The House of Favourite Newspapers

Mpenzi Wangu Sarafina -23

0

Gloria alisimama mbele ya kitanda alichokuwa mume wake, mashavu yake yalilowanishwa na machozi yaliyokuwa yakimtoka, aliumia, hakuamini kama huo ndiyo ungekuwa mwisho wa mume wake aliyekuwa akimpenda.

Moyo wake ulichoma, japokuwa mwanaume huyo alikuwa mtumiaji wa madawa ya kulevya lakini kwake hakujali, alikuwa mume bora, aliyemfanya kuwa mwanamke bora ambaye kamwe hakutaka kumuona akiondoka mikononi mwake.

Alisimama huku akimwangalia, hakuwa mume wake, hakuwa akihema, alibadilika na kuwa marehemu. Madaktari wakfika katika kitanda hicho, walipogundua kwamba alikuwa amefariki wakamfunika kwa shuka la kijani na kuanza kumuondoa mahali hapo.

Wakati wakimtoa ndipo ile barua aliyoiandika David ikaanguka chini. Gloria akaichukua na kuanza kuisoma. Ilikuwa ni barua yenye kuchoma, iliyomtoa machozi mno moyoni mwake.

Alimkumbuka Sarafina, alimkumbuka yule mtoto aliyekuwa amebebwa, moyo wake uliumia mno na hakuamini kama kungekuwa na mwanaume ambaye angekuwa na moyo kama wa mume wake.

Alimsikitikia mwanamke yule, alijua kwamba Sarafina aliacha chuo kwa kuwa alikuwa na mimba, mimba ile aliitunza miezi yote na kujifungua, kwa kuwa hakuwa na maisha mazuri ndipo akaamua kuishi mitaani.

Alitakiwa kumlaumu mume wake lakini kutokana na mapenzi ya dhati aliyokuwa nayo moyoni, hakumlaumu zaidi ya kumuachia Mungu. Alilia, alihuzunika, macho yake yakawa mekundu mno kwa ajili ya kulia sana.

“Why did you do this?” (kwa nini ulifanya hivi?) aliuliza huku akiwa na barua ile mikononi mwake.

Huo ndiyo ulikuwa mwisho wa kila kitu, mume wake alifariki dunia na baada ya siku tatu wakamzika David katika makaburi ya Kinondoni jini Dar es Salaam.

****

“Juma…Juma fungua mlango!” alisema Ibrahim huku akiwa amesimama mlangoni, hakuonekana kujiamini, alikuwa akiangalia huku na kule kuona kama kulikuwa na watu waliokuwa wakimfuatilia.

Mlango ukafunguliwa na mwanaume mmoja, alivalia pensi nyekundu na juu hakuwa na nguo yoyote ile. Alibaki akimshangaa Ibrahim, hakumuelewa kutokana na mazingira yaliyokuwepo, mikononi mwake alikuwa na mtoto mdogo aliyekuwa akilia sana.

“Imekuwaje? Mbona mtoto? Kwani shemeji alikuwa na mimba?” aliuliza Juma huku akimshangaa Ibrahim.

“Subiri niingie ndani kwanza!” alisema Ibrahim na kuingia.

Juma hakuwa na majibu, kila alipomwangalia Ibrahim, alichanganyikiwa, hakujua ni kitu gani kilikuwa kimetokea mpaka mwanaume huyo kuja na mtoto. Alijua kabisa kwamba Malaika hakuwa na mimba, mbaya zaidi Ibrahim hakuwa na msichana mwingine kiasi cha kusema kwamba aliachiwa mtoto, sasa yule mtoto alitoka wapi?

“Imekuwaje na mtoto?” aliuliza Juma.

Hapo ndipo Ibrahim alipoanza kumwambia Juma kila kitu kilichotokea hospitalini, jinsi alivyomuona mtoto yule na kwenda kumchukua. Alimsimulia kila kitu na wote kugundua kwamba inawezekana manesi walikuwa wamepanga njama za kumuuza mtoto huyo kama hospitali nyingine zilivyofanya.

“Inabidi uwe na uhakika na hili! Rudi hospitalini!” alisema Juma.

“Hivihivi?”
“Badilisha nguo halafu vaa kofia!” alishauri Juma.

Hilo ndilo alilolifanya, alitaka kujua ni kitu gani kilikuwa kimetokea. Akabadilisha nguo na kuanza kurudi huko. Akasahau kuhusu mpenzi wake, Malaika, kitu kilichokuwa kichwani mwake ni mtoto yule aliyekuwa amempata.

Alipofika getini, walinzi hawakumgundua, akaingia mpaka ndani ambapo kule akakuta watu wakiwa wamekusanyana, wengine walikuwa wakijadili ishu ya mtoto iliyomfanya Ibrahim kusogea karibu ili apate ukweli juu ya kila kitu kilichokuwa kimetokea.

“Basi ndiyo hivyo! Jamaa kavimba ile kinoma. Hawa manesi siyo kabisa, wameiba mtoto bhana,” alisema jamaa mmoja.

“Kweli kabisa. Yaani unawezaje kuiba mtoto! Mtu anakuja ana mimba, mnamuhudumia, kapata mapacha halafu mnaiba mtoto mmoja, kweli haki hii?” alihoji jamaa mwingine.

“Siyo haki kabisa.”

“Kwa hiyo jamaa yupo wapi?” aliingilia Ibrahim.

“Kakamatwa! Kapelekwa polisi. Kapiga risasi kama kumi hivi,” alisema jamaa mwingine na kuongezea chumvi na wakati risasi iliyopigwa ilikuwa moja tu.

“Duuh! Yupo kituo gani?”
“Hapo Osterbay!”

Ibrahim hakutaka kubaki mahali hapo, akaondoka na kuelekea katika kituo hicho. Hakuchukua muda mrefu akafika huko, stori iliyokuwa ikibamba kituoni hapo ni juu ya mtoto aliyekuwa ameibwa.

Polisi wanawake walionekana kuchukia zaidi, walijua uchungu wa mwana, walipokuwa wakiwaona madaktari na manesi ambao walihusika katika wizi ule waliwaonyeshea chuki kubwa.

“Samahani bro!” alisema Ibrahim huku akiwa amemsogelea Richard.

“Naomba baadaye! Waandishi naomba mnihoji baadaye!” alisema Richard, kwa jinsi Ibrahim alivyoonekana, jinsi alivyovaa shati lake na kuchomekea kinadhifu, akahisi kwamba alikuwa mwandishi wa habari.

“Ila bro!”
“Naomba uniache!” alisema Richard kwa hasira, tena kwa sauti ya juu, hakuonekana kuwa sawa, akaelekea kaunta, baada ya dakika chache akatoka nje, akaingia ndani ya gari lake, akaliwasha na kuondoka kurudi hospitalini.

****

Hali ya Malaika ilikuwa mbaya kitandani, ugonjwa wa Sickle Cell uliendelea kumtesa, alikuwa akilia, muda wote ule aliona dhahiri kwamba alikuwa akienda kufa.

Madaktari walikuwa wakihangaika kuyaokoa maisha yake, hawakutaka kumpoteza binti huyo aliyekuwa na sura ya kipole, kwao, hakukuwa na kitu ambacho kingewauma kama kuona msichana huyo akifariki dunia.

Madaktari walikuwa wakiingia kwa zamu, walimuwekea dripu za damu kwani alikuwa amepoteza damu kwa kiwango kikubwa sana. Alitia huruma pale kitandani alipokuwa na kwa jinsi alivyokuwa akisikia maumivu, alimuona malaika mtoa roho akiwa ameingia wodini kwa ajili yake.

Alibaki akimuomba Mungu, alimshukuru kwa kila kitu, alijua dhahiri kwamba alikuwa akienda kufa lakini alitaka Mungu ampe nafasi ya kufanya mambo yaliyo mema, pale alipokosea, arekebishe na kufariki kwa amani kabisa.

Hakuwahi kuwa na maisha mazuri, siku zote maisha yake yalitawaliwa na umasikini mkubwa. Hakuwa na pesa lakini alimuomba Mungu amponye ili aweze kuwasaidia watu wengine, wale waliokuwa na matatizo, awasaidie watoke kwenye matatizo hayo waliyokuwa nayo.

Alimuomba Mungu kwa dakika kadhaa, machozi yalikuwa yakimtoka, moyo wake ulimuuma mno, ilikuwa ni kama Mungu alisikia kilio chake kwani baada ya kusema Amen, akahisi mwili wake ukianza kurudi katika hali ya kawaida, maumivu aliyokuwa nayo katika mifupa yake yakaanza kupotea.

Moyo wake ukawa na furaha kubwa, hakuamini kile kilichokuwa kikitokea, alilia sana, wakati mwingine alikuwa na hisia kwamba kulikuwa na mtu aliyekuja kitandani pale, alikuwa akimshika kuanzia miguuni mpaka kichwani, alitamani kuzungumza kitu lakini akauona mdomo wake kuwa mzito.

Alitaka kuuliza mtu huyo alikuwa nani lakini alishindwa kufanya hivyo. Mifupa ikaacha kuuma, alibaki akishangaa, ulikuwa ni muujiza ambao hakuwa ameutegemea maishani mwake kwani kwa kawaida mifupa yake ilivyokuwa ikiuma, mpaka kupata nafuu ilikuwa ikichukua muda mrefu.

“Ugonjwa huu ni kusudio langu ili upate kile nilichomuahidi mama yako siku moja,” alisikia sauti hiyo ikizungumza, ilikuwa ni kama pembeni yake kulikuwa na mtu aliyekuwa akimwambia maneno hayo.

Haraka sana akageuka upande wa kulia ambapo alihisi kulikuwa na mtu akiwa amesimama na kumwambia maneno hayo, hakukuwa na mtu na hakujua alikuwa nani.

Aliposikia sauti hiyo, ghafla maumivu ya mifupa yakaanza kurudi tena, kwa kasi mara mbili zaidi ya ile aliyokuwa nayo kipindi cha nyuma. Alilia kwa sauti, maumivu yalizidi, alihangaika pale kitandani, alirusha miguu yake huku na kule kiasi kwamba kila mtu aliyekuwa ndani ya wodi ile alihisi kwamba hiyo ndiyo ilikuwa dakika za mwisho za kuvuta pumzi ya dunia hii.

“Lete dripu nyingine, lete dripu nyingine,” alisema daktari aliyekuwa akimhudumia, haraka sana nesi mmoja akachomoka mahali hapo na kwenda katika benki ya damu ambapo baada ya sekunde hamsini akarudi akiwa na dripu nyingine ya damu.

Wakamuwekea harakaharaka, walikuwa wakijaribu kuyaokoa maisha yake, hawakujua sababu ya hali yake kubadilika ghafla kitandani pale alipokuwa. Baada ya kuwekewa dripu ile ya damu, kidogo akarudi katika hali yake ya kawaida, machozi yalikuwa yakimtoka huku akiwa ameyafumba macho yake.

Alitia huruma pale alipokuwa. Daktari yule na nesi hawakuondoka, walibaki mahali hapo wakiangalia kila kitu kilichokuwa kikiendelea mahali hapo.

“Is she going to die?” (atakufa?) aliuliza nesi huku akionekana kuwa na hofu kubwa.

“No! I guess God is going to do something!” (hapana! Nafikiri Mungu anakwenda kufanya jambo) alisema daktari huyo huku akimwangalia Malaika aliyekuwa kimya kitandani pale.

Wala hazikupita dakika nyingi, Ibrahim akaingia ndani ya wodi hiyo, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kutaka kujua hali ya mpenzi wake. Madaktari hawakumwambia kitu, walijua fika kwamba wangemshtua hivyo kumwambia kwamba alikuwa akiendelea vizuri na angeweza kuruhusiwa baada ya siku kadhaa.

“Alikuwa analia?” aliuliza Ibrahim.

“Ndiyo! Alikuwa akihitaji kukuona wewe!” alidanganya daktari.

“Na damu imepungua kwa kiasi kikubwa mpaka kuwekewa dripu ya pili?’ aliuliza Ibrahim huku akimwangalia Malaika.

“Ndiyo! Ila ni mzima!”
“Mmh!”

“Nini?”

Ibrahim alikuwa akimwangalia Malaika kitandani pale, kwa jinsi alivyoonekana ilikuwa ni vigumu kugundua kama msichana huyo alikuwa mzima. Alikuwa akipumulia mashine ya gesi, alionekana kuzidiwa na hata mapigo yake ya moyo yalivyokuwa yakidunda alionekana kama mtu ambaye alikuwa katika hatua za mwisho kuvuta pumzi ya dunia hii.

“Malaika! Ongea nami, Malaika usiniache peke yangu,” alisema Ibrahim huku akimwangalia msichana huyo kitandani pale.

“Usilie Ibrahim,” Ibrahim aliisikia sauti ya Malaika ikimwambia hivyo, ilikuwa ni sauti ya chini kabisa, ya kunong’oneza ambayo ilimshtua sana Ibrahim, akayainua macho yake na kumwangalia msichana huyo.

“Malaika…Malaika…” aliita.

“Usilie! Mungu anataka kufanya muujiza juu ya afya yangu,” alisema Malaika kwa sauti ya chini sana na kisha kutoa tabasamu pana, tabasamu lililowashtua hata madaktari wenyewe kwani lilikuwa tabasamu lililojaa matumaini makubwa kwamba ni kweli Mungu angekwenda kufanya muujiza juu ya afya yake.

 

Je, nini kitaendelea?
Tukutane kesho hapahapa.

Leave A Reply