MR NICE AFANYIWA KITU MBAYA GESTI
DAR ES SALAAM: Mfalme wa Takeu, Lucas Mkenda maarufu kama Mr. Nice juzi Jumatatu alifanyiwa kitu mbaya maeneo ya uswahilini, Manzese Uwanja wa Fisi jijini Dar baada ya kuwa amelewa, Risasi Mchanganyiko lina mkanda kamili.
MWANZO WA MCHEZO HUU HAPA
Baadhi ya mashabiki wa Muziki wa Dansi waliliambia Risasi Mchