The House of Favourite Newspapers

Mpenzi Wangu Sarafina-01

MTUNZI: Nyemo Chilongani

SIMU: 0718069269

 

“Jamani leo natangaza rasmi….” alisikika jamaa mmoja akiwaambia wenzake.

“Tangaza…” wenzake walisema huku wakicheka.

“Kuanzia leo kwa hapa chuo, hakuna demu mkali kama yule Msukuma…” alisema jamaa huyo.

“Msukuma gani?” aliuliza jamaa mmoja huku akimwangalia mwenzake huyo aliyeamua kutangaza.

“Sarafina Butati! Yaani hakunaga!”

“Hahaha!” watu wote wakajikuta wakicheka.

“Jamani yule mtoto mkali! Jamani yule mtoto anaita! Jamani yule mtoto ana figa! Jamani! Jamani! Jamani! Nasema hivi! Kwa hapa chuo hakuna demu mkali kama Sarafina,” alisema jamaa huyo.

“Anamshinda Manka wa Kichaga?” aliuliza jamaa mwingine.

“Manka! Hivi yule demu anaingia kwa Sarafina? Hivi ushawahi kuvuta picha kichwani mwako ukamuona Sarafina akiwa mtupu? Yule mtoto jamani ni mkali sana, kuna kila haki ya sisi marijali kumpigia misele,” alisema jamaa huyo na wote kuanza kucheka.

Huyo ndiye msichana aliyekuwa gumzo katika Chuo cha Amazon kilichokuwa Temeke jijini Dar es Salaam. Kila mwanaume aliyekuwa katika chuo hicho cha ufundi alivutiwa na msichana huyo, uzuri wake uliwapagawisha wanaume wengi kiasi kwamba kila mmoja alimtolea macho.

Sarafina alikuwa msichana mrefu, mwenye mwendo wa maringo, alikuwa na hipsi pana ambazo kwa watoto wa mjini walipenda kuziita pisto, alikuwa na miguu iliyojazia kidogo huku akiwa na mapaja manene kiasi kwamba kila alipoyaruhusu yaonekane, kila mwanaume aliyamezea mate.

Usoni hakuwa wa kawaida, alikuwa na sura nyembamba, mdomo wake ulikuwa na lipsi pana, hata kama macho yake alikuwa akiyakaza, bado yalionekana kusinzia kwa mbali mithili ya mwanamke aliyekula kungu.

Mashavuni mwake alikuwa na vishimo viwili ambavyo viliufanya uzuri wake kuonekana kila alipokuwa akicheka hata kutabasamu. Hakuwa msichana wa kusuka, muda mwingi nywele zake alikuwa akizikata huku sura yake hiyo akiipendezesha na miwani meusi.

Sarafina hakujua kutembea kwa kasi, kila alipokuwa akitembea, alitembea kwa mwendo wa maringo kana kwamba hakuwa akikanyaga ardhi hiihii. Aliwadatisha wanaume wote waliokuwa chuoni hapo, kila mmoja alimpenda, kila mmoja alitamani hata siku moja msichana huyo mrembo awe mpenzi wake.

Sauti yake ilikuwa nyororo, kipindi cha kwanza wanaume wengi walihisi kwamba msichana huyo alikuwa akifanya kusudi lakini baada ya kumzoea wakagundua kwamba hiyo ilikuwa ndiyo sauti yake ya kila siku, sauti ya kumtoa nyoka pangoni, sauti iliyowadatisha hata wanaume waliokuwa mbali waisikiapo kutaka kumuona msichana huyo aliyeitoa sauti hiyo.

Sarafina alikuwa na sifa ya kuwa msichana mrembo, hakuonekana kuwa na kasoro, kila alipopita, alikuwa gumzo, wanaume walimsifia kwa kuwa alikuwa na mvuto wa ajabu.

Japokuwa alikuwa mzuri na wa kuvutia sana lakini Sarafina hakuwa mtu wa maringo, alipenda kuzungumza na kila mtu, wanaume wengi wakatumia nafasi hiyohiyo kumtongoza lakini msichana huyo hakuwa mwepesi kuingilika kama wasichana wengine, hakuwa msichana mwepesi hata kidogo.

Wanaume waliteseka, walihangaika, ikafika kipindi wakahisi kwamba inawezekana msichana huyo alipenda mwanaume aliyekuwa na gari, waliokuwa na magari wakamfuata kwa lengo la kumuingiza katika mitego yao lakini hawakufanikiwa.

Wengine wakahisi kwamba msichana huyo alihitaji pesa, wanaume wakajipanga vilivyo, wakamfuata huku mifuko ikiwa imejaa lakini msichana huyo hakuingilika, hakuwakubalia, kwake, hakujali pesa wala magari.

Wanaume hawakuchoka, kila mmoja alikuwa na uhakika wa kumpata msichana huyo kama tu wangeweza kuweka nguvu zao katika ufuatiliaji. Kitu walichokifanya ni kuanza kumtumia zawadi mbalimbali msichana huyo.

