MPENZI WANGU SARAFINA-05

Moyo wa Richard haukuwa na nafuu, ulitawaliwa na majonzi tele, alikosa furaha ambayo alitegemea kwamba angeipata. Alihuzunika mno kwa sababu alikataliwa na msichana aliyekuwa akimpenda kwa moyo wote.

Hakuacha kumfikiria, kila alipolala usiku, taswira ya msichana huyo ilimjia ndotoni. Wakati mwingine alitamani kumwambia kwamba alikuwa mtoto wa bilionea mkubwa lakini aliogopa kufanya hivyo.

Kila siku ilikuwa ni ya mateso tele, alipokwenda chuo na kumuona Sarafina akiwa na wakina David, moyo wake ulimuuma kupita kawaida. Alitamani kuwafuata wanaume hao na kuwaambia wamuachie msichana aliyekuwa akimpenda kwa moyo wa dhati lakini hilo halikuwezekana kabisa.

Siku ziliendelea kukatika, baada ya miezi kadhaa, akamuona Sarafina akianza kubadilika. Hakuonekana kuwa na furaha kama kipindi cha nyuma, hakuonekana kuwa na ukaribu na David kama ilivyokuwa.

Hilo halikumsumbua, aligundua kwamba mwanaume huyo alimchezea msichana huyo na hivyo kuamua kuachana naye. Hiyo ilionekana kuwa nafasi yake na kumfuata lakini alihofia. Kama Sarafina alimkataa kipindi cha nyuma, alikuwa amebadilika nini? Ilikuwa ni lazima kumkataa kwa mara nyingine tena.

Akaachana naye, akaendelea na mambo yake lakini kila alipomuona, moyo wake haukuacha kuuma kwani alitamani kumuona akiwa na furaha siku zote, furaha isiyomuhusisha mwanaume yeyote yule zaidi yake.

Baada ya kupita miezi mitatu, akashtuka kumuona msichana huyo akiwa amenenepa na kugundua kwamba alikuwa na mimba. Huo ndiyo ulikuwa msumari mkubwa kuliko yote moyoni mwake. Aliumia kwani kwa jinsi alivyompenda Sarafina hakutegemea kumuona akiwa na mimba ya mwanaume mwingine.

Uongozi wa chuo ulipogundua hilo, haukutaka kumuacha, ukamfukuza. Richard aliumia zaidi, alitamani kumfuata Sarafina na kumwambia kwamba alikuwa tayari kumlea hata mtoto wake lakini mwisho wa siku awe naye lakini hilo lilishindikana kabisa.

Alikaa siku mbili, akaamua kumtafuta Sarafina, ili akimpata aweze kuzungumza naye lakini kitu kilichomchosha ni baada ya kuambiwa kwamba msichana huyo alirudi nyumbani kwao Mwanza.

“Lakini nasikia kwao ni masikini! Itakuwaje?” alijiuliza lakini hakupata jibu.

Hakutaka kuishia hapo, alichokifanya ni kumpigia simu, haikuwa ikipatikana, marafiki wa msichana huyo wakamwambia kwamba aliachana na matumizi ya simu kwani kila alipokuwa akiliona jina la David moyo wake ulimuuma mno.

“Na atarudi lini?” aliuliza Richard.

“Labda akijifungua!”

“Daah! Nitakwenda Mwanza kumtafuta. Anaishi wapi vile?” aliuliza Richard.

“Mabatini!”

“Mmh! Napafahamu! Nitakwenda huko!” alisema Richard.

Alipafahamu Mabatini, ulikuwa ni mmoja wa mitaa masikini jijini Mwanza. Moyo wake ulikuwa na hamu kubwa ya kumsaidia, ni kweli alimkataa, ni kweli hakumtaka lakini bado ndani ya moyo wake alisikia mapenzi mazito juu ya msichana huyo.

Alimpenda sana, hakutaka kubaki Dar es Salaam, siku iliyofuatia akapanda ndege na kuelekea Mwanza huku lengo lake likiwa ni kuonana na msichana huyo na kumwambia kwamba alikuwa tayari kumlea mtoto wake ambaye angemzaa.

****

Sarafina na Catherine wakafika katika zahanati moja uswahilini kwa ajili ya kutoa mimba. Msichana huyo alionekana kuogopa, katika maisha yake alisikia sana juu ya madhara ya kutoa mimba, alijua kabisa kwamba kizazi kingeweza kuharibika au yeye kufa lakini hayo hayakumtoa dhamira yake aliyotaka kuifanya.

