MPENZI WANGU SARAFINA-06

Baada ya saa kadhaa ndege ikaanza kuingia katika uwanja wa ndege jijini Mwanza, Richard akateremka na kuanza kuelekea katika jengo la uwanja huo. Hakutaka kuzungumza na mtu yeyote, kitu pekee kilichokuwa kichwani mwake wakati huo kilikuwa ni msichana Sarafina ambaye katika kipindi hicho aliamini kwamba alikuwa nyumbani kwao.

Akatoka ndani ya jengo la uwanja huo, alipofika nje akachukua teksi ambayo ilimpeleka mpaka katika Hoteli ya Tausi na kutulia hapo. Siku hiyo hakutaka kuzunguka, kwa kuwa ilikuwa ni jioni, akafanya mambo mengine huku akipanga siku inayofuatia ndiyo ya kwenda nyumbani kwa kina Sarafina kumuona kwa kuamini kwamba kama angefanya hivyo basi msichana huyo angeweza kukubaliana naye kwamba alikuwa akimpenda kwa moyo wa dhati.

“Hakuniamini! Sasa nitataka aniamini niliposema kwamba ninampenda,” alisema Richard.

Alishindwa kuuficha moyo wake, ulikuwa kwenye mapenzi ya dhati, alimpenda sana Sarafina zaidi ya msichana yeyote yule, hakujali kuhusu mimba aliyokuwa nayo, alichokuwa akikiangalia ni jinsi moyo wake ulivyokuwa ukimpenda.

Usiku huo akalala na ilipofika asubuhi, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kwenda katika Mtaa wa Mabatini kwa lengo la kuonana na Sarafina aliyekuwa ameelekea huko kutokea Dar es Salaam.

Hakuwa akipafahamu lakini kwa kuwa aliulizia sana, akapelekwa mpaka katika mtaa huo na alipoulizia jina la sarafina, ilikuwa rahisi kupelekwa huko. Hakuchukua dakika nyingi akafika, hali aliyoikuta nyumbani hapo haikumvutia kabisa.

Aliwakuta wazazi wote wawili wakiwa wamekaa nje, kwa jinsi walivyoonekana, walikuwa na hasira kupita kawaida. Hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea mahali hapo, hakujua kama Sarafina alikuwepo ndani au la.

Aliwasalimia na kusimama kiheshima, akawaambia kilichokuwa kimewaleta. Mzee Butati akasimama kwa hasira, akili yake ilimwambia kwamba mwanaume aliyesimama mbele ya macho yao ndiye aliyempa ujauzito binti yao kwani hata lafudhi yake ilisikika kama mtu aliyetokea Dar.

“Wewe ndiye uliyempa mimba binti yangu?” aliuliza mzee Butati huku akionekana kuwa na hasira, palepale alipokaa, akachukua panga lililokuwa pembeni yake.

“Mzee! Nimekuja tuzungumze kwanza!”

“Niambie kama wewe ndiye uliyempa mimba mtoto wangu?” aliuliza mzee Butati kwa hasira, tayari watu waliokuwa pembeni wakasogea kwani hali ilivyoonekana mahali hapo, ilikuwa ni lazima mzee Butati afanye jambo.

Richard aliogopa, alitetemeka, kwa jinsi alivyomwangalia mzee yule, aliziona hasira zake usoni mwake, kijasho chembamba kilikuwa kikimtoka, kwa lile panga alilokuwa nalo mkononi mwake akahisi kabisa kwamba mzee huyo angeweza kumfanyia jambo baya.

Hakukimbia, alitulia huku akimwangalia mzee huyo machoni, alijaribu kumwambia ukweli kwamba yeye hakuhusika, alimfahamu sana Sarafina lakini ukweli ni kwamba hakuwahi kupendwa na msichana huyo mrembo.

Mzee Butati akatulia, akahisi kwamba kijana huyo alikuwa na mambo mengi ya kumwambia hivyo kumpunguza hasira zake na kumruhusu kukaa chini na kusikiliza ni kitu gani kijana huyo alitaka kumwambia.

Richard hakutaka kuficha, alitaka kuwa mkweli kwa kila kitu, alichoamini ni kwamba msichana huyo alikuwa ndani ya nyumba hiyo na kitu ambacho kingemfanya kuwa na amani ni kuwaambia wazee hao ukweli juu ya kile kilichokuwa kimetokea.

Akaanza kuwahadithia kilichokuwa kimetokea jijini Dar. Hakutaka kuwaficha kwa kitu chochote kile, aliwaambia jinsi alivyokuwa na malengo na binti yao, alivyodhamiria kuwa naye na mwisho wa siku kumuoa lakini msichana huyo alikataa.

