The House of Favourite Newspapers

MPENZI WANGU SARAFINA-02

MTUNZI: NYEMO CHILONGANI

Miongoni mwa wanaume waliokuwa wakimpenda Sarafina alikuwa kijana Richard Lema. Huyu hakumpenda msichana huyo kipindi hicho tangu siku ya kwanza alipokanyaga katika chuo hicho alitokea kumpenda kwani kila alipomwangalia, aliuona uzuri wa msichana huyo japokuwa hakuwa amelizoea jiji.

Richard alikuwa miongoni mwa watoto wa matajiri wakubwa jijini Dar es Salaam, alikwenda kusoma katika chuo hicho kwa sababu tu hakutaka kuishi maisha ya kifahari, siku zote alijihesabia kuwa mtu wa kawaida, kijana aliyetoka katika familia nyingine ya kimasikini.

Hakukuwa na mtu aliyejua maisha halisi yake, kila siku chuoni hapo alikuwa akienda kwa daladala, alikuwa na gari la kifahari nyumbani kwao lakini hakutaka mtu yeyote afahamu kama alikuwa mtoto wa kitajiri na hata marafiki zake walipotaka kumtembelea, aliwaita katika chumba alichopanga uswahilini Tandale.

Kila siku alipokuwa akimwangalia Sarafina, mapigo yake ya moyo yalikuwa yakidunda mno, alimpenda msichana huyo, alitamani sana kumfuata na kumwambia ukweli kwamba alikuwa akimpenda kwa moyo wote lakini aliogopa, hakujiamini, hakuwahi kuzungumza na msichana yeyote yule.

Hata uzuri wa msichana huyo ulipoanza kuonekana, bado alikuwa kwenye mapenzi ya dhati, alimpenda sana lakini kumfuata na kumwambia ukweli wa moyo wake lilikuwa jambo gumu sana kufanyika, aliendelea kuumia kila siku, aliendelea kuteseka lakini kufumbua mdomo wake na kumwambia msichana huyo ukweli, hakuthubutu kabisa.

“Nitamwambia tu! Lakini lini? Mbona nateseka tu kila siku?” alijiuliza lakini akakosa jibu kabisa.

Siku zikaendelea kukatika, idadi ya wanaume waliokuwa wakimpenda msichana huyo ikaongezeka, Richard alichukia, aliumia, alitamani kuwasimamisha wanaume wote kwa kuwaambia wasimfuate msichana huyo lakini ilishindikana, kila siku idadi ya wanaume hao iliendelea kuongezeka zaidi.

Baada ya kukaa kwa mwaka mzima chuoni ndipo alipoamua kujipanga, akatafuta siku maalumu ya kumwambia msichana huyo ukweli, hakutaka kuvumilia, kama kulikuwa na watu wanakataliwa, basi hata naye alitakiwa kujaribu bahati yake na kama ingetokea kukataliwa, isingekuwa mara ya kwanza.

“Ila ninaogopa! Mungu! Naomba unitie ujasiri,” alisema Richard, siku hiyo ilipofika, akaamua kumfuata msichana huyo.

***

Richard hakutaka kuvumilia, hakuwa radhi kuuona moyo wake ukiteseka na wakati mtu ambaye angempa pumziko alikuwepo katika dunia hii. Hakutaka kusubiri, aliogopa kuchoka na hivyo akapanga siku ya kumfuata Sarafina kwa ajili ya kumwambia ukweli jinsi moyo wake ulivyojisikia.

Alijipanga sana, muda wa kutoka darasani, akaanza kujivutavuta kwa ajili ya kuzungumza na Sarafina. Hakuwa na nafasi, wakati yeye akitaka kumsogelea msichana huyo mrembo na kumwambia ukweli, tayari wanaume wawili walimuwahi na kuanza kuzungumza na msichana huyo.

Moyo wake uliumia mno, siku hiyo aliitenga kwa ajili ya msichana huyo, hakuamini kama ingeshindikana kabisa kuzungumza naye. Akavumilia, akasubiri wale wamalize kuongea naye lakini cha ajabu wanaume hao walimng’ang’ania kama ruba.

Mpaka inafika saa kumi na moja alipokuwa akiondoka, wanaume hao wakaondoka naye. Alikasirika sana lakini hakuwa na jinsi, akaondoka mpaka nyumbani kwao, akaingia chumbani na kuwa na kujilaza kitandani.

