MPENZI WAKO ANAKUOMBA SANA FEDHA ?

 HII INAKUHUSU Ipo dhana iliyojengeka kwenye vichwa vya watu wengi, wanaume kwa wanawake kwamba unapokuwa na mpenzi ambaye mara kwa mara anakuomba fedha, tambua kwamba hana mapenzi na wewe ila yupo kimaslahi zaidi.Utawasikia wanaume wakielezana kwamba siku hizi unaweza kuanzisha uhusiano na mwanamke unayempenda lakini baada ya muda mfupi sana, ataanza kukuomba fedha, ataibuka na matatizo chungu nzima ambayo yote yanahitaji fedha kwa lengo la ‘kukupiga mizinga’.

Wanachokiamini wengi ni kwamba mwanamke wa aina hii hafai kabisa na unatakiwa kumuepuka mapema. Kwa wanawake ambao nao kidogo wanajiweza kiuchumi, nao wamekuwa wakiamini kwamba mwanaume anayependa kukuombaomba fedha, hana mapenzi ya dhati na wewe na kinachomfanya awe karibu na wewe, si mapenzi bali ni kwa sababu anaangalia maslahi yake.

Siku chache zilizopita, nilipokea ujumbe kutoka kwa moja kati ya wasomaji wangu wa siku nyingi. Huyu dada aliniambia yeye anaishughulisha na biashara lakini tatizo kubwa ambalo amekuwa akikumbana nalo, kila anapoanzisha uhusiano, wanaume anaokuwa nao wanakuwa wanamuomba sana fedha mpaka inafika mahali anaamua kuachana nao. Wiki chache zilizopita pia nilipigiwa simu na msomaji mwingine ambaye aliniambia kwamba kuna mwanamke anampenda sana lakini tatizo lake, anamuomba sana fedha, yaani haziwezi kupita siku mbili tatu bila kuja na shida ambayo inahitaji fedha.

Jambo ambalo unatakiwa kulielewa, ni kwamba mapenzi ni kusaidiana. Unapompenda mtu fulani, bila kujali kama wewe ni mwanaume au mwanamke, ule moyo wa upendo unakufanya utamani kumuona akiwa na furaha. Wakati mwingine hata kama hujaombwa, ukimuona mtu unayempenda anahitaji kitu fulani, ule upendo utakusukuma kumtimizia kwa moyo mweupe kabisa! Ndiyo, kwa sababu unataka afurahi. Kwa mwanaume, unapokuwa kwenye uhusiano na mwanamke, tayari linakuwa ni jukumu lako kumtimizia mahitaji yake mbalimbali.

Ni makosa kwa mwanaume kulalamika kwamba eti mpenzi wake anakuomba sana fedha, kwa hiyo ulitaka akiwa na shida aende ‘kudanga’ mitaani au akamuombe nani kama siyo wewe? Kama unao uwezo wa kumsaidia, msaidie tena bila kuhesabu wala kunung’unika.

Lakini pia kama wewe mwanamke ndiye mwenye uwezo kuliko mwenzako, bado hakuna tatizo lolote kwa wewe kumsaidia kwa sababu leo wewe unaweza kuwa nazo lakini hujui miezi michache baadaye hali yako itakuwaje. Yawezekana yuleyule uliyekuwa unamuona kama ni mzigo kwako, ndiyo akaja kukusaidia.

Penzi la kweli halina masharti, wala halihesabu gharama, ukiamua kumpenda kwa dhati, muoneshe kwa hali na mali kwamba unampenda, isiwe ‘I love you’ zinaishia mdomoni tu lakini unapotakiwa kumgharamia unaanza kukunja sura, mapenzi hayapo hivyo.

Lakini pia, kwa wewe unayependwa, isiwe kwa sababu unajua kwamba mtu fulani anakupenda basi ndiyo iwe sababu ya kuwa kila dakika unampiga ‘mizinga’ tu, mfanye ajisikie amani kukusaidia kwa kadiri ya uwezo wake lakini isiwe kama unamlipisha kwa sababu anakupenda. Kwa leo ni hayo tu, tukutane tena wiki ijayo.

 


Loading...

Toa comment