The House of Favourite Newspapers

MPENZI WANGU SARAFINA-08

0

David hakutaka kukumbuka kuhusu Sarafina, kwake, msichana huyo alikuwa kama wengine tu, kutembea nao na kufanya mapenzi kisha kuwaacha wakiwa na maumivu makali, na mbaya zaidi kuwaacha na mimba huku akikataa kwamba haikuwa yake.

Alipotoka kwa Sarafina, moyo wake ukavutika kwa msichana mwingine, huyo aliitwa Paulina. Alikuwa ni miongoni mwa wasichana warembo chuoni hapo. Alimpenda, alimvutia kwani mapaja yake manene na kalio lake kubwa lilimpagawisha kupita kawaida.

Kama kawaida yake akajitosa, alitaka kutembea na msichana huyo, amuonyeshee mapenzi ya dhati kama alivyomuonyeshea Sarafina, amfanye ajione kuwa mwanamke mwenye thamani, anayependwa zaidi ya mwanamke yeyote katika dunia hii, lakini akishamaliza kazi yake, amuache na kuendelea na maisha yake.

David aliingia kwa gia ya kumsifia, kwamba alikuwa mwanamke mrembo, mwenye sifa za kuitwa mrembo ambaye alikuwa na umbo kali hata Agnes Masogange hakuwa akiingia. Moyo wa Paulina ukafurahi, akapenda kusifiwa, akapewa sifa kemkem na kuambiwa kwamba sura yake ilikuwa ya kitoto, iliyokuwa na mvuto kama video vixen, Baby Annaiyah kitu kilichomfanya kumpenda mwanaume huyo.

Alipenda kuonana naye kwa kuwa tu kila walipokutana alikuwa akisifiwa. David akautumia udhaifu huohuo kummaliza Paulina, akawa haoni wala asikii, yeye ndiye aliyekuwa akimpigia sana simu David na kuzungumza naye kwani aliamini kwamba kila alipofanya hivyo ilikuwa ni lazima kusifiwa.

“Eti kama Jenifer Lopez,” alisema Paulina huku akitoa kicheko cha kike.

“Ndiyo hivyo Paulina. U msichana mzuri sana mpaka Jini Maimuna anakuonea wivu. Mtoto unajua kucheka, unajua kutembea. Na huko nyuma ulivyoumbika. Mtoto mashallah! Yaani ungekuwa Mombasa, sasa hivi unamiliki ndege yako, biashara kubwa kutoka Dubai,” alisema David, jinsi alivyoongea alionekana kumaanisha japokuwa ukweli ni kwamba alitaka kupata nafasi ya kukiona kitovu cha msichana huyo na baadaye kushuka chini kidogo.

“Wala mimi siyo mzuri!” alisema Paulina huku akitaka kusikia david angempa sifa zipi nyingine.

“Unajidanganya! Nilipokuona mara ya kwanza, nilidhani nimekutana na jini. Nilipokusalimia, hakika mtoto una sauti nzuri sana, hivi ushawahi kuimba kwaya?” aliuliza David.

“Hapana!”
“Kwa sisi tuliowahi kuimba, sauti yako ni sauti ya kwanza, ile inayowafanya wenye mapepo walipuke, ni sauti ambayo ukiimba kwa muda mrefu, Mungu atasimama kwenye kiti chake cha enzi na kujivunia uumbaji wake, kujivunia kumpa msichana mmoja sauti nzuri ya kumsifu na kumuabudu,” alisema David.

Kila mstari aliomwambia Paulina, alilainika, akamuona david kuwa mwanaume mzuri, ambaye alistahili kuwa maishani mwake. Akasimama kutoka kitandani, akakisogelea kioo na kuanza kujiangalia. Sifa za mwanaume huyo zikaanza kujirudia kichwani mwake, kweli, kile alichokisema David ndicho alichokiona, akalitingisha kidogo kalio lake.

“Ahsante Mungu kwa kunipa hii silaha matata!” alisema Paulina kisha kutoa tabasamu.

Paulina alianza kubana, akabana na kubana lakini akashindwa kuvumilia. Katika siku ambayo hakuitarajia, akajikuta akilala kwenye kitanda cha David, akaipanua miguu yake na kuvunja amri ya sita na mwanaume huyo.

Hilo likawa kosa, damu zikakutana, akajiona kama amemalizwa kila kitu, hakuwa na ujanja tena, mwanaume huyo aliitumia nafasi hiyohiyo kukutana naye kimwili, hata kama alikuwa hataki, alikumbushwa namna alivyokuwa fundi kitandani, akakumbushwa jinsi alivyokuwa akiguna juu ya sita kwa sita na mwisho wa siku kumkubalia tena.

Wakabanjuka na kubanjuka, starehe zikaongezeka, baada ya miezi miwili, msichana Paulina akaanza kujisikia tofauti, hakutaka kuchelewa, akaenda kupima, majibu yakatoka na kuambiwa kwamba alikuwa na mimba.

Alijuta, alimtafuta David na kumwambia kuhusu ujauzito huo, kama ilivyokuwa kwa Sarafina, akamkatalia, akamwambia kwamba haikuwa yake, na kama alikuwa na mchezo wa kupata mimba sehemu nyingine kisha kumsingizia, basi wasijuane.

Paulina akaumia lakini hakuwa na jinsi, akakubaliana na mwanaume huyo, alichokifanya ni kutoa mimba na maisha yake kuendelea huku akijiahidi kwamba asingeweza kuuruhusu mwili wake uchezewe na mwanaume mwingine kama ilivyokuwa kwa David.