Alikuwa mtoto wa bilionea mkubwa ambaye alitokea kumpenda msichana Sarafina. Utajiri mkubwa aliokuwa nao baba yake ulionyesha dhahiri kwamba hakuwa na hadhi ya kuwa na msichana kama Sarafina, alitakiwa kuwa na msichana aliyekuwa na hadhi kubwa, msichana ambaye kwenda Marekani, Italia ilikuwa ni sawa na kwenda Kariakoo.

Hakutaka kujali hilo, alipomfuata, utajiri wake aliuweka pembeni, aliyatanguliza mapenzi kwani aliamini kwamba pesa zisingeweza kununua mapenzi, hata kama angekuwa na pesa kiasi gani angeishia kununua ngono na si upendo.

“Kwa nini inakuwa hivi? Wale ni wakina nani? Kwa nini wanamng’ang’ania sana?” alijiuliza Richard pasipo kupata jibu.

Wivu mkali ukaukamata moyo wake, huo haukuwa mwisho, ulikuwa ni kama mwanzo wa harakati zake, aliendelea kumfuatilia lakini wanaume walewale hawakutaka kumuacha, kila siku walikuwa naye, walizungumza naye sana mpaka akawa anakasirika.

“Hawa ni wakina nani?” alijiuliza.

Hapo ndipo alipoanza kufuatilia, alitaka kuwajua wanaume wale walikuwa wakina nani na walihitaji nini kwa Sarafina. Kwenye kufuatilia kwake akagundua kwamba wanaume hao walikuwa marafiki wakubwa, mmoja aliitwa David Kimario, mwanaume aliyekuwa akitingisha kwa kuzifunua sketi za wanawake na mwingine alikuwa Paschal Malengo ambaye huyo alikuwa muonganishaji mkubwa aliyekuwa akitumiwa na David.

Japokuwa David alikuwa bingwa wa kutembea na wasichana wengi lakini kwa Sarafina alifua dafu, alijitahidi sana kumtongoza lakini alimkatalia kumtumia Paschal ambaye alijua sana kucheza na akili za wasichana.

Kitendo cha kuwa na Sarafina kila siku, Paschal alijitahidi kumuweka sawa, alijitahidi kuulainisha moyo wa msichana huyo ukubaliane na David ambaye alikufa na kuoza moyoni mwake.

“Kumbe! Kwa staili hii sitoweza kuongea naye, ngoja nitafute namba yake ya simu,” aliwaza.

Hilo ndilo alilolifanya, akaitafuta namba ya msichana huyo. Kuipata haikuwa kazi kubwa, watu wengi walikuwa nayo, alipoipata tu, akatafuta siku na kumpigia simu kwa lengo la kuonana naye.

“Wewe nani?” aliuliza Sarafina.

“Richard!”
“Okey! Nikusaidie nini Rich?” aliuliza Sarafina.

“Ningependa nionane na wewe!”
“Ili?”

“Nizungumze na wewe!”
“Kuhusu?”
“Stori tu!”
“Samahani! Sina muda kaka yangu!”
“Saraf….”

“Naomba unielewe! Sina muda!” alisema Sarafina na kisha kukata simu.

Moyo wa Richard ukauma vilivyo, akanyong’onyea, akajilaza kitandani na kuanza kumfikiria msichana huyo. Alijua kwamba alikuwa na muda wa kutosha wa kuonana naye lakini hakutaka kwa kuwa hakumfahamu, hakujua ni kwa jinsi gani alikuwa akimpenda.

Hakutaka kukubali, kwa kuwa alimpigia simu, alichokifanya ni kumtumia meseji. Ilikuwa vigumu sana kujibiwa, alipofikisha meseji ya ishirini ndipo akatumiwa meseji fupi tu iliyosomeka ‘Nalala’.

“Uwe na usiku mwema!” alimalizia kwa kumtumia na msichana huyo hakujibu kitu chochote kile.

Kwa jinsi mapenzi yalivyouendesha moyo wake, usiku mzima alibaki akiiangalia meseji ile ya ‘Nalala’ aliyoandikiwa na msichana yule. Moyo wake ulifarijika, hakuumia kwa kumtumia meseji ishirini na zote hazikujibiwa, kitendo cha kuambiwa meseji moja iliyomaanisha kwamba hakutakiwa kutuma meseji yoyote, moyoni mwake akaridhika.

