MPENZI WANGU SARAFINA-15

MTUNZI: NYEMO CHILONGANI

 

Ibrahim alirudi mpaka kule alipokuwa akilala na Malaika, alipofika, hakumwambia kitu kwa kuwa alikuwa na watoto wengine, akamvutia pembeni na kwenda naye kukaa sehemu, Malaika alishangaa, haikuwa kawaida, alimwangalia Ibrahim, jinsi alivyokuwa siku hiyo alionekana kabisa kuwa na kitu alichotaka kumwambia.

Kabla ya kuzungumza kitu akamwangalia Malaika, alitamani kumwambia ukweli lakini moyo wake ulikuwa mzito kufunguka. Mkononi alishikilia mfuko wa nailoni ambao ndani yake kulikuwa na laptop aliyokuwa ameiba na ile bahasha iliyojaa pesa.

“Kuna nini?” aliuliza Malaika huku akimwangalia Ibrahim.

“Tuondoke!”
“Tuondoke! Kwenda wapi?” aliuliza Malaika.

“Popote! Hapa si salama kwetu,” alisema Ibrahim huku akimwangalia Malaika.

Malaika hakutaka kukubaliana naye, kwanza alitaka kufahamu ni kitu gani kilikuwa kimetokea, halikuwa suala la kuondoka mahali hapo pasipo kujua kulikuwa na nini. Alimuuliza Ibrahim lakini kijana huyo hakutaka kumjibu kitu chochote kile.

“Kuna nini?”

“Hakuna kitu!”
“Sasa tutaondokaje? Mimi siwezi kuondoka,” alijibu Malaika.

Alimaanisna alichokizungumza, asingeweza kuondoka kuelekea sehemu yoyote ile. Hapo ndipo palikuwa nyumbani kwake, hakuwa na ndugu, watu pekee aliokuwa amewazoea walikuwa watoto wenzake hao tu.

Ibrahim hakutaka kumwambia Malaika ukweli, hakumwamini msichana, alijua kwa namna moja au nyingine kama ungeamua kumwambia ukweli, hata kama ungemwambia hiyo ni siri asingeweza kuitunza.

Alipoona Malaika amekataa kuondoka naye, kwa hasira akaondoka zake. Kwanza alitaka kwenda kutafuta chumba Magomeni ili pale atakapomwambia Malaika kwamba wanaondoka, basi ajue ni mahali gani walipokuwa wakienda.

Alizunguka Magomeni huku akiwaulizia madalali ambapo baada ya kumpata akaambiwa kwamba chumba kilikuwepo kwa mzee Masharubu hivyo kwenda kukiona. Kilikuwa chumba kizuri, akakipenda na hivyo na hivyo kulipia, akaacha kila kitu humo na kurudi Ilala mikono mitupu kwa ajili ya kumchukua Malaika na kuondoka naye.

“Nimesema siondoki mpaka uniambie kwanza,” alisema Malaika.

“Sawa. Ngoja nikwambie,” alisema Ibrahim.

Hakutaka kumficha, alimpenda, alikuwa msichana wake ambaye alimchukulia kama mke wake, akamwambia jinsi hali ilivyokuwa tangu hatua ya kwanza mpaka alipokuja kuiba kiasi kile cha fedha na kuondoka nacho.

Malaika aliogopa, alitetemeka, hakujua vitu hivyo aliibiwa nani, hakujua mwenyewe angechukua hatua gani kama angemgundua kwamba yeye ndiye aliyeiba vitu hivyo.

“Posta kubwa mpenzi! Hawawezi kunijua. Tuondoke,” alisema Ibrahim huku akionekana kuwa na uhakika kwamba kusingekuwa na mtu yeyote ambaye angemgundua.

Malaika akakubaliana naye na kuondoka mahali hapo. Walikuwa wakitembea kwa mwendo wa taratibu, walikuwa wakizungumza mambo mengi, walipanga biashara zao ambazo walitakiwa kuzifanya wakiwa huko. Walipigwa na maisha na waliamini kwamba pesa zile zingeweza kuyabadilisha maisha yao.

