The House of Favourite Newspapers

Mpenzi Wako Anapokusaliti, Lazima Ujifunze Kitu

vegeterians-couple-bedMpenzi msomaji wangu, bila shaka uko poa kabisa, bila kukupotezea muda wako twende moja kwa moja kwenye mada ambayo nimekuandalia leo, inazungumzia juu ya usaliti, jinsi ambavyo maisha yetu yanaendelea baada ya kukumbana na maumivu ya kusalitiwa.

Uchunguzi nilioufanya ambao ulikuwa ni pamoja na kuzungumza na marafiki pamoja na wasomaji ambao nimekuwa nikiwasiliana nao mara kwa mara, unaonyesha kuwa asilimia 66 ya watu hao wamekumbana na maumivu ya usaliti. Ni asilimia 34 tu ambao wamedai hawayafahamu kabisa maumivu ya kusalitiwa zaidi ya kuyasikia kutoka kwa watu wengine.

Hilo ni suala la bahati sana kwenye dunia yetu tunayoishi zama hizi iliyotawaliwa na vishawishi vingi pia ni jambo la kumshukuru Mungu, hata hivyo swali linabaki palepale, kwa wale ambao wamesalitiwa wamejifunza jambo gani?

Kwenye suala zima la uhusiano wa mapenzi uzoefu unaonyesha kuwa watu wengi huacha kuwa waaminifu pale inapotokea wanasalitiwa na wapenzi wao waliokuwa wanawaamini sana. Huona dunia nzima hakuna mwanaume au mwanamke muaminifu, wote ni wasaliti na hupoteza ari ya kuwa waaminifu.

Lakini napenda kuwakumbusha wasomaji wangu kuwa kila usaliti unasababu zake. Hakuna usaliti unaotokea tu bila kuwa na sababu. Ukijaribu kuangalia utagundua kuwa pengine ni tamaa, kipato, mvuto na vitu vingine vingi ambavyo husababisha kutokea kwa suala hili.

Sasa tunatakiwa kujifunza nini? Suala muhimu la kujifunza inapotokea umesalitiwa kabla ya kujenga akilini mwako taswira kuwa wanawake au wanaume wote si waaminifu ni kuchunguza mazingira yaliyosababisha mpenzi wako kukusaliti.

Angalia kwa namna moja au nyingine kama pia unahusika kuchangia jambo hilo kutokea. Ukigundua kuwa unahusika hutakiwi kujilaumu badala yake beba udhaifu wako ili uwe tayari kusahihisha makosa hayo wakati mwingine. Hiyo ni elimu tosha kwako, pia hapo unatakiwa kufahamu jambo la msingi kuwa mpenzi wako uliyemuamini ameshindwa kuubeba udhaifu wako na kukulindia heshima hata asikusaliti.

Sasa hapo kuhusu suala zima la msamaha ni wewe mwenyewe mwenye uamuzi juu ya hilo kutokana na mazingira ya tukio lenyewe, lakini ninazidi kusisitiza kabla ya uamuzi wowote ni muhimu tukio hilo likupe elimu ya kukusaidia katika maisha yako ya kimapenzi, isije ikajirudia tena ukasalitiwa kutokana na udhaifu huo.

Ni imani yangu kuwa unapouruhusu moyo na akili yako kukubali kujielimisha ni rahisi kuepuka mtazamo hasi ndani ya akili yako jambo ambalo litakusaidia mno katika maisha yako ya uhusiano yanayoendelea mbele baada ya kutokea tukio hilo.

Comments are closed.