Hiyo ilikuwa ndiyo tabia yake, David hakuridhika, akaendelea kuwafunua wasichana wengi na kila alipokutana na marafiki zake akaanza kuwaambia kuhusu sifa za wanawake mbalimbali, alijua wanene walikuwa na mbwembwe gani kitandani, alijua wembamba walikuwaje, weupe na weusi, wote alijua wanafananaje.

Baada ya kutembea nao sana, mwisho wa siku akakutana na msichana mmoja, binti aliyetoka katika familia bora, huyu aliitwa Gloria, msichana mrembo, mwenye figa matata ambaye alikutana naye katika Ufukwe wa Mbalamwezi.

Alimfuata na kuzungumza naye, kwa kuwa alikuwa muongeaji sana, ndani ya dakika kadhaa wakawa kama watu waliofahamiana miaka mingi iliyopita hivyo kubadilishana namba za simu.

“Basi nitakucheki!” alisema David.

“Usijali! Nitasubiri simu yako,” alisema Gloria huku akiingia ndani ya gari lake la kifahari kisha kuondoka mahali hapo huku David akiwa amesimama akiliangalia linavyoondoka.

“Hawa ndiyo wanawake sasa. Huyu naoa,” alijisema huku akiachia tabasamu pana.

****

Sarafina alionekana kama kituko, watu wachache waliokuwa wakimwangalia walibaki wakimshangaa, hawakuamini kumuona mwanamke aliyekuwa kwenye hali ile kama alivyokuwa Sarafina.

Alikuwa akiendelea kukimbia kuelekea katika Hospitali ya Mwananyamala, hakufahamu kama Magomeni kulikuwa na hospitali, hospitali alizokuwa akizifahamu zilikuwa mbili tu, Muhimbili na hiyo aliyokuwa akiifuata.

Kama kulia, alilia sana lakini hakukuwa na kitu kilichobadilika, mtoto Malaika aliendelea kuwa kwenye hali ileile, mboni nyeusi haikurudi, macho yake yaliendelea kuwa meupe huku mwili ukimtetemeka.

Huku akiwa njiani akikimbia na tayari akiwa amefika Kinondoni Studio, ghafla akapigiwa honi, akayapeleka macho yake pembeni kuliangalia gari lililompigia honi, macho yake yakatua katika gari moja ndogo.

“Dada unakwenda wapi?” aliuliza mwanaume aliyekuwa ndani ya gari hilo, harakaharaka Sarafina akamkimbilia huku akilia.

“Naomba unisaidie! Mtoto wangu anakufa! Malaika wangu anakufa,” alisema Sarafina huku akimwangalia mwanaume huyo ambapo baada ya kupeleka macho kwa Malaika, yeye mwenyewe alishangaa.

“Mungu wangu!” alisema, hapohapo akaufungua mlango, akamuingiza ndani na kuanza kuelekea hospitali.

Njiani, dereva aliendesha gari kwa mwendo wa kasi. Hakuchukua muda mrefu akafika hospitalini hapo ambapo akamfungulia Sarafina mlango na kisha kumteremsha.

“Nesi! Nesi msaada jamani!” alipiga kelele mwanaume huyo. Manesi wawili wakasogea, walipomwangalia Malaika, wao wenyewe wakashangaa, wakamchukua na kumpeleka katika chumba cha matibabu kisha kumuwekea dripu ya maji yaliyochanganywa na dawa.

Sarafina alibaki kwenye benchi akilia, alimwangalia mwanaume yule, alishindwa ni kwa jinsi gani alitakiwa kumshukuru kwani alikuwa amemsaidia kwa kiasi kikubwa na inawezekana pasipo yeye basi mtoto wake, Malaika angeweza kufa njiani.

“Nashukuru sana,” alisema Sarafina huku akilia.

“Usijali mama!”

Matibabu  yaliendelea, mwanaume yule hakuondoka, alibaki hapohapo hospitali akitaka kuona ni kitu gani ambacho kingetokea. Kila alipomwangalia Sarafina, hakujua alikuwa na nini ndani yake, alikuwa akiendesha kuelekea klabu lakini ghafla, huku akiwa na haraka akamuona mwanamke huyo, hakuwa na lengo la kusimama, hakuwa na lengo la kuzungumza naye lakini alishtukia gari lake likisimama na yeye mwenyewe kuzungumza kitu ambacho hakukitaka kabisa.

“Ni Mungu ndiye aliyesimamisha gari langu! Kwa nini alitaka nimsaidie mwanamke huyu?” alijiuliza lakini alikosa jibu.

Akasahau kuhusu klabu, hakutaka kwenda tena huko, alibaki hospitalini hapo na Sarafina huku akimfariji kwamba mtoto wake angepona na kusingekuwa na kitu chochote kibaya ambacho kingetokea.

Baada ya saa moja, mlango wa chumba alichokuwemo mtoto wake ukafunguliwa, nesi mmoja akatoka kutoka humo, harakaharaka Sarafina akasimama na kumfuata nesi, alitaka kujua ni kitu gani kiliendelea, alitaka kujua hali ya mtoto wake.

“Mtoto wangu anaendeleaje?” aliuliza Sarafina huku akimwangalia nesi yule machoni, akashindwa kujibu swali hilo, ghafla machozi yakaanza kumlenga na mwisho wa siku kutiririka mashavuni mwake.

“Nini kinaendelea?” aliuliza Sarafina, machozi ya nesi yalimjibu swali alilokuwa ameuliza, huku akiwa na presha kubwa moyoni mwake, ghafla nesi yule akaanza kulia kwa sauti, Sarafina akashtuka, naye akaanza kulia, sauti ndogo ikaanza kusikika moyoni mwake kwamba mtoto wake, Malaika alikuwa amefariki dunia.

 

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumatano.

Leave A Reply