Huku wakiwa wamefika Ilala, ghafla gari moja likafunga breki pembeni yao, hawakujua walikuwa wakina nani, waliduwaa, walilishangaa gari hilo ambalo ghafla likafunguliwa milango, wanaume wawili wakatoka, wakawafuata na kuwakamata wote wawili, hawakutaka kuwauliza maswali yoyote yale, wakawapakiza ndani ya gari.

Watu waliokuwa njiani walikuwa wakishangaa, hawakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea. Mara ya kwanza walihisi ni watu waliokuwa wakiigiza, lakini baada kupakizwa ndani ya gari na kuondoka mahali hapo wakagundua kwamba watu hao hawakuwa wakiigiza bali lilikuwa tukio la utekaji lililokuwa likitokea mahali hapo.

Malaika alikuwa akilia, hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea, alipiga kelele lakini ghafla akashtukia akizabwa vibao vitatu mfululizo, damu zikaanza kumtoka mdomoni kwani vibao vile vya shavu viliuchana mdomo wake kwa ndani.

“Nyamaza nguruwe weee,” alisema Jumanne huku akimwangalia Malaika kwa macho ya hasira.

“Tumefanya nini bro?” aliuliza Ibrahim lakini badala ya kujibiwa swali hilo, akaanza kupigwa ngumi za mbavu mfululizo.

Wote wakaamriwa kunyamaza, hawakutakiwa kuzungumza kitu chochote ndani ya gari. Watu hao walionekana kuwa na hasira mno, viunoni mwao walikuwa na bastola, walikuwa tayari kufanya kitu chochote kile kama tu wangeambiwa na David wakifanye.

“Mkuu! Tumempata mtuhumiwa!” alisema Jumanne wakati akizungumza na David kwenye simu.

“Safi sana! Kompyuta mmeipata?”
“Bado! Ndiyo tunataka atupeleke ilipo. Tukiipata tufanye nini bosi?” aliuliza Jumanne.

“Muueni!”
“Ila tumemkuta na demu wake, itakuwaje?” aliuliza Jumanne.

“Waueni wote wawili na miili yao muende mkaitupe,” alisema David na kukata simu.

Hayo ndiyo yalikuwa maagizo waliyokuwa wamepewa, wakamuuliza Ibrahim mahali kompyuta ilipokuwa, akawaambia kwamba aliiweka katika chumba kimoja kilichokuwa Magomeni. Wakamwambia waende huko na hivyo safari ya kwenda huko ikaanza.

Hawakuchukua muda mrefu wakafika Magomeni Mapipa ambapo wakaenda mpaka katika nyumba aliyopanga Ibrahim na kisha kumwambia apige hodi. Mlango ulipofunguliwa, wakabadilika, wakajifanya kuwa marafiki wa David na hivyo kuelekea chumbani.

Ilikuwa ni vigumu kugundua kwamba Jumanne alikuwa adui mkubwa wa Ibrahim kwani walikuwa wakizungumza kwa furaha kana kwamba hakukuwa na jambo baya lililokuwa nyuma yao.

Wakaingia mpaka chumbani, kulikuwa na mfuko uliokuwa na kompyuta hiyo lakini pia kulikuwa na bahasha. Hakutaka pesa, kitu muhimu kilikuwa ni ile kompyuta. Akaichukua na kisha kutoka ndani ya chumba kile na kurudi garini ambapo Fred alibaki na Malaika.

“Jamani! Si mmekwishapata mnachokitaka. Naomba mtuache,” alisema Ibrahim huku akilia kama mtoto.

“Bado kuna kazi! Tunaelekea msitu wa Pande kwenda kufundishana adabu kidogo ili iwe fundisho,” alisema Jumanne huku akijigusa kiunoni kuona kama bastola yake ilikuwepo.

Safari ya kuelekea katika msitu wa Pande ikaanza. Ibrahim na Malaika hawakujua kulikuwa na kitu gani lakini mioyo yao ilihisi kabisa kwamba walikuwa wakienda kuuawa. Walijitahidi kuomba msamaha lakini hawakusamehewa, watu hao walitaka kutekeleza maagizo waliyopewa na bosi wao kwamba ni lazima wawaue.

