The House of Favourite Newspapers

MPENZI WANGU SARAFINA-17

0

Malaika alikuwa kitandani, mwili wake haukuwa na nguvu, kwa juu, dripu ya damu ilikuwa ikining’inia. Aliyafumba macho yake, wakati mwingine aliyafumbua na kuangalia huku na kule.

Alikuwa kwenye maumivu makali mno, pale kitandani alipokuwa, hakuacha kulia, aliumia na alihisi maumivu makali katika mifupa yake. Ugonjwa huo ulikuwa ukimtesa kupita kawaida, alionekana kukata tamaa na kila alipoangalia maisha yake ya mbele, alihisi kabisa kwamba alikuwa akiend kufa.

Ibrahim ambaye alikuwa akiingia ndani ya wodi ile, alipokuwa akimwangalia msichana wake, moyo wake ulichoma kupita kawaida. Hakuamini kama hizo ndizo zilikuwa hatua za mwisho za msichana huyo.

Wakati mwingine alikataa kabisa kukaa karibu naye kwani kwa jinsi msichana huyo alivyokuwa akilalamikia maumivu makali ya mifupa ilimfanya kutamani kulia, ili kupusha uchungu mkubwa moyoni mwake, wakati mwingine alikuwa akiondoka kabisa.

Kipindi hicho kilikuwa ni cha mateso makali, aliendelea kukaa hospitalini hapo kwa siku mbili ndipo akaruhusiwa huku akiwa amekwishawekewa damu ya kutosha. Kitu kimoja alichokuwa akihitaji kukifahamu sana ni sababu iliyowafanya kutokuuawa na watu wale.

Hakukumbuka kitu chochote ambacho kilitokea msituni. Alichokikumbuka ni kwamba walikuwa ndani ya gari, wanaume wale walisema kwamba walikuwa wakienda kuwaua ila cha ajabu kabisa mpaka muda huo wote walikuwa hai.

“Nini kilitokea?” aliuliza Malaika.

“Walituacha baada ya kuona upo hoi,” alijibu Ibrahim huku akimwangalia Malaika.

“Kweli?”
“Ndiyo! Unajisikiaje lakini?” aliuliza Ibrahim.

“Kidogo nafuu! Ila wakati mwingine mifupa inauma mno,” alisema Malaika.

Ibrahim aliumia, muda mwingi maneno ya daktari yalikuwa yakimjia kichwani mwake, akakosa amani, akakosa furaha na kujua kwamba mpenzi wake huyo kuna siku angekufa, na hata kwa jinsi walivyokuwa wakifurahia maisha, kuna siku msichana huyo asingekuwa mikononi mwake.

Hakutaka kumwambia, alijua ni kwa namna gani msichana huyo angeumia kama tu angemwambia ukweli juu ya kile kilichokuwa kimetokea. Hakuishi kwa furaha tena, hata msichana huyo alipokuwa akimwambia maneno mazuri ya matumaini lakini bado kumbukumbu zake zilikuwa palepale kwamba ilikuwa ni lazima msichana huyo afariki dunia.

Hawakuwa na maisha ya kitajiri, zile pesa alizokuwa ameziiba Ibrahim ndizo ambazo ziliyaendesha maisha yao. Alikuwa na akili ya biashara, alijua kabisa kwamba kwa kiasi alichokuwa nacho ingekuwa kazi nyepesi kabisa kama angeanzisha biashara na kufanikiwa.

Hakuwa na umri mkubwa, wakati Malaika akiwa na miaka saba, yeye alikuwa na miaka kumi na sabab hivyo kidogo akili yake ilikuwa imepanuka vya kutosha. Akafungua genge la kuuza mbogamboga za majani, hakuishia hapo, akaamua kununua toroli na madumu na kuanza kuuza maji.

