Mpenzi Wangu Sarafina-25
Kwa Ibrahim, ni kama pua zake ziliziba, chumba kizima kilikuwa na harufu mbaya lakini hakusikia hata kidogo. Kila siku alikaa chumbani humo, mpenzi wake alionekana kukata tamaa, mwili wake ulizidi kuisha na vidonda vilimtesa kupita kawaida.
Hakuondoka chumbani, hakumkimbia, kila siku alipambana naye pamoja, alimtia nguvu na kumwambia kwamba kuna siku angepokea uponyaji na Mungu aliyaandaa maisha mazuri kwa ajili yake.
Malaika alilia na kulia, hakuwa na nguvu, kila alipomwangalia Ibrahim, aliyaona kabisa mapenzi ya mwanaume huyo, jinsi alivyompenda kiasi kwamba hakuwa tayari kumkimbia kwa kuwa tu alikuwa akitoa harufu mbaya.
Imani yake iliyoanza kuyumba kipindi cha nyuma ikaanza kurudi tena, alimwamini Mungu kwamba kuna siku angeweza kusimama tena, kutembea na kufanya mambo mengine kama kipindi cha nyuma.
Hakujua sababu ya Mungu kumpitisha katika maisha hayo, yalikuwa ni maisha yaliyoumiza mno, maisha ambayo yalimfanya kila siku kuona muda wowote ule angekufa kama alivyokufa mama yake. Hakuona kama angepokea tumaini lolote lile, alijua kabisa kwamba hizo ndizo zilikuwa siku za mwisho za uhai wake.
“Ibrahim mpenzi!” aliita Malaika huku akimwangalia mwanaume huyo.
“Ndiyo mpenzi!”
“Unaamini pamoja na mimi kwamba nitapona?” aliuliza Malaika huku akimwangalia Ibrahim, kwa kukiangalia kitanda harakaharaka, tena katika kipindi ambacho Malaika alikuwa amejifunika shuka, ilikuwa vigumu kuamini kama kitandani hapo kulikuwa na mtu kwa jinsi alivyokonda na kubaki mifupa mitupu.
“Ninaamini kwamba Mungu atakuponya! Huwezi kufa Malaika,” alisema Ibrahim huku machozi yakimtoka, alikosa tumaini, hakujua ni kwa jinsi gani angeweza kumsaidia msichana huyo maishani mwake.
“Hata mimi naamini nitapona. SITOKUFA BALI NITAISHI,” alisema Malaika kwa imani kubwa kutoka moyoni mwake, kama Mungu alikuwa akitenda miujiza kwa kuwa tu watu waliamini, aliamini kwamba hata yeye pia angeweza kumfanyia muujiza huo.
Kila siku wapangaji walikuwa watu wa kulalamika, walimlalamikia mwenye nyumba kwamba Malaika hakutakiwa kuishi ndani ya nyumba hiyo kwani kwa jinsi alivyokuwa akinuka, ilikuwa ni balaa tupu.
Mwenye nyumba hakutaka kuwasikiliza, aliyajua maisha ya msichana huyo, jinsi alivyokuwa akiteseka lakini zaidi alijua maisha ya Ibrahim, alikuwa akimpenda Malaika kiasi kwamba hakutaka kusikia lolote lile kutoka kwa mtu yeyote.
Kila siku ndani ya nyumba kulikuwa na kelele kiasi kwamba baadhi ya wapangaji wakatishia kuhama nyumba hiyo kwani mateso yalizidi, harufu kali iliendelea kuzitesa pua zao kila siku.
Mwenye nyumba hakuwa radhi kuona akipoteza wapangaji kwa ajili ya mpangaji mmoja tu, hivyo alichokifanya ni kumfuata Ibrahim na kuzungumza naye.
Alimwambia hali halisi, jinsi wapangaji wenzake walivyokuwa wakilalamika kimyakimya kwamba mpenzi wake alizidi kutoa harufu kiasi kwamba hata kama utapika pilau, harufu ya pilau haisikiki zaidi ya harufu mbaya ya mwili wa Malaika.
“Mzee! Sina pesa yoyote ile, tutaishi wapi?’ aliuliza Ibrahim huku akimwangalia baba mwenye nyumba.
“Popote pale lakini si hapa. Ibrahim, si kwamba mimi ndiye nawafukuza, ninalazimishwa, ninafanya hivi huku nikiumia sana, hasa hali aliyokuwa nayo mwenzio, hakika inaniumiza sana,” alisema mzee huyo huku akimwangalia Malaika, kwa jinsi alivyokuwa kitandani pale, ilionekana kama angeishi mpaka siku inayofuata basi alitakiwa kumshukuru sana Mungu.
“Mzee! Nipo kwenye wakati mgumu sana. Unaweza kutupa hata mwezi mmoja?” aliuliza Ibrahim.
“Mwezi mmoja? Kwa jinsi hawa watu walivyokuwa na kelele, hata wakijua nimewapa siku mbili, maneno mengi,” alisema mzee huyo.
Aliumia lakini hakuwa na jinsi, alimwangalia mpenzi wake, Ibrahim akashindwa kuvumilia, akaanza kulia kwa sauti, aliumia moyoni mwake, hakuamini kama kweli alikuwa akipitia maisha hayo, mpenzi wake aliteseka, mpenzi wake alikuwa hoi, mpenzi wake alikaribia kufa, mpenzi wake huyo alikuwa na siku chache za kuishi dunia.
Siku iliyofuata, akaamua kuondoka nyumbani hapo, hakujua ni mahali gani alitakiwa kwenda, aliuchukua mkeka tu, mpenzi wake, Malaika hakuweza kutembea, alimbeba mgongoni, alipotoka ndani tu, watu wote waliokuwa nje wakaziba pua zao kwani harufu iliyokuwa ikisikika ilinuka mno.
Nzi wakaanza kumfuata Malaika aliyekuwa mgongoni, kila mtu alikuwa akishangaa, wengine wakahisi kwamba Ibrahim alikuwa amebeba maiti ambayo ilianza kuharibika, wengine wakaelekea msikitini na kuleta jeneza kwani walihisi kwamba ile iliyokuwa imebebwa ilikuwa maiti.
“Tukaizike! Utatembeaje na maiti?” aliuliza jamaa mmoja, alikuwa mtu mwema, hakujua kama mtu aliyebebwa alikuwa mzima kabisa.
“Mpenzi wangu yupo hai. Mungu atamponya!”
“Yupo hai huyu?”
“Ndiyo! Mungu atampa mwili mpya, kama binadamu tunakuwa na spea taili, kwamba kama taili hili likiharibika linawekwa jingine, unafikiri Mungu katuumba bila kutuwekea spea nyingine? Mwili huu ukichoka, Mungu anautoa na kuweka mwingine. Mpenzi wangu atapona tu,” alisema Ibrahim kwa ujasiri na imani kubwa.
Akaondoka na kuelekea Tandale. Njia nzima alipokuwa akipita watu waliziba pua zao, Malaika alikuwa akinuka sana, vidonda viliendelea kumuuma na muda mwingi pale mgongoni alipokuwa amebebwa alikuwa akilia kama mtoto mdogo.
Hawakujua ni mahali gani walitakiwa kwenda kuishi, alichokifanya Ibrahim ni kwenda Tandale katika Mto wa Ng’ombe, pembezoni mwa mto huo na kujenga kibanda fulani kidogo ambacho hakikuonekana kuwa na nguvu, alichomeka miti na kukizungushia magunia, akaingia ndani na kuanza kuishi na Malaika.
Yalikuwa ni maisha yaliyoumiza sana, hakuwa na kiasi kikubwa cha fedha, hichohicho kidogo alichokuwa nacho ndicho ambacho alikitumia kununua chakula na dawa ambazo kila siku ilikuwa ni lazima Malaika apakwe katika vidonda vyake.
“Malaika! Hapa ndiyo kwetu! Tutaishi mpaka hapo Mungu atakapoona imetosha,” alisema Ibrahim huku akimwangalia Malaika aliyeitikia tu. Huku wakiwa wanazungumza ghafla Malaika akaanza kusikia baridi kali.
Akaanza kupiga kelele kwa maumivu makali, alimwambia Ibrahim kwamba alikuwa akisikia maumivu makali ambayo hakuwahi kuyasikia kabla. Ibrahim akamsogelea, akamshika kichwa, joto la mwili wake lilibadilika na kuwa la juu kabisa.
Palepale chini akaanza kurusha miguu na mikono yake huku na kule kama mtu aliyekuwa akikaribia kukata roho. Ibrahim alichanganyikiwa, alimuita Malaika kwa sauti kubwa, hakutaka kuona msichana huyo akifa, hakutaka kuona msichana huyo akimuacha peke yake.
“Usiniache mpenzi! Naomba usiniache! Usife mpenzi! Ninakupenda naomba usife. Mungu naomba usimchukue Malaika wangu, chukua chochote kile lakini niachie Malaika wangu,” alisema Ibrahim huku akijaribu kuzuia kilichotaka kutokea.
Hapohapo, ghafla sana Malaika akatulia, joto la mwili likazidi kupanda, mwili ukanyooka na kutulia tuli.
“Malaikaaaaaaaaa…..” aliita Ibrahim kwa sauti kubwa huku akijaribu kumuamsha mpenzi wake lakini hakuamka, hata macho yake yalifumba.
***
Richard alikuwa njiani akielekea nyumbani kwake, hakuamini kilichokuwa kimetokea, mtoto wake mpendwa alikuwa mapajani mwake. Hakutaka kumpigia simu mke wake na kumwambia kilichokuwa kimetokea, alitaka kumsapraizi kwani aliamini kwamba kile kingekuwa kitu ambacho kingempa furaha maisha yake yote.
Aliendesha gari kwa umakini mkubwa na baada ya dakika kadhaa akafika nyumbani kwake ambapo mlinzi akafungua geti na kuteremka. Akaanza kuelekea ndani, akamkuta mke wake akiwa sebuleni akimnyonyesha mtoto.
Akasimama, akamwangalia huku akitoa tabasamu. Bianca akashtuka, hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea, akamsogelea mume wake ambaye alimuonyeshea mtoto yule. Kitendo cha Bianca kutua macho yake kwa mtoto yule, moyo wake ukapiga paaa kwani alifanana na mtoto aliyekuwa akimnyonyesha.
“Is this my baby?” (huyu ni mtoto wangu?) aliuliza Bianca huku akiwa haamini.
“He is the one,” (ndiye yeye)
“Where did you get him?” (umempata wapi?) aliuliza Bianca huku akimchukua.
Hakuamini macho yake, machozi ya furaha yaliyochanganyikana na uchungu yakaanza kujikusanya machoni mwake na kuanza kulia. Alijisikia hali ya tofauti kabisa, hakuamini kile kilichotokea, alijua kwamba asingeweza kumuona tena mtoto wake, alikata tamaa na kumwachia Mungu kumbe upande wa pili bado Mungu alikuwa akiendelea kufanya kazi yake.
Kila mmoja alikuwa na furaha tele, Bianca akashindwa kuvumilia, akawapigia simu marafiki zake na kuwaambia kwamba alimpata mtoto wake, ni kwamba Mungu alikuwa upande wake na alimpigiania.
Wote walifurahi, furaha ikarudi ndani ya nyuma. Richard hakukumbuka chochote kuhusu Ibrahim, kwake maisha yalikuwa yakiendelea kama kawaida. Siku moja baada ya kukaa ofisini na kuanza kuyakumbuka maisha yake ya nyuma ndipo akakumbuka namna alivyompata mtoto wake.
Moyo wake ukauma, hakuamini kama yeye ndiye aliyefanya ujinga ule, kuondoka chumbani kwa Ibrahim pasipo hata kumshukuru na wakati yeye ndiye aliyemsaidia kumpata mtoto huyo, ndiye alikuwa kijana aliyemuiba mtoto kule nesi alipomficha, kwa maana hiyo alikuwa na uwezo wa kumfanya chochote mtoto yule.
Moyo wake ukamuhukumu, hakuwa amefanya utu, alisikia maumivu mazito moyoni mwake, aliumia kupita kawaida na kujiona akiwa mkosaji mkubwa ndani ya dunia hii.
Hapohapo akachukua simu yake na kumpigia mke wake, alipopokea, akaanza kumwambia jinsi alivyompata mtoto, hakumficha, alimwambia ukweli kwamba alishindwa kumshukuru kijana yule, hivyo akaondoka zake huku akiwa na mtoto.
“Hukumshukuru?” aliuliza Bianca huku akishangaa.
“Mke wangu! Nilizidiwa na furaha, nilitaka kuzungumza, nikashindwa, kiukweli nilifanya kosa kubwa sana,” alisema Richard huku simu ikiwa sikioni mwake.
Bianca akamwambia kwamba ilikuwa ni lazima waelekee huko kwa ajili ya kumshukuru kijana huyo kwani kwa kile alichokuwa amekifanya kilikuwa ni kitu kikubwa ambacho hata kama wangempa milioni mia moja bado kusingelingana na kile alichokuwa amekifanya.
Richard hakutaka kubaki ofisini, akatoka, akachukua gari lake na kumpitia mke wake ambapo moja kwa moja wakaanza safari ya kuelekea huko. Njiani, walizungumza sana, Richard aliendelea kuhuzunika moyoni mwake, hakuamini kama aliweza kufanya jambo kama lile, alitakiwa kuonyesha shukrani, alitakiwa kumuonyeshea kijana yule dalili zote za kumshukuru kwa kile alichokuwa amekifanya.
Hawakuchukua muda mwingi wakafika Magomeni ambapo moja kwa moja wakapaki gari na kuelekea ndani ya nyumba ile. Hakukuwa na mtu ila kwa kuwa Richard alikuwa akikifahamu chumba, akaelekea na kuugonga mlango ule ambapo baada ya sekunde chache, mlango ukafunguliwa na mwanamke mmoja mweupe aliyejichubua kufungua mlango.
“Kuna mtu namuulizia,” alisema Ricard mara baada ya salamu.
“Nani?”
“Anaishi katika chumba hiki,” alisema Richard.
“Humu haishi mwanaume. Nimepanga mimi tu,” alijibu msichana huyo.
Richard alishangaa, alihisi kwamba alikosea chumba, akaangalia vyumba vyote na kuvihesabu, kilikuwa chumba kilekile. Wakati wakiwa wamesimama hapo baba mwenye nyuma akatokea na mwanamke yule kumwambia kile kilichokuwa kimetokea.
“Hebu njooni huku,” alisema baba mwenye nyumba ambapo akawapeleka nje ya nyumba ile na kuanza kuzungumza nao.
Alijua aliokuwa akiwaulizia, aliwaambia kwamba mtu huyo hakuwepo nyumbani hapo, hakuishia hapo, aliwahadithia kila kitu kilichokuwa kimetokea, kwamba Ibrahim alikuwa akiishi na msichana mmoja ndani ya chumba kile, msichana mgonjwa aliyekuwa hoi, mwili kuharibika na kutoa harufu chafu.
Ilikuwa simulizi ya kusisimua ambapo Richard na mkewe wakabaki wakitokwa na machozi, hawakuamini kile walichokuwa wakikisikia kwamba mtu aliyekuwa akiwasaidia alikuwa na mpenzi aliyekuwa kwenye hali mbaya, na mbaya zaidi hakuwa na pesa, aliteseka, maisha yaliwapiga mno.
Moyo wa Richard ukazidi kuumia zaidi, alijiona kufanya kosa kubwa, alikuwa na uwezo mkubwa wa kumsaidia msichana huyo na hata kama alibakiza miezi mitatu ya kuishi, aliona kabisa kwamba angejitahidi sana kumuhudumia kama shukrani yake kwa Ibrahim mpaka siku ambayo angefariki dunia.
“Baada ya kuhama walihamia wapi?’ aliuliza Richard huku machozi yakitiririka mashavuni mwake.
“Waliondoka! Taarifa za chini nilisikia wakiishi Tandale, kando ya Mto wa Ng’ombe, Ibrahim alijenga kibanda hapo lakini….” Alisema baba mwenye nyumba na kunyamaza.
“Lakini nini?”
“Yule mpenzi wake alifariki dunia katika maumivu makali sana,” alisema baba mwenye nyumba, yeye mwenyewe akashindwa kuvumilia, machozi yakaanza kumlenga.
“Alifariki dunia?”
“Ndiyo! Ilikuwa juzi ndiyo nilipata taarifa hiyo na watu kwenda kumzika katika makaburi ya Kwa Ally Maua,” alisema baba mwenye nyumba. Bianca akashindwa kuvumilia, akaelekea ndani ya gari na kuanza kulia kama mtoto kana kwamba msichana aliyekufa alikuwa mdogo wake wa damu.
Je, nini kitaendelea?
Tukutane kesho hapahapa.