The House of Favourite Newspapers

MPENZI WANGU SARAFINA-16

0

Safari ilikuwa ikiendelea kuelekea katika Msitu wa Pande, kitu kilichokuwa kichwani mwao ni kufanya mauaji kwa watoto hao bila kuwaonea huruma. Mawingu yalijikusanya angani na baada ya dakika chache, manyunyu yakaanza kudondoka na hatimaye mvua kubwa kuanza kunyesha.

Hilo halikuwazuia kusonga mbele, ilikuwa ni lazima kuhakikisha kwamba wanafanya kile walichotakiwa kufanya. Safari iliendelea na walipofika sehemu ambayo ilionekana kuwa nzuri kuingia upande wa wa msitu huo, gari likakatwa kona na kuingia humo.

Ibrahim alikuwa kimya, kipigo alichokuwa amepewa kilimchosha kupita kawaida. Alivimba, aliamua kunyamaza kwani kama kuomba msamaha, alijitahidi sana kufanya hivyo lakini hakukuwa na mtu aliyejali chochote kile.

Wakati wakiwa wameingia msituni, ghafla hali ya ajabu ikaanza kumshika Malaika, akaanza kutetemeka pale alipokuwa na ndani ya sekund chache akaanza kupiga kelele za maumivu makali.

Kila mmoja alishangaa, kabla walihisi kwamba alikuwa akijifanyisha lakini walivyomwangalia, alionekana kuhisi maumivu makali. Mwili wake ukaanza kuvimba, akazidi kutetemeka kama mtu aliyekuwa akisikia baridi kali.

Damu zikaanza kumtoka puani. Hali ilionekana kutisha, japokuwa Fredi na Jumanne walikuwa na roho za kinyama lakini wakaanza kumuonea huruma msichana huyo ambaye hapohapo akaanguka na kuanza kukakamaa mwili.

“Kuna nini?” aliuliza Fredi huku akiendesha gari.

“Hata mimi sijui! Wewe, mwenzio mgonjwa huyu?” aliuliza Jumanne.

“Sijui! Nashangaa! Sikuwahi kumkuta kwenye hali hii hata siku moja,” alisema Ibrahim huku akionekana kuogopa, akamsogelea Malaika pale chini, msichana huyo aliendelea kukakamaa huku damu zikimtoka na macho yake kuanza kuwa mekundu kama yaliyokuwa yakikusanya damu nyingi.

“Malaika! Malaika! Malaika!” aliita Ibrahim huku akianza kulia.

Hakukuwa na safari ya kuingia zaidi msituni, Fredi akalisimamisha gari lake na kuanza kurudi walipotoka. Walikuwa wakienda kuwaua watu hao, japokuwa naye alitakiwa kuuliwa lakini hali aliyokuwa nayo ilimuumiza kila mtu.

Wakarudi barabarani, wakasimisha gari na kumwambia Ibrahim ateremke na Malaika huku mvua kubwa ikipiga nje. Ibrahim hakuwa na jinsi, akamchukua Malaika wake, akamshusha kutoka garini na kumuweka kwenye lami.

“Bro! Mbona mnataka kutuacha! Mbona mnanichia majanga?” aliuliza Ibrahim huku akilia, kila alipomwangalia mpenzi wake, Malaika moyo ulimuuma mno.

“Baki naye, utaomba msaada! Msaada pekee tuliowapa ni kuwaacheni hai!” alisema Jumanne na Fredi kuliondoa gari mahali hapo ambapo baadaye akampigia simu David na kumwambia kwamba tayari waliwaua watu hao kwa kuamini kwamba wasingeonana tena katika maisha yao.

Ibrahim akabaki na Malaika wake, aliangalia kila upande, hakukuwa na magari mengi yaliyokuwa yakipita na hata yale machache yaliyokuwa yakipita mahali hapo hayakuwa yakisimama hata kidogo.

Alishindwa kujua afanye nini, kila alipomwangalia Malaika, moyo wake ulimwambia kwamba hiyo ndiyo ilikuwa siku ya mwisho za uhai wa msichana huyo mdogo ambaye tangu kuzaliwa kwake, alikuwa mtu wa kuteseka tu.