Alikaa kwenye benchi na Catherine, japokuwa walikuwa wakiongea lakini Sarafina hakuonekana kuwa sawa kabisa, alikuwa kimya, kichwa alikiinamisha na muda mwingi machozi yalikuwa yakimtoka.

Kichwa chake kilisumbuliwa na fikira kuhusu David, bado hakuamini kama mwanaume huyo alimtenda kiasi chote hicho. Yaani pamoja na mapenzi aliyompa, pamoja na kumthamini sana lakini mwisho wa siku mwanaume huyo akaondoka mikononi mwake.

Baada ya dakika ishirini, daktari akatokea mahali hapo na kuwaita. Akawauliza tatizo walilokuwa nalo na wao kumwambia ukweli kile kilichowapeleka kuwa ndani ya zahanati hiyo.

“Kama ni ya wiki mbili, gharama ni elfu sitini,” alisema daktari huyo.

“Hakuna tatizo!”

Wakaambiwa wasubiri kwenye benchi, muda wote Sarafina hakuonekana kuwa na raha, mapigo ya moyo yalikuwa yakidunda huku mbele yake akikiona kifo. Hakuhitaji mtoto kipindi hicho, bado alihitaji sana kusoma na ndiyo maana alikuwa mahali hapo.

“Naogopa sana Cathy!” alisema Sarafina huku akimwangalia rafiki yake.

“Unaogopa nini? Wala huwezi kufa, ni kitendo cha dakika kadhaa tu, hata maumivu husikii tena,” alisema Catherine.

“Kweli?”
“Ndiyo!”

Alimwamini sana, wakaendelea kusubiri na baada ya dakika kadhaa, daktari akamuita Sarafina ambaye aliingia ndani ya chumba kile na kumtaka kulala kitandani. Akafanya hivyo.

Mapigo yake ya moyo yaliendelea kudunda zaidi, aliogopa, moyo wake ukajawa na hofu huku kijasho chembamba kikianza kumtoka. Alipoiona mikasi na visu juu ya meza, alizidi kuogoa zaidi.

“Mbona unatetemeka binti?’ aliuliza daktari.

“Hapana! Hapana dokta! Siwezi!” alisema Sarafina huku akijitoa katika kitanda alichokuwa amelala.

Akatoka ndani ya chumba kile, daktari akabaki akimshangaa. Hakusimama kuzungumza na Catherine aliyekuwa akimsubiri kwenye benchi, aliunganisha na kutoka nje kabisa. Rafiki yake huyo alibaki akishangaa, hakuamini kama kazi ile ilifanyika kwa dakika chache namna ile.

Alipomfikia, akamuuliza kama daktari alimaliza lakini Sarafina alimwambia kwamba aliahirisha, hakutaka kuitoa mimba hiyo, alikuwa radhi kuzaa lakini si kuua kiumbe kisicho na hatia.

“Unasemaje?” aliuliza Catherine huku akionekana kutokuamini.

“Acha nizae. Naweza kumzaa Lady Jay D au Nyerere. Sipo tayari kutoa mimba,” alisema Sarafina.

Catherine alishangaa lakini ndiyo ulikuwa msimamo wa msichana huyo, hakutaka kutoa mimba na alikuwa tayari kuona akizaa na kumtunza mtoto wake. Wakaondoka na kurudi chuo, huko, maisha yaliendelea, hakuacha kumpigia simu David, mwanaume huyo hakuwa akipokea na wakati mwingine alihisi kama anasumbuliwa na hivyo kuizima simu hiyo.

Sarafina aliendelea kuumia moyoni mwake lakini hakuwa na jinsi. Alipokuwa akimuona Richard alijishtukia, wakati mwingine alikuwa akijificha kwani mwanaume huyo ndiye aliyeonyesha kuwa na shida naye kwa hali na mali japokuwa alionekana kuwa masikini wa kutupwa.

Baada ya miezi kadhaa, kila mtu akajua kwamba alikuwa na mimba, muonekano wake ukawatia hofu wanachuo wote. Uongozi ukamuita na kuzungumza naye, hakubisha, akawaambia kwamba kweli alikuwa na mimba hivyo kufukuzwa chuoni.

Hakuwa na pa kwenda zaidi ya nyumbani kwao. Ingekuwa rahisi kwenda nyumbani kwa kina David kama tu wangekuwa pamoja lakini kwa kuwa alikuwa amekataliwa na mwanaume huyo, hakuwa na jinsi zaidi ya kujipanga kurudi jijini Mwanza.