“We have to kill them both, that is an order from the big boss,” (Inabidi tuwaue, hiyo ni amri kutoka kwa bosi mkuu) alisema Jumanne kwa Kiingereza kwa kuamini kwamba mateka wao hawakuwa wakielewa.

“No problem,” (hakuna tatizo) alijibu Fred huku safari ikiendelea kama kawaida, na muda huo tayari walikuwa wanakaribia Mbezi kwa Msuguri.

****

David alikuwa kimya sebuleni kwake, masikio yake aliyategesha katika simu yake, alikuwa akisikilizia ni kitu gani kingetokea baada ya kuwatuma vijana wake kwa ajili ya kumuua kijana ambaye alimuibia pesa zake na laptop yake ambayo ilikuwa muhimu kuliko kitu chochote kile.

Alitaka kusikia kwamba kijana huyo amekufa kwani hakutaka kuona akiendelea kuishi kutokana na kile alichokuwa amekifanya ambacho kwake kilionekana kama kumpotezea muda na baya zaidi kumpotezea marafiki zake ambao mambo yao mengi alikuwa ameyahifadhi katika kompyuta ile.

Japokuwa aliambiwa kwamba angepigiwa simu lakini aliona kama vijana hao wanachelewa na hivyo kuwa na kimuhemuhe cha kutaka kuwapigia na kusikia ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea huko.

Akaichukua simu yake na kumpigia Jumanne ambapo baada ya kupokea akamwambia kwamba kila kitu kilikuwa tayari na kijana huyo alitekwa akiwa na msichana, akaagiza kwamba wote hao ilikuwa ni lazima wauawe.

“Haina shida,” alisema Jumanne.

Akarudi kwenye kiti chake, akashusha pumzi ndefu na kukunja nne, hatimaye kile alichokuwa amekihitaji kilifanyika na hivyo kilichokuwa kikisubiriwa ni kitu kimoja tu, kuwaua watu hao na maisha yake kuendelea.

Akaendelea kusubiri zaidi, baada ya saa moja akaona simu yake ikianza kuita, kwa haraka sana akaichukua na kuangalia namba, simu ilikuwa ikitoka kwa Jumanne, haraka sana akaipokea.

“Imekuwaje?” aliuliza huku akiwa na presha ya kutaka kujua kilichotokea.

“Tumemaliza, hakukuwa na ugumu wowote ule, tumefumua vichwa vyao,” alisikika Jumanne kutoka upande wa pili.

“Safi sana.”

“Hakikisha unakaa kwenye televisheni bosi kuangalia, manake kwa tulivyofanya, vyombo vya habari vitatangaza sana mwaka mzima,” alitamba Jumanne.

“Safi sana. Hiyo ndiyo adhabu yao wote wawili japokuwa hako kasichana hakakuhusika ila kaache nako kafe,” alisema David, akafurahi sana na kisha kukata simu.

****

Richard alibaki akiwa anatetemeka pale kitini alipokuwa amekaa, hakuamini kama kweli mke wake angejifungua salama au la, muda wote alionekana kuwa na hofu tele na wakati mwingine aliikutanisha mikono yake na kumuomba Mungu amfanyie muujiza ili mkewe ajifungue salama salimini.

Alimwangalia dada wa kazi, kwa jinsi alivyoonekana, alionekana kuwa na hofu kubwa, alihisi kwamba wakati mkewe akifikishwa katika hospitali hiyo hakuwa mzima kiafya, hakuwa na dalili za kupona kama ilivyokuwa kwa wanawake wengine.

Wakati akiwa amekwishakata tamaa, mara mlango ukafunguliwa na daktari kutoka ndani ya chumba kile. Haraka sana Richard akasimama na kumsogelea, alitaka kujua ukweli juu ya kile kilichokuwa kikiendelea mule ndani.

Uso wa daktari huyo ulimpa majibu yaliyomvunja moyo, hakuonekana kuwa na furaha, amani, na hata mlango ulivyokuwa wazi, kama mkewe alijifungua salama ilikuwa ni lazima angesikia sauti ya mtoto akilia, cha ajabu kabisa, chumba kilikuwa kimya.

“Nini kimetokea? Mke wangu amejifungua salama?” aliuliza David huku akimwangalia daktari huyo.

“Njoo ofisini kwangu!”

Richard hakuwa na la kufanya zaidi ya kumfuata daktari huyo. Moyo wake ulikuwa na hofu kubwa, hakuamini kama mke wake alijifungua salama, alijua kulikuwa na tatizo kubwa na ndiyo maana daktari hakutaka kumwambia akiwa nje ya chumba kile.

Hakumfuata peke yake bali hata mtunza bustani na dada wa kazi wote walisimama na kumfuata daktari huyo ambapo baada ya kuingia ndani ya ofisi hiyo, wakakaribishwa katika viti na kutulia, wakabaki wakimwangalia daktari huyo.

“Kwanza pole sana,” alisema daktari huyo.

Hakutaka kumficha kitu chochote kile, alimwambia ukweli kwamba yeye na madaktari wenzake walijitahidi sana kuokoa maisha ya mke wake na mtoto lakini wakafika kipindi ambacho walitakiwa kumuokoa mtu mmoja na mwingine afe kwani Bianca alikuwa amepoteza damu nyingi na alipata tatizo kidogo katika mfumo wake wa uzazi.

“Tukaona ni bora kuyaokoa maisha ya mama,” alisema daktari huku akimwangalia Richard.

“Kwa hiyo mtoto wangu amekufa? Mtoto wangu amekufa?” aliuliza Richard huku akilia kama mtoto, machozi yalitiririka mashavuni mwake.

“Pole sana,” alisema daktari huyo.

Richard hakuacha kulia, moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali, hakuamini kile kilichokuwa kimetokea, alimpenda sana mke wake na alikuwa akijiandaa kupata mtoto wake wa kwanza. Walikuwa wamekwishamfanyia shopping hata kabla ya kuzaliwa. Moyoni mwake tayari alitengeneza upendo mkubwa kwa mtoto wake huyo ambaye kwa bahati mbaya sana, alifariki dunia japokuwa madaktari walijaribu kwa nguvu zao zote.

Hakubembelezeka, kitu alichokuwa akikizubiria kwa hamu muda huo kilikuwa ni mtoto tu. Alilia na kulia huku akilitaja jina la mtoto wake ambalo tayari alikuwa amelipanga. Baada ya kubembelezwa kwa nusu saa nzima, akatolewa ndani ya chumba kile na kuelekea kule kulipokuwa na benchi ambapo alikaa na kujiinamia chini huku akilia kwa kugugumia.

Hakutaka kumuona mtu yeyote zaidi mke wake, Bianca ambaye hakujua alikuwa kwenye hali gani kipindi hicho. Baada ya saa moja, Bianca akatolewa ndani ya chumba kile na kupelekwa katika chumba kingine.

Alikuwa kimya kitandani, dripu ya maji ilikuwa ikining’inia juu ya kitanda chake. Hakuwa na fahamu, hakujua kitu gani kilikuwa kikiendelea. Richard alipomuona mke wake, akasimama na kuanza kukisogelea kitanda kile. Alikuwa akilia kwa uchungu, hakuamini kile alichokuwa akikiona.

Mlango wa chumba kingine ukafunguliwa na yeye kutakiwa kubaki nje, alibaki akiwa amesimama nje ya mlango wa chumba hicho. Alikuwa akilia, kila kitu alichokuwa akikipitia wakati huo alihisi kama alikuwa katika njozi fulani ya kusisimua ambapo baada ya muda angeshtuka na kujikuta akiwa kitandani.

“Bianca mke wangu!” aliita Richard kwa sauti ya chini, machozi yaliendelea kumtiririka mashavuni mwake.

 

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Ijumaa hapahapa.

Toa comment