Hilo halikutosha, halikubadilisha moyo wake, aliendelea kuwa na msimamo uleule kwamba hakutaka kuingia kwenye uhusiano na mwanaume yeyote yule, kitu alichokuwa akikitaka ni kusoma na kufikia malengo yake.

Alikwenda Dar es Salaam kwa ajili ya kusoma chuo. Hakuzaliwa katika familia yenye uwezo mkubwa sana jijini Mwanza, ilikuwa familia ya kawaida iliyokuwa na maisha ya kawaida sana ambayo ilikuwa ikiishi katika mtaa wa kimasikini, mtaa choka mbaya wa Mabatini hapohapo Mwanza.

Alipomaliza kusoma katika Shule ya Sekondari ya Mwanza, wazazi wake wakakopa pesa katika kikoba cha Saccos moja kwa ajili ya Sarafina na kuelekea jijini Dar es Salaam kusoma, walipopewa, wakamlipia ada ya mwaka mzima na kumpa fedha nyingine kwa ajili ya maisha yake huko.

Sarafina alipofika chuoni, alionekana kuwa msichana wa kawaida, hakuonekana kama alikuwa na mvuto lakini baada ya kukaa kwa miezi sita, wanaume wakaona utofauti, uzuri wake wa asili ukaanza kuonekana.

Mpaka kipindi hicho, Sarafina hakuwahi kumjua mwanaume, alikuwa msichana bikira ambaye alijiapiza kwamba mwanaume wa kwanza ambaye angempa nafasi ya kuutoa usichana wake ndiye ambaye angekuwa mume wake.

Alijitunza, kila siku aliwakatalia wanaume, japokuwa alifuatwa sana lakini hakuchoka kuwakataa wanaume, kwake, bado ndoto yake ya kuolewa akiwa bikira iliendelea kuishi moyoni mwake, hakuwapenda wanaume wenye magari, hakuwapenda wanaume wenye pesa, alichokuwa akikihitaji ni kumpata mwanaume mwenye uwezo wa kawaida ambaye angemuonyeshea mapenzi ya dhati, mwanaume ambaye angemwambia ‘Nakupenda’ kila siku asubuhi na usiku.

“Sara! Unajua wewe ni mzuri sana!” alisema mwanaume mmoja, aliamua kumfuata Sarafina kama walivyokuwa wenzake.

“Umekwishaniambia sana Jumanne!”

“Nimetokea kukupenda bure!”

“Kwani wote wanaonipenda wananipenda na hela?” aliuliza Sarafina huku akitoa tabasamu lililompa matumaini mengi Jumanne.

“Hahah! Sarafina! U mzuri sana, hebu angalia jinsi unavyotabasamu, dimpozi zako zinaniua kishenzi, hakika nimeona wanawake wengi warembo lakini kwako! Haki ya Mungu hakuna kama wewe,” alisema Jumanne huku akitoa tabasamu ambalo aliamini kwamba lingemchanya msichana huyo.

“Nashukuru! Naomba niondoke.”
“Kwa hiyo?”
“Kuhusu nini? Si umeniita, nimekuja, umenisifia, nimekubali!”
“Ila sijamaliza.”
“Basi malizia!”
“Nakupenda.”
“Nashukuru! Kingine?”
“Ningependa uwe mpenzi wangu!”

“Haiwezekani Jumanne.”
“Sarafina, pamoja na tabasamu lako lote bado unanikataa?”
“Kwani tabasamu ndiyo kupendwa? Si kila tabasamu ni la furaha Jumanne. Mwingine anatabasamu lakini moyo wake unawaka moto. Naomba unielewe, sihitaji kuwa na mwanaume yeyote yule,” alisema Sarafina, tayari alisimama pale alipokuwa, hakutaka kuongea tena, huyo akaondoka zake.

Jumanne alibaki akiwa amekaa kitini, hakuamini kama kweli alimkataa, alikwishajigamba kwa wenzake kwamba angempata Sarafina kwa gharama zozote zile, waliwekeana dau lakini mwisho wa siku msichana huyo alimkataa huku akimtolea tabasamu pana.

Moyo wake uliuma, ulichoma mno, hakutaka kukubali, aliendelea kumfuatilia msichana huyo lakini hakukuwa na kilichobadilika, kama ulivyokuwa msimamo wake kipindi cha nyuma ndiyo ukawa uleule kwamba hakutaka kuwa na mwanaume yeyote yule.

“Nitaendelea kuwa bikira mpaka nitakapoolewa. Mwanaume wangu wa kwanza kumvulia nguo atakuwa mume wangu,” alisema Sarafina huku akiwa kitandani. Usingizi ukampitia.

 

Je, nini kitaendelea?

Tukutane Jumamosi mahali hapa.

Comments are closed.