Ndani ya basi mawazo yake yalikuwa kwa wazazi wake, hakujua wangemfanya nini baada ya kugundua kwamba alikuwa mjauzito. Walitumia kiasi cha fedha kwa ajili yake, walikopa kuhakikisha anapata elimu bora lakini mwisho wa siku alikuwa akiwapelekea mimba nyumbani.

Alipofika Mwanza, kabla ya kwenda nyumbani akatafuta saluni, akatoa blichi na kiduku kisha kujiweka kama msichana wa kawaida asiyekuwa na tatizo lolote lile. Alipofika nyumbani, wazazi wake walishangaa, hakikuwa kipindi cha likizo lakini alikuwa amerudi, alirudi kufanya nini?

“Una mimba?” aliuliza mama yake huku akimwangalia kwa mshtuko, aliligundua hilo baada ya kuona mabadiliko makubwa.
“Ndiyo mama! Naomba unisamehe!” alisema mama yake.

“Yeleuwiiiiiiii….una mimba!” alisema mama yake kwa kupayuka.

Hakuzungumza kitu zaidi ya kupiga kelele, akamwambia kwamba hiyo ilikuwa kesi kubwa na alitakiwa kumsubiri baba yake. Sarafina akabaki akitetemeka, alimfahamu baba yake, alikuwa mwanaume mkorofi ambaye hakuwa na masihara hata kidogo.

Alibaki nyumbani hapo akilia tu, alimsubiri baba yake, wakati mwingine alijisemea kwamba ilikuwa ni lazima kufukuzwa lakini wakati mwingine aliamini kwamba baba yake asingeweza kumfukuza kwa kuwa alikuwa mtoto wake.

Ilipofika saa kumi na mbili jioni, Mzee Butati akafika nyumbani hapo, kwanza alishangaa kumkuta sarafina, hicho hakikuwa kipindi cha likizo sasa ilikuwaje binti huyo awe nyumbani hapo. Akamsalimia na kwenda chumbani, huko, mkewe akamwambia kilichokuwa kimetokea.

Maneno hayo yalimtia hasira, hakuamini kama kweli mtoto wake kipenzi, Sarafina alirudi nyumbani hapo akiwa na mimba. Alikumbuka mkopo waliokuwa wakikopa kwa ajili ya msichana huyo, alikumbuka maumivu aliyokuwa akiyapata kufanya kazi ili kulipa mikopo aliyokuwa akichukua kwa ajili ya binti yake, leo hii, pamoja na tabu zote, alirudi nyumbani akiwa na mimba.

“Unasemaje?” alimuuliza mkewe kana kwamba hakujua alichoambiwa.
“Amekuja na mimba. Huyo hapo na tumbo lake,” alisema mkewe.

Mzee Butati akatoka chumbani na kuelekea sebuleni, alionekana kama mbogo, alikuwa na hasira mno, hakutaka kuzungumza kitu chochote kile, akamshika mkono Sarafina na kutoka naye nje kwani aliamini kwamba kama angempiga basi angeweza kusababisha matatizo kwa mtoto.

“Umekuja kufanya nini na mimba yako?” aliuliza Mzee Butati huku akimwangalia sarafina.
“Nisamehe baba!” alisema Sarafina huku akilia kwa uchungu, tayari majirani waliokuwa ndani ya nyumba zao wakatoka nje na kuangalia kilichokuwa kikiendelea.

“Ninasema hivi! Ondoka nyumbani kwangu, sitaki kukuona, yaani kuanzia leo wewe siyo mtoto wangu! Ondoka nyumbani kwanguuuuuu…” alisema Mzee Butati kwa hasira kiasi kwamba mpaka akawa anatetemeka.

Sarafina aliogopa, aliwahi kumuona baba yake akiwa kwenye hasira lakini siku hiyo alionekana kuwa tofauti, alionekana kuwa na hasira kuliko siku zote. Akaondoka huku akilia, katika mfuko wa sketi yake alikuwa na kiasi cha shilini laki moja tu, hakujua maisha yangekuwaje na kiasi hicho cha fedha.

Giza likaanza kuingia, akaondoka nyumbani hapo huku akilia. Wazazi wake walimfukuza, hakuamini kama angeweza kupokelewa na watu wengine, mawazo yaliyomjia kichwani mwake ni kurudi Dar es Salaam.

Usiku wa siku hiyo akachukua chumba gesti na siku iliyofuata akapanda ndani ya basi na kuanza safari ya kurudi Dar. Moyo wake ulikuwa na huzuni kubwa, hakujua ni wapi alitakiwa kuelekea, aliwaza kwenda nyumbani kwa kina david lakini hakuamini kama mwanaume huyo angeweza kumpokea, alijua kabisa kwamba angemfukuza kwa kuwa tayari alimpa hela ya kutoa mimba lakini hakufanya hivyo.