Hakukoma, hata siku iliyofuata aliendelea kumtumia meseji lakini hakuwa akijibu mpaka alipotumiwa meseji nyingi mno. Hayo ndiyo yalikuwa maisha yake na baada ya wiki mbili, ili kuepuka usumbufu, Sarafina akakubaliana na Richard na kuonana naye.

“Tuonane wapi?” aliuliza Sarafina.

“Nakusikiliza wewe tu! Ila mimi naishi Tandale, sasa unaweza kuangalia sehemu rahisi ya mimi na wewe kuonana,” alisema Richard.

“Kule Tandale kwa vibaka?”
“Ndiyo hukohuko, mabonde kuinama kulipojaa roba za mbao!” alijibu Richard.

“Mmh!”

“Ungependa tuonane wapi?”
“Serena hotel”
“Mmh!”
“Mbona unaguna!”
“Nitaweza kugharamia jamani! Kule maji si yatakuwa shilingi elfu kumi! Nitaweza kweli?” aliuliza Richard, wakati huo walikuwa wakizungumza.

“Sasa wewe unamfuata msichana mzuri halafu huna hela?”

“Basi sawa. Sipendi kuacha kuonana na wewe! Nitajitahidi nifike huko,” alisema Richard na hivyo kupanga kuonana siku hiyo saa kumi na moja jioni.

Saa tisa na nusu tayari Richard alikuwa mahali hapo, alivalia simpo, kama kawaida yake hakutaka kwenda na gari lake la kifahari, alichukua daladala ambayo ilimshusha Akiba na kuchukua Bajaj iliyompeleka mpaka katika Hoteli ya Serena na kuingia ndani, sehemu ya mgahawa na kuagiza soda.

“Nimekwishafika!” alisema Richard.

“Sawa. Niandalie chakula. Mbuzi wa kuchoma, chipsi na soseji nne!” alisikika Sarafina.

“Mmh!”

“Mbona unaguna! Au niahirishe?”
“Hapana! Wewe njoo!”

Kwa kipindi kichache tu Sarafina alivyoanza kuzoeana na kina David alibadilika. Maneno matamu aliyokuwa akiambiwa na Paschal kuhusu David yalimteka. Moyo wake ukabadilika, matumizi makubwa waliyokuwa wakitumia wanaume hao pamoja naye akaona kwamba kila mwanaume aliyekuwa akija mbele yake ilimbidi kuwa na fedha za kutosha.

Alikumbuka kwamba alitoka kwenye familia iliyokuwa na umasikini mkubwa, kitendo cha David kuwa radhi kutoa kiasi chochote cha fedha kuhakikisha anampata kikamlevya Sarafina na kugundua kwamba pesa ilikuwa kila kitu katika maisha yake.

Hakuwahi kumuona Richard, hakuwa akimpenda ila alichokuwa akikitaka ni kutumia pesa zake tu. Alijua kwamba hakuwa na fedha kwa sababu hata mtaa aliokuwa akiishi ulikuwa ni walala hoi hivyo alimwambia vitu ambavyo aliamini kwamba asingeweza kuvitimiza hata mara moja.

Baada ya dakika kadhaa, Sarafina akafika mahali hapo. Richard alipomuona akiingia, hakutaka kubaki kitini, kwa heshima akasimama na kumkaribisha msichana huyo ambaye akatulia kitini. Kabla ya kufanya kitu chochote kile, Richard akamuita dada wa chakula na kumwambia kuhusu ile oda aliyokuwa ameiweka, mwenyewe alikuwa amefika.

“Karibuni sana,” alisema dada wa chakula huku akiweka chakula mezani.

“Ahsante sana,” alisema Richard huku akiwa na maji tu, akajifanya kutokuwa na fedha kabisa.

Richard alibaki akimwangalia Sarafina. Kwa jinsi alivyokuwa akionekana siku hiyo, alionekana kuwa tofauti na Sarafina aliyekuwa akimfahamu. Alibadilika, muonekano wake ulikuwa ni wa tofauti sana.

Kichwani alikuwa na mtindo mpya wa nywele, alizinyoa nywele zake kwa mtindo wa kiduku kwa mbali huku akiwa amezipaka blichi iliyomfanya kuonekana tofauti kabisa huku puani akiwa na kipini kilichosindikizwa na tattoo iliyokuwa kifuani mwake, pembeni kidogo ya titi lake. Japokuwa alikuwa na mabadiliko makubwa mwilini mwake lakini Richard hakuacha kumpenda msichana huyo, kwake, bado aliendelea kuwa namba moja moyoni mwake.