“Malaika usiniache! Usiniache Malaika subiri niendelee kusimamisha magari,” alisema Ibrahim huku akiwa amemuinamia msichana huyo na mvua kali ikiendelea kunyesha.

Ibrahim hakutaka kuacha, bado alihitaji msaada mkubwa kutoka kwenye gari lolote lile, alimwangalia msichana Malaika, alionyesha kabisa kwamba alikuwa akienda kufa kwani kwa jinsi mwili wake ulivyokuwa, alionekana kutokuwa na muda mwingi wa kuendelea kuishi.

Magari hayakusimama, yaliendelea kuwapita. Uamuzi wa mwisho kabisa alioufanya Ibrahim ni kumbeba Malaika na kumuweka katikati ya barabara na kusimama karibu yake, alitaka kuona gari lolote ambalo lingepita alisimamishe.

Wala hazikupita dakika nyingi, gari ndogo aina ya Spacio likaonekana mbele yake. Ibrahim akapunga mikono juu kama kulisimamisha gari hilo. Alikuwa akipiga kelele ili aonekane kwani kama asingelisimamisha na gari hilo kupita, ilimaanisha lingemgonga yeye na msichana Malaika aliyelala chini.

Ilikuwa ni kama bahati, dereva wa gari hilo akamuona, akafunga breki kwa nguvu na gari kusimama kama mita tatu kutoka pale aliposimama Ibrahim. Hakutaka kusikia lolote, akambeba Malaika na kulifuata gari hilo ambapo dereva akafungua kioo.

“Vipi?” aliuliza dereva huyo.

“Naomba mtusaidie! Malaika anakufa,” alisema Ibrahim, hapokuwa alikuwa na moyo wa kushujaa lakini alishindwa kujizuia, akaanza kulia, machozi yake hayakuonekana kutokana na mvua iliyokuwa ikiendelea kunyesha.

Dereva huyo mwanaume akamwangalia Malaika, kwa jinsi alivyoonekana, alikuwa kama mfu. Alitaka kumwambia Ibrahim asijisumbue sana kwa kuwa rafiki yake alikuwa amekufa lakini hakutaka kumuumiza.

Akamfungulia mlango na kuingia ndani, akabaki akimshangaa Malaika, alionekana kuwa binti mdogo lakini hali aliyokuwa nayo ilimtisha mno.

“Imekuwaje?” aliuliza dereva huyo.

“Naomba utupeleke hospitali! Malaika wangu atakufa,” alisema Ibrahim huku akilia kama mtoto.

Kwa hali aliyokuwanayo Malaika hakukuwa na la kupoteza mahali hapo, kwa haraka sana akapiga moto na kuondoka mahali hapo kwa kasi. Alikuwa na jukumu la kuyaokoa maisha ya msichana huyo mdogo, mvua kubwa iliendelea kunyesha lakini hilo halikumfanya kupunguza mwendo, aliendelea kusonga mbele kwa mwendo wa kasi.

Akafika Kibamba katika Hospitali ya Dk. Faroukh, akaliingiza gari ndani ya hospitali hiyo ambapo machela ikaletwa haraka sana na msichana huyo kuwekwa juu yake na kusukumwa kuelekea ndani ya jengo la hospitali hiyo.

“Mmh! Jamani! Kuna nini tena?” aliuliza nesi mmoja, alivyokuwa akimwangalia Malaika katika machela ile, aliogopa kwani kwa jinsi alivyokuwa, alionekana kama tayari alikuwa mfu.

“Hali ni mbaya! Naomba muokoe afya ya binti huyu,” alisema dereva.

Malaika akapelekwa mpaka katika chumba cha upasuaji na kuingizwa humo. Hawakuangalia pesa, kitu cha kwanza kabisa walichokijali kwa wakati huo ni hali ya msichana huyo mdogo.

Alipofikishwa ndani, madaktari wawili wakaingia, waliguswa kumuhudumia msichana huyo mdogo ambaye alionekana kuhitaji msaada hasa. Ibrahim na dereva yule hawakutakiwa kuingia ndani, wakabaki nje kwenye benchi huku wakisikilizia ni kitu gani kingeendelea huko.

