The House of Favourite Newspapers

Mpoto, Watu Wakisema ni Kiki Wanakosea?

0

NA OJUKU ABRAHAM | GAZETI LA IJUMAA | ZA CHEMBE LAZIMA UKAE

JUMATATU iliyopita, Mzee Francis Kanyasu maarufu kama Ngosha, anayetajwa kama ndiye aliyechora Nembo ya Taifa, alifariki dunia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa amelazwa akitokea Amana. Umekuwa ni kama msiba wa taifa hasa kwa jinsi ambavyo nembo hiyo imekuwa kama utambulisho wetu kama nchi, maana unapatikana kila eneo.

Msanii Mrisho Mpoto.

Ni mtu muhimu kiasi kwamba baada ya kuwa amesahauliwa kwa miaka mingi, Serikali ilimchukua na kumtibu baada ya kuibuliwa na ITV wiki kadhaa zilizopita. Wakati ninaandika makala haya, taarifa juu ya mazishi yake zilikuwa bado hazijatolewa, lakini ni wazi kuwa msiba huu utasimamiwa kwa karibu na Serikali, kama ambavyo Naibu Waziri wa Afya, Hamisi Kigwangalla alivyosema wakati akitibiwa kuwa itamuangalia kwa karibu.

Lakini wakati nikiendelea kujiuliza, nimekutana na taarifa ya masikitiko ya msanii wa Muziki wa Asili, Mrisho Mpoto katika mojawapo ya mitandao ya kijamii, ikielezea jinsi gani alipatwa na mshtuko baada ya kubaini kuwa alikuwa ndiye yule aliyemtumia katika video ya wimbo wake uitwao Njoo Uichukue, alioufanya kabla hajatoa ule wa Sizonje ambao ndiyo umebamba zaidi.

Amemkumbuka baada ya kumtazama kwa makini alipopata taarifa za kufariki kwake. Kwamba alifika ofisini kwao akionekana kama chizi, lakini baada ya kukataa kumbeza na kumsikiliza, hatimaye aliwashauri namna ya kutengeneza video ya wimbo huo, akiomba sehemu moja ‘aekti’ yeye, ile
maana ya kikongwe muuza bangi.

Marehemu alimwambia Mpoto kuwa anapenda kazi zake na akamtabiria mambo mazuri katika muziki wake, lakini zaidi akimuacha na kumbukumbu ya maneno kuwa ‘ayachukulie maneno hayo ni ya chizi kaongea’! Katika kumalizia masikitiko yake hayo, Mpoto ambaye anasema mzee huyo aliwatoroka wasijue kwa kumpata baada ya ku-shut kipande chake hicho, amewataka wanafamilia kumjulisha kuhusu mazishi yake! Dah, kwa hili Mpoto ameniangusha.

 

Ninamfahamu kitambo kidogo msanii huyu na niseme wazi kuwa ninazimia aina yake ya usanii. Ameamua kujitofautisha ili pengine kukimbia ushindani katika muziki wa aina nyingine. Ubunifu huo peke yake ni mafanikio. Mpoto ni mzuri kichwani kuliko wasanii wengi tunaoweza kumweka nao mezani.

Anafahamu mambo mengi, ya siasa, utamaduni, jamii na hata michezo, tofauti na wengine ambao ukiwatoa katika sanaa wanayoifanya, hawana umahiri katika maeneo mengine, hata kama yanatawala jamii inayowazunguka. Kuna maswali mengi kama utafuatilia alichokisema Mpoto kuhusu mzee huyo mchoraji wa nembo ya taifa.

 

Ni kweli aliwakimbia mara tu baada ya shooting? Neno kuwatoroka,maana yake aliondoka pasipo kukamilisha project na hakuaga, kwa nini? Na hivi inawezekanaje Mpoto asimtambue mzee huyu tangu alipoibuliwa na ITV, akawa gumzo katika vyombo mbalimbali vya habari, akitembelewa na Mheshimiwa Rais Magufuli hospitalini kwa kipindi cha zaidi ya wiki kadhaa? Leo amefariki ndiyo anamgundua! Kama nilivyosema pale mwanzo, ninamfahamu huyu msanii na sijawahi kumuona akizitafuta kiki kwa staili ya namna hii, kitu gani kimemkumba? Yaani siku zote hakumkumbuka mzee Ngosha hadi amefariki?

Kwa mtu wa kufikiri, anaweza kuamini kulikuwa na tatizo la kimsingi kati yake na marehemu ndiyo maana hakutaka jamii ijue kama aliwahi kufanya naye kazi.

Pengine angemkumbuka akiwa hai, kuna kitu angesema. Nimshauri tu Mpoto kuwa makini wakati mwingine na kauli anazozitoa, hata kama kwa ujumla wake hazina chembe ya shaka maana kuwapa watu maswali ya kujiuliza ni dalili ya kutoaminika kwa ulichokisema, vinginevyo atuambie kuwa kwa muda wote, hakuwahi kumuona Mzee Ngosha iwe gazetini, runinga wala mitandao ya kijamii!

KWA USHAURI: +255 719 786 355

VIDEO: TAZAMA MAAJABU YA MRISHO MPOTO

Leave A Reply