“Sarafina!” alimuita.

“Niambie! Umesema unaitwa nani vile?”
“Richard!”
“Ooh! Okey! Niambie Richard!”

Richard akavuta pumzi ndefu, akamwangalia msichana huyo, akashusha pumzi, kilichomuuma ni kwamba Sarafina hakulifahamu jina lake, alijiona kupuuzwa sana, alijiona kutokujaliwa na msichana huyo na ndiyo maana alisahauliwa jina lake japokuwa alikuwa akiwasiliana naye sana tu.

Richard hakutaka kujificha, aliteseka kwa kipindi kirefu moyoni mwake hivyo kumwambia jinsi alivyokuwa akimpenda. Sarafina alibaki kimya, alikuwa akimwangalia Richard na kumsikiliza kila neno alilokuwa akizungumza.

Kwa muonekano wake, mwanaume huyo alionekana kumpenda sana lakini kitu kilichompa wakati mgumu Sarafina ni kwamba hakuwa mwanaume wa ndoto yake, alitoka kwenye familia ya kimasikini, alitakiwa kuitoa familia yake kutoka pale ilipokuwa, kitendo cha kuwa na mwanaume masikini kama Richard kilimaanisha kwamba angeyafanya maisha yake kuwa vilevile.

“Unanipenda mimi?” aliuliza Sarafina.

“Ndiyo! Ninakupenda sana kutoka moyoni mwangu!” alijibu Richard huku akimwangalia kwa jicho lililomaanisha upendo mkubwa aliokuwa nao moyoni mwake.

“Daah!”
“Kuna nini tena?”
“Umechelewa!”
“Najua kwamba msichana mrembo kama wewe huwezi kuwa singo! Ila naomba unifikirie! Sarafina, ninakupenda, wewe ni msichana unayeufanya moyo wangu kutetemeka, ni msichana ambaye naamini nikiwa na wewe nitakuwa na furaha, amani moyoni mwangu,” alisema Richard huku akimwangalia Sarafina.

“Siwezi kuwa na wewe!”
“Kwa nini?”

“Richard! Mimi si hadhi yako! Samahani! Sikudharau ila ni bora nikwambie ukweli, halafu mbali na hilo, nina mpenzi!” aljibu Sarafina.

“Una mpenzi?”
“Ndiyo! Anaitwa David! Yule mwanaume ninayekuwa naye sana chuoni,” alisema Sarafina.

Hakukuwa na kitu kilichowahi kuuchoma moyo wake kama kuyasikia maneno hayo. Alihisi kitu kama msumari wa moto ukiuchoma moyo wake vilivyo. Akayafumba macho yake, akakiinamisha kichwa chake chini, alipokiinua, machozi yakaanza kujikusanya machoni mwake.

“Sarafina! Ninakupenda kupita kawaida, ninaomba niwe nawe. Nimepoteza muda wangu kwa ajili yako, nimekuwa nikikufikiria sana. Sarafina, ninakupenda, ninakupenda zaidi ya unavyofikiria, ninakupenda zaidi ya David anavyokupenda, ninakupenda kuliko mwanamke yeyote chini ya jua,” alisema Richard huku kwa mbali machozi yakianza kutoka.

“Haiwezekani Richard. Ahsante sana kwa chakula,” alisema Sarafina, hakutaka kubaki mahali hapo, akasimama na kuanza kuondoka huku akiwa hajui ni kwa jinsi gani mwanaume huyo alikuwa akimpenda moyoni mwake.

Alipoondoka, Sarafina hakuangalia nyuma, Richard alibaki mezani pale huku akiwa amechoka na kuumia vilivyo. Alimwangalia Sarafina alivyokuwa akiondoka, hata kuondoka mahali hapo akashindwa na hivyo kuchukua chumba katika hoteli hiyo na kulala siku hiyo.

Usingizi ulikuwa mzito, kichwa chake kilivurugika, alichanganyikiwa kupita kawaida. Kila alipofumba macho, taswira ya msichana huyo ilimjia kichwani mwake kitu kilichomfanya kuwa kwenye hali mbaya kupita kawaida.

“Sarafina! Nitakupata tu! Siwezi kuacha kukwambia kwamba nakupenda. Nitakupata tu,” alisema Richard na kutulia katikati ya kitanda, usingizi haukuja, usiku mzima alikesha kama popo akimfikiria Sarafina.

 

Je, nini kitaendelea?
Tukutane kesho hapahapa.

Comments are closed.