Aliamini kwamba kupitia biashara hizo zingeweza kumsaidia. Ndani alibakiza kiasi cha milioni tano na alitaka kuona kiasi hicho kikiendelea kukua na si kupungua kwani kama kuyahatarisha maisha yake kwa ajili ya pesa hizo aliyahatarisha hivyo hakuona kama kulikuwa na sababu ya kuzitumbua pesa hizo.

“Ibrahim, naomba uniambie kitu kimoja,” alisema Malaika huku akimwangalia Ibrahim.

“Kitu gani?”
“Kwa nini huna furaha siku hizi?” aliuliza Malaika.

“Nani? Mimi?”
“Kwani kuna nani mwingine hapa?”
“Malaika! Nafikiria zaidi maisha, ni kwa jinsi gani maisha yetu yataendelea kwenda mbele. Hivi huoni jinsi tunavyoishi kwa shida kidogo? Tuna pesa, nafikiria ni kwa jinsi gani nitaweza kufungua biashara nyingi,” alisema Ibrahim, alitoa maelezo mengi ambayo hayakuwa na maana.

“Bado hujanipa jibu ninalolitaka,” alisema Malaika.

Moyoni mwake alianza kuhisi kitu, akajua kwamba kulikuwa na kitu ambacho mwanaume huyo hakutaka kumwambia. Aliyahofia maisha yake, alijua kwamba kulikuwa na uwezekano wa kufa na ndiyo maana mwanaume huyo hakutaka kumwambia ukweli.

Ibrahim alijikaza kiume, wakati ameulizwa swali hilo, hakutaka kuonyesha majonzi yoyote yale japokuwa bado kumbukumbu za maneno aliyoyasema daktari zilikuwa zikijirudia kichwani mwake.

Hali ya Malaika haikubadilika, katika kipindi cha mvua ambacho kilikuwa na baridi kali alikuwa akilalamika maumivu ya mifupa hasa katika uti wa mgongo, alihisi kabisa pingili za uti wa mgongo zilikuwa zikiachia.

Yalikuwa ni maumivu makubwa, akawa akipelekwa hospitalini ambapo huko, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuongezewa damu kwani ilikuwa ikipungua kwa kasi kubwa mno.

Hayo yalikuwa ni maisha ya mateso, ugonjwa wa sickle cell uliendelea kuyatesa maisha yake kiasi kwamba kuna wakati aliomba kufa kwani mauamivu aliyokuwa akiyasikia hayakuwa yakielezeka.

“Hizi Folic Acid zitaweza kumsaidia, cha msingi awe anakunywa kidonge kimoja kwa siku,” alisema daktari, alikuwa akimwambia Ibrahim.

Folic Acid zilikuwa moja ya dawa zenye nguvu ambazo alitakiwa kunywa mgonjwa aliyekuwa akiumwa ugonjwa huo. Wakati seli hai nyekundu za damu zinapokuwa zikipambana kuhakikisha damu haipungui, dawa hiyo ndiyo inayozisaidia seli hizo katika mapambano hayo.

Ilikuwa kazi kubwa, mwili ulikiwa kuwa na damu ya kutosha. Kila siku kazi ya Malaika ilikuwa ni kunywa vidonge hivyo ambavyo viliuzwa kwa bei ya juu lakini kwa kuwa Ibrahim alikuwa na pesa, hilo halikuonekana kuwa tatizo.

“Kuna siku utapona tu!” alisema Ibrahim huku akimwangalia Malaika aliyeonekana kukata tamaa kabisa.

“Kweli?”
“Ndiyo!”
“Ila nimesikia huu ugonjwa mbaya sana!”

“Hakuna. Si ugonjwa mbaya! Ni ugonjwa wa kawaida ambao unaweza kupona kabisa,” alisema Ibrahim huku akimwangalia Malaika.

Hiyo ndiyo ilikuwa kazi kubwa aliyokuwa nayo. Kila siku ilikuwa ni lazima amtie moyo kwani pasipo kufanya hivyo ilimaanisha kwamba binti huyo angekufa kwa kuwa tu angekata tamaa mbele yake alingeona giza.

