washitakiwa wengine ni Charles Mrutu, Benedict Kungwa, Jumanne Chima, Ahmed Nyagongo na Pius Kulagwa.

 

Wakili wa Serikali, Elizabeth Mkunde,  amemueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba,  kwamba washitakiwa wameshaandika barua hivyo, na wanaomba mahakama iwape muda kwa ajili ya kuingia katika makubaliano.

 

Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 16, mwaka huu 2019 kwa ajili ya kutajwa.

Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka manne ya kujihusisha na biashara ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh milioni 785.6.

 

Inadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Januari, 2014 na Oktoba, mwaka huu wakiwa Dar es Salaam, Tanga, Iringa na Mtwara, walijihusisha na mtandao wa ujangili kwa kukusanya na kuuza nyara za serikali ambazo ni vipande vya meno ya tembo 50 vyenye thamani ya Dola za Marekani 180,000 sawa na Sh milioni 392.8 bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.

 

Pia inadaiwa Oktoba 26, mwaka huu, washitakiwa hao wakiwa Mbagala-Zakhem jijini Dar es Salaam, walikutwa na vipande vya meno ya tembo 10 vyenye uzito wa kilo 13.85 vya thamani ya Dola za Marekani 30,000 sawa na Sh milioni 65.4.

 

Wanadaiwa pia kuwa Oktoba 27, mwaka huu, wakiwa Tabata Kisukuru washitakiwa hao walikutwa na vipande vinne vya meno hayo ya tembo yenye uzito wa kilo 11.1 na thamani ya Dola za Marekani 15,000 sawa na Sh milioni 32.7 .

 

Pia, Oktoba 29, mwaka huu walikutwa na vipande 36 vya thamani ya Sh milioni 294.6 bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Comments are closed.