Wazazi wa Sarafina walikuwa kimya wakimwangalia Richard, alizungumza kwa kujiamini, aliwaambia wazazi hao jinsi alivyokuwa, alikuwa mtoto wa bilionea mkubwa nchini Tanzania na lengo lake kubwa la kutaka kuwa na Sarafina ni kumzalia watoto, kujenga familia na kumsaidia yeye na familia yake.

Mzee Butati alivyosikia hivyo, akapiga hatua fupifupi kurudi nyuma, akaliweka panga chini kisha kushika mikono yake kichwani. Alichanganyikiwa, alikuwa kwenye umasikini mkubwa sana lakini mwisho wa siku, alimfukuza binti yake, kwa maana hiyo msaada ambao alitakiwa kuupata asingeweza kuupata.

“Mke wangu! Tumefanya makosa,” alisema mzee Butati huku akimwangalia mke wake, uso wake tu ulionyesha kujuta kwa kile alichokuwa amekifanya.

Huo haukuwa muda wa majuto, ulikuwa ni muda wa kukubaliana kwa kile kilichokuwa kimetokea, walimwambia Richard ukweli kwamba walimfukukuza Sarafina siku iliyopita, na mpaka muda huo hawakujua binti huyo alikuwa wapi.

Richard alishangaa, hakuamini kama Tanzania bado kungekuwa na wazazi wenye roho kama hiyo, alinyong’onyea, moyo wake ukaingiwa na hasira, katika vitu ambavyo hakuwa akivipenda ni kuona msichana aliyekuwa akimpenda akipata shida. Hakuzungumza kitu, akaondoka mahali hapo.

Kilichofuata kilikuwa ni kuzunguka kila kona jijini Mwanza, alijua kwamba angebahatika kumuona msichana huyo mjini. Alifanya kazi hiyo ya kuzunguka kwa siku tatu lakini hakufanikiwa, akaamua kurudi jijini Dar ambapo hakukaa sana, baada ya wiki mbili, akaondoka na kuelekea nchini Marekani kusoma katika Chuo cha Mississippi kilichokuwa katika jiji hilohilo.

****

Maisha ya Sarafina hayakubadilika, bado yalikuwa kwenye msoto mkubwa, hakuwa na pa kulala, aliendelea kulala katika vibaraza vya nyumba mbalimbali. Usiku, baridi lilimpiga, mbu walimuuma lakini hakuwa na cha kufanya.

Alikwishakwenda kwa marafiki zake kuomba msaada, kwa Catherine, alifukuzwa kama mbwa, alipomfuata rafiki yake mwingine, Matilda, hakumfungulia mlango, kwa kifupi hakutaka kabisa kuonana naye.

Mrembo yule, aliyewatikisa wanaume akaanza kufifia, urembo wake aliokuwa akiringia ukaanza kupotea, figa yake kali ikaanza kondoka, Sarafina alilia mno, aliyajutia maisha yake, tamaa ya kupenda pesa leo hii ilimfanya kuishi katika maisha aliyokuwa akiishi.

Mchana wanaume walipokuwa wakimuona walimmendea, walihisi kwamba alikuwa msichana aliyekuwa akiishi nyumba fulani na usiku ulipoingia, walishangaa kumuona akiwa analala mitaani, tena katika vibaraza vya nyumba.

Hawakumuelewa msichana huyo, wanaume hawakutaka kumfuata, alikuwa mzuri lakini kila mmoja alimuogopa kwa kuhisi kwamba alikuwa ofisa wa Usalama wa Taifa ambaye alifika Tandale kwa ajili ya kuchunguza kitu fulani.

Uoga wa wanaume hao ukamfanya kupata nafuu, hakusumbuliwa, hakubakwa, aliendelea kuishi maisha hayohayo huku asubuhi akiamka na kwenda kutafuta kazi ya kuwahudumia wateja katika migahawa mbalimbali.

Baada ya kuzunguka sana, hatimaye akafika katika Baa ya Las vegas iliyokuwa hapohapo Tandale. Alikwenda hapo kwa lengo moja la kutafuta kazi. Hakutamani kuwa mfanyakazi wa baa lakini kwa hatua aliyokuwa amefikia, hakuwa na jinsi, alikuwa radhi kuifanya kazi hiyo na mwisho wa siku apate hela ya kula.

“Hapa kazi ipo! Upo tayari kuuza baa?” aliuliza mwanaume mmoja huku akimwangalia Sarafina kwa macho ya matamanio.