Ibrahim alikuwa akilia mno, kwake, kila alipoangalia hakuona kabisa kama kulikuwa na dalili za mpenzi wake kupona. Alikata tamaa na aliona kabisa huo ndiyo ulikuwa mwisho wa msichana huyo mrembo.

“Mungu naomba umsaidie! Naomba umponye Malaika wangu,” alisema Ibrahim huku akiwa amejiinamia.

Muda ulizidi kwenda mbele, dakika zikakatika na mlango wa chumba kile haukufunguliwa. Kila mmoja akahisi kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wa msichana yule ila baada ya saa moja, ukafunguliwa na daktari kutoka.

Uso wake tu ukaonyesha kile kilichokuwa kimeendelea ndani ya chumba kile hakikuwa kizuri, alionekana kukata tamaa, alionekana kama mtu ambaye alijitolea sana lakini mwisho wa siku hakufanikiwa kwa kile alichokuwa amekikusudia.

Akawaangalia Ibrahim na dereva waliokuwa nje ya chumba kile kwenye benchi na kuwaomba kumfuata. Wakamfuata mpaka taika ofisi yake ambapo huko hakutaka kuwaficha, aliwaambia ukweli kwamba Malaika alikuwa kwenye hali mbaya, alikuwa akiumwa ugonjwa ambao kama angevuka salama miaka kumi na nane, angepona kabisa kwani asilimia tisini na tano walikuwa wakifa kabla ya kuvuka umri huo.

“Anaumwa nini?” aliuliza dereva.

“Sickle cell!”

“Sickle cell?”
“Ndiyo!”

Dereva akashusha pumzi nzito, akamwangalia Ibrahim ambaye hata ugonjwa huo hakuwa akiufahamu, na mbaya zaidi hakuwahi hata kuusikia. Hakujua ulikuwa ugonjwa wa nini, hakujua ni kwa jinsi gani ugonjwa huo ulikuwa ukiathiri mwili wa mgonjwa.

Sickle Cell ulikuwa ni miongoni mwa magonjwa mabaya yaliyokuwa yakiua watu wengi duniani hasa watoto. Mtu aliyekuwa na ugonjwa huu, mara nyingi ilikuwa ni lazima afe kama tu hatofikisha umri wa miaka kumi na nane na kuvuka salama.

Ugonjwa huu ambao husababisha damu kupungua kwa kiwango kikubwa, tena mara kwa mara mwilini mwa mgonjwa, ulikuwa gumzo nchini Tanzania kipindi hicho. Ugonjwa huo unapokomaa, mwili wa mgonjwa hudhoofika na kusikia maumivu makali.

Ni ugonjwa unaohitaji damu nyingi kwani mgonjwa anaweza kuwa na damu ya kutosha leo hii asubuhi na jioni akaonekana kutokuwa na damu ya kutosha kutokana na seli hai nyekundu kuzishambulia seli ambazo hupeleka damu katika mifupa.

“Atapona?” lilikuwa swali la kwanza alilouliza Ibrahim.

“Kupona atapona ila….”

“Ila nini daktari!”
“Sijajua kama atafikisha umri wa miaka kumi na nane. Kwa kifupi, katika kipindi hiki cha maisha yake kitakuwa ni kipindi chenye mateso sana. Atahitajika kula sana vyakula vya kuongeza damu lakini pia vilevile atatakiwa kwenda hospitali kuongeza damu mara kwa mara, hata kwa wiki mara kumi, vinginevyo, atakufa,” alisema daktari huyo ambaye hakutaka kuficha chochote kile.

“Hivyo tu halafu atapona moja kwa moja.”
“Kama atavuka miaka kumi na nane akiwa hai, ugonjwa utapona na ataishi ila kama hatovuka basi atakufa kwani ugonjwa huu huwa haumruhusu mtu kuvuka miaka hiyo, kwa bahati akivuka, na ugonjwa unapona moja kwa moja,” alisema daktari huyo maneno yaliyomfanya Ibrahim kushusha pumzi nzito.

Leave A Reply