Siku hiyo usiku gari likaingia Ubungo jijini Dar, akateremka na kwenda katika Mtaa wa tandale na kuchukua chumba katika gesti moja na kutulia humo. Usiku mzima hakulala, kichwa chake kilikuwa na mawazo tele, alikuwa na ndoto za kuwa mtu mwenye heshima hapo baadaye lakini ndoto yake hiyo ikafutika kama upepo, mimba aliyokuwa nayo ikayaharibu maisha yake.

Usiku huo ulikuwa mgumu kupata usingizi, alikuwa akiyafikiria maisha yake, aliharibu hivyo ilikuwa ni lazima kufikiria namna ambavyo angeishi na mimba yake mpaka kujifungua salama.

“Nitafanya kila kitu kumtunza mtoto wangu!” alisema.

Asubuhi ilipofika, akatoka ndani ya chumba kile, akaanza kuelekea katika sehemu mbalimbali, hasa migahawa akitafuta kazi. Hakutamani kuishi maisha ya kumtegemea mtu mwingine, alitaka kuishi kwa kujitegemea yeye mwenyewe.

Alizunguka katika migahawa yote Tandale japo apate kazi, hakupata kazi, akaelekea Mwananyamala napo mambo yalikuwa magumu. Siku hiyo ilikuwa ni siku ya kuzunguka kila kona, akakosa kazi, mpaka inafika saa moja usiku, alikuwa amechoka, mfukoni alikuuwa na shilingi elfu kumi na tano tu na hakuwa amekula.

Akaelekea katika mgahawa mmoja na kula, alipomaliza, akaondoka na kuelekea mitaani. Hakuwa na sehemu ya kulala, alipopaona kufaa ilikuwa ni kwenye nyumba moja ya kawaida ambayo ilikuwa na kigiza fulani huku kukiwa na kibaraza, hapo ndipo palionekana kuwa sehemu sahihi ya yeye kulala, akatafuta maboksi, akayakosa hivyo kutafuta viroba vya gunia, akavipata, havikuwa visafi, hakujali, akavitandika na kulala kwani hakuwa na jinsi.

Kutoka katika uzuri wa ajabu, kupapatikiwa na wanaume wengi mpaka kufikia hatua ya kulala mtaani, tena juu ya viroba ilikuwa ni hatua moja kubwa kushuka chini. Usiku huo akayafikiria maisha yake kwa ujumla, jinsi alivyokuwa akipapatikiwa na wanaume wengi, jinsi alivyokuwa akipendwa kila sehemu.

Mtu ambaye alimjia kichwani mwake mara nyingi hakuwa mwingine bali Richard. Akamfikiria sana mwanaume huyo, jinsi alivyokuwa akimpenda, aliamini kwamba kama angepata mimba ya mwanaume huyo asingeweza kumfukuza japokuwa alikuwa masikini.

Akajuta, akalia sana, akaumia lakini hilo halikuweza kubadilisha maisha yake. Pale alipokuwa, akapata kazi kubwa ya kufukuza mbu waliokuwa wakimuuma, baridi lilimpiga lakini hakujali, akaingia katika maisha ya mitaani, alikuwa na kazi kubwa ya kuendelea kuishi katika maisha hayo. Hakujua angeishi kwa kipindi gani, hakujua kama angeishi mpaka kifo chake, hakuwa na jinsi, alikubaliana na maisha hayo yaliyosababishwa na uzuri wake wa sura na umbo lake matata.

Wakati akiwa na mawazo lukuki, akapitiwa na usingizi, akalala na kuamshwa na adhana iliyokuwa ikiadhiniwa alfajiri, akaamka, hakulala tena, alikaa na ilipofika saa moja asubuhi, akaanza kuzunguka huku na kule kutafuta kazi.

Hakuchagua kazi, alitaka yoyote ambayo ingeyafanya maisha yake kuwa na afueni. Alizunguka na kuzunguka, mfukoni alikuwa na kumi na moja, alikula na kuendelea kuzungumza, jua likamchoma lakini hakujali, mpaka inafika saa moja usiku, hakupata kazi, akabakiwa na kiasi kidogo zaidi cha fedha na ilipofika majira ya saa tano usiku, akarudi katika nyumba ileile, akaweka viroba vyake na kulala huku akiwa hoi. Kila alipoyatathmini maisha yake ya baadaye, aliiona dhiki kubwa ikimsogelea.

 

Je, nini kitaendelea?

Tukutane kesho hapahapa.

Toa comment