“Nipo tayari mzee wangu!”
“Sawa. Mshahara utakuwa elfu thelathini kwa mwezi!” alisema mwanaume huyo.

“Elfu thelathini?” aliuliza Sarafina, hakuamini kama kungekuwa na kazi yenye mshahara mdogo kama huo.

“Ndiyo! Unaona mdogo?” aliuliza mzee huyo huku akianza kubadilika.

“Hapana! Ni mkubwa na ndiyo maana nimeshangaa,” alisema Sarafina, japokuwa ilikuwa ni kazi ya kuuza baa lakini hakutaka kuiacha.

Akaanza kazi katika baa hiyo, walevi walipokuwa wakifika mahali hapo, walipenda sana kuhudumiwa na Sarafina kwa kuwa alikuwa msichana mrembo na msafi. Kila wakati alipenda kutabasamu japokuwa moyoni mwake kulikuwa na maumivu makali mno.

Kama ilivyokuwa kwa wahudumu wengine, hata yeye alikuwa akishikwashikwa, kila alipobeba chupa ya pombe na kupeleka katika meza za wateja, huko alishikwa makalio na hata wakati mwingine kusifiwa kwa uzuri aliokuwa nao.

“Unajua wewe dada mzuri sana,” alisema jamaa mmoja huku akimwangalia Sarafina.

“Ahsante!”

“Unakunywa pombe?”

“Hapana!”

“Daah! Unakosa ladha moja matata sana duniani! Pole. Hivi unaweza kunipa namba yako ya simu?’ aliuliza jamaa huyo.

“Sina simu!”
“Basi nikupe yangu moja ili tuwasiliane!” alisema mwanaume huyo.

“Huwa sijui kutumia simu!”
“Nitakufundisha!”
“Hapana! Usijali! Unataka Safari na nini?” aliuliza Sarafina.

Hakupumzika, kila siku alikuwa akisumbuliwa na wanaume hao, walimsfia kutokana na uzuri aliokuwa nao. Ni kama wanaume waliambiana kwani baada ya siku kadhaa wanaanza kujaa hapo baa na kila mmoja alitaka kuhudumiwa na Sarafina.

“Mimi namtaka yule dada mweupe ndiyo anihudumie,” alisema jamaa mmoja baada ya kufika hapo baa.

“Nani? Asnath?”
“Hapana yule mcheshi!”

“Mariamu?”

“Yule pale. Psipsiiiii…cheupe!” aliita jamaa huyo baada ya kumuona Sarafina.

Japokuwa tumbo lake lilikwishaanza kuonekana kwa mbali lakini msichana huyo alionekana kuwa kivutio kwa wateja wengi. Aliifanya kazi hiyo kwa kujitoa sana, kila mmoja alimpenda kutokana na upole wake.

Maisha yalikuwa na unafuu japokuwa yaliendelea kuwa mabaya. Hakuwa na chumba, alichangia chumba na wenzake, kama ikitokea mmoja akapata mteja, basi siku hiyo wengine wote walitakiwa kulala nje, na kama ulitaka kulala ndani basi ujue kwamba ni lazima uingiliwe na ukubali.

Hilo, kwa Sarafina lilikuwa gumu, wenzake walipokuwa wakipata wateja, alikwenda baa na kulala kwenye viti. Yalikuwa ni maisha yenye mateso mno lakini alivumilia.

Baada ya miezi miwili tumbo lake likaanza kuonekana, watu wakagundua kwamba alikuwa na mimba, wanaume waliokuwa wakimuona mrembo wakaanza kuondoka. Mimba iliharibu kila kitu lakini  kwa Sarafina hakutaka kujali, hakuitoa mimba yake kwa kuwa alimuonea huruma mtoto aliyekuwa tumboni mwake, hivyo kubaki na mimba wala hakuona kama kulikuwa na tatizo.

Miezi ikasonga, ilipofikisha miezi sita, meneja wa baa hiyo akaamua kumfukuza Sarafina kazi. Msichana huyo akakimbilia mitaani, kulekule alipokuwa akiishi zamani. Hakuwa na fedha za kutosha kupanga chumba bali alianza upya kulala mitaani kama kawaida yake.

Mbu walimng’ata, alipigwa na baridi kali lakini hakujali, ndiyo kwanza aliendelea kufanya mambo yake, asubuhi anaamka na kuzurura kuombaomba mitaani na jioni anarudi kwenye kibaraza kulala.

 

Je, nini kitaendelea?
Tukutane kesho hapahapa.

Toa comment