Kidogo Malaika akafarijika, kwake, kitu kilichompa tumaini la kuishi kwa kipindi kirefu kilikuwa ni maneno ya mwanaume huyo. Alimpenda kutoka moyoni mwake, na kila siku alimwambia kwamba hakuogopa kufa bali kitu pekee alichokuwa akikiogopa moyoni mwake ni kumpoteza tu.

“Kweli?”

“Ndiyo! Siogopi kufa tena! Kitu pekee ninachokiogopa ni kukupoteza mpenzi,” alisema Malaika huku akimwangalia mpenzi wake huyo aliyeonekana kuwa kwenye mapenzi ya dhati.

****

Maisha ya David yalikuwa ni kula bata tu, kila siku alikuwa mtu wa kusafiri kusafirisha madawa ya kulevya. Aliingiza kiasi kikubwa cha pesa na Bwana Mpobela alikuwa akimtegemea kwani mbali na kusafirisha huko, David alikuwa mjanja, viwanja vya ndege kulipoonekana kuna noma, alitumia kila ujanja hata kusafirisha kwa meli ya mizigo lakini mwisho wa siku mzigo ufike salama.

Mpaka katika kipindi hicho, mke wake, Gloria hakujua kitu chochote kile, alidanganywa vya kutosha na kuona kwamba mume wake huyo alikuwa mfanyabiashara ambaye alikuwa akisafiri safiri.

Biashara ilikuwa, watumiaji wa madawa ya kulevya wakaongezeka. David akatanua utajiri wake, akaanza kuvuma jijini Dar es Salaam kwamba alikuwa bilionea aliyekuwa akichipukia.

Baada ya miaka miwili kufanya biashara hiyo, David akaanza kuvutika na utumiaji wa madawa ya kulevya. Alikuwa akishangaa, vijana wengi walikuwa wakitumia madawa hayo na kuyasifia, mzigo mkubwa aliokuwa akiupeleka Tanzania ulikuwa ukimalizika kwa kipindi kifupi sana hali iliyomfanya kugundua kwamba kulikuwa na watumiaji wengi waliokuwa wameongezeka.

Alitaka kujua kuhusu madawa hayo, kama kuna wengi walikuwa wakivuta na kuendelea kuishi, kwa nini na yeye asijaribu kufanya hivyo? Hapo ndipo alipoanza kujiingiza katika utumiaji wa madawa hayo.

Hakutaka kumwambia mkewe, alifanya kificho, siku za kwanza zilionekana kuwa za mateso lakini baada ya wiki moja ya kutumia, akavutiwa mno na madawa hayo. Kila alipokuwa akivuta, akili yake ilihama, alijiona kuwa na nguvu kubwa, alijiamini na alihisi kuwa na uwezo wa kufanya jambo lolote lile.

Hiyo ilikuwa ndiyo stimu yenyewe. Alipokuwa akivuta, alijifungia hotelini na kuanza kubwia unga mdogomdogo kitu kilichomfanya kujisikia hali ya tofauti kuliko kipindi cha nyuma.

Taratibu akawa anaingia katika mkumbo wa matumizi ya madawa hayo, wakati mwingine hakuwa akifanya kazi nyingine zaidi ya kujifungia hotelini na kuanza kuvuta madawa hayo ambayo kwake yalionekana kuwa kitu bora na muhimu kuliko vyote katika dunia hii.

“Nilichelewa sana kujua hiki kitu! Kwa nini sikuambiwa mapema?” alijiuliza kila alipokuwa akitumia. Wakati mwingine alijihisi akiwa Marekani akizungumza na bilionea Bill Gates kuhusu kuinua hali ya uchumi wa Tanzania na wakati ukweli ni kwamba alikuwa nchini Tanzania, katika hoteli moja jijini Dar es Salaam.

 

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumatano hapahapa.

Leave A Reply