Mr. Ebbo Asisitiza Udumishaji Mila!

Mr. Ebbo enzi za uhai wake.

NGO’MBE wamejaa kila mahali. Mbolea yao imetapakaa sehemu yote na milio inasikika kila eneo.

Wingi wa mapembe yao unapendezesha sana na kwenye migongo yao. Kucheua kwa wanyama hao kunanifanya nimrudishie Mungu utukufu wake.

 

Ghafla nasikia mluzi kwa nguvu, nashtuka na kutazama nyuma, hapohapo napigwa na butwaa kutokana na mtu aliyesimama wima na kuweka fimbo mabegani, miguuni akiwa peku tena amejitanda lile vazi la Kimasai, kichwani akiwa amesuka kwa kulaza nywele kurudi nyuma. Yes, ni Abel Loshilaa Motika ‘Mr. Ebbo’.

 

Mr. Ebbo: Hey, wewe nani na unafanya nini huku weye?

Mimi: (huku nikitetemeka) naitwa Masalu, mwandishi wa habari Global Publishers, mzima wewe?

Mr. Ebbo: Oooh, salama kabisa bwana. Huko ulikotoka mambo yanakwendaje?

Mimi: Safi tu, hivi ile staili ya uimbaji wako kwa kutumia lafudhi ya Kimasai ni mtindo tu au uko hivyo kabisa?

 

Mr. Ebbo: Mimi ni Mmasai kweli na ndiyo maana niliamua kuja kwenye muziki kupitia mila, tamaduni na desturi za kikwetu ikiwa ni kufikisha ujumbe kwa jamii na wakati huohuo kudumisha mila kama nilivyosema hapo awali.

Mr. Ebbo enzi za uhai wake.

Mimi: Wakati unaanza kuimba mwanzoni mwa miaka ya 2000, hukufikiria kwamba unaweza kupata ugumu wa kupokelewa na mashabiki, kwamba watakuwa hawawezi kuelewa matamshi ya lafudhi ya Kimasai kupitia Kiswahili?

 

Mr. Ebbo (huku akicheka kwa kukenua meno tu), hapana unajua ni ubunifu wa sanaa na ndiyo maana mtu kama John Walker alikuja na staili ya ulevi. Lakini watu walimuelewa kutokana na ujumbe aliokuwa anauwakilisha kwa jamii ingawa ilikuwa kama mlevi anazungumza, lakini pia sababu nyingine iliyonifanya nitoke Kimasai ni kwamba kabila langu lilikuwa nyuma kwa vitu vingi sana, nikaona nije na staili hiyo ikiwa ni njia ya kukuza zaidi kabila langu.

 

Mimi: Vizuri sana Mr. Ebbo. Jina hilo ulilipataje ilhali wewe ni Abel?

Mr. Ebbo: Umenikumbusha rafiki yangu mmoja sijakuuliza kama yupo. Oscar Ndauka, huyo ndiye alinipa jina la Mr. Ebbo. Nakumbuka nilikuwa nimekaa naye mahali fulani tunajadili mambo ya sanaa na kuniambia kwa nini nisitumie Mr. Ebbo kwa sababu jina langu hutamkwa hivyo kwa Kiingereza, basi kuanzia hapo nikawa Mr. Ebbo, msalimie sana ukirudi huko najua leo umekuja mara moja tu, wanaokuja huku jumlajumla tunawajua sana.

 

Mimi: Ok, ile studio yako ya Motika Records pale Tanga uliiacha kwenye mikono ya nani maana siku hizi sisikii wimbo wowote uliopikwa studioni hapo.

Mr. Ebbo: Unajua kama ilivyo kawaida, safari ya kuja huku siku zote huwa ni fumbo ambalo huwezi kujua unajikuta tu umeshafika huku na unapewa makazi yako, siku naondoka huko sikuwa na wazo kwamba itakuwa hivyo kwa hiyo kila kitu kilikuwa mkononi mwangu, ilikuwa ni vigumu sana waliobaki kuendeleza baada ya hapo kwa sababu pia lengo kubwa la studio hiyo ilikuwa ni kukuza mila za makabila mbalimbali nchini kupitia muziki, yote ni mipango ya mwenye kushika pumzi yetu, Mungu wa Mbinguni.

 

Mimi: (nikishusha pumzi ndefu) ni jambo gani lilikuwa linakukera sana wakati ukiwa kwenye ulimwengu wetu?

Mr. Ebbo: (akikaa na kunipa ishara ya mimi kufanya hivyo), swali zuri sana na unaonekana wewe ni mwandishi mzuri. Kwa kweli nilikuwa nachukizwa sana na watu kusahau na kutupa kabisa mila na desturi zao.

 

Mtu anajifanya wa mjini na kusahau kwao, wengine anafika mahali anaamua kabisa kubadili hata jina kwa sababu jina lake halisi analiona kama baya halijakaa kiswaga za mjini, kosa kubwa sana kufanya hivyo. Watu wadumishe mila, hayo maisha ya uzungu ni ya kazi gani? Mbona wao (wazungu) wakiwa Afrika hufurahia maisha yetu? Watu wabaki kwenye asili zao. Tena siyo kubaki tu na wajivunie na kuona fahari kuzaliwa kwenye makabila yao.

 

Mimi: Umeshaonana na John Walker?

Mr. Ebbo: Ndiyo lakini mara moja tu, unajua natumia muda wangu mwingi sana kukaa na mifugo yangu hii, kuna siku alikuwa anapita nikamuona kwa mbali na kumuita kama kubahatisha lakini kumbe alikuwa ni yeye.

 

Mimi: Muziki vipi kwa huku? Unapiga mzigo kama kawaida?

Mr. Ebbo: Siyo sana. Nakumbuka mara ya mwisho nilialikwa kwenda kuimba kwenye mapokezi ya Captain John Komba, tangu siku hiyo sikuimba tena.

Mimi: Nakumbuka vibao vyako kama Mimi Mmasai, Bado, Kamongo na vingine vingi ambavyo vilikuwa vinanikuna kwa kweli…

 

Mr. Ebbo: Ni ubunifu na kuumiza kichwa lakini lengo ni kwamba ujumbe umefika na umefanyiwa kazi.

Mimi: Mr. Ebbo nikushukuru sana. Basi naomba unioneshe mahali pa kutokea huku maana sielewi chochote.

 

Mr. Ebbo: Ngoja kwanza nikaswage ng’ombe wangu naona wanaanza kufika mbali, nisubiri hapo nakuja, nataka ufikishe salamu zangu kwa wasanii niliowaacha akina Mr. Blue, Lady Jay Dee, Dudubaya, Mr. Nice na akina Q-Chillah, TID, Jay Moe na wengine niliowasahau.

 

Mimi: Wahi uje unioneshe bwana nataka nitoke huku na pia hongera sana leo (Ijumaa iliyopita, Desemba 1) umetimiza miaka sita tangu uondoke kwenye ulimwengu wetu.

Wakati namsubiri Mr. Ebbo, nashangaa nainua kichwa na kukutana na mazingira ya chumba changu na hapohapo nasonya na kulaumu kazi ya ndoto.

 

Ndoto hizi bwana, kwa nini naota nazungumza na watu maarufu ambao hatunao tena? Dah! Sijui lakini.

Kwa maoni na ushauri nicheki kwa namba hizi; 0673 42 38 45.

BRIGHTON MASALU | GAZETI LA AMANI | Saa Tisa Usiku Kitandani Kwangu.

 

GLOBAL HABARI: MADABIDA KIZIMBANI KWA KUSAMBAZA ARVS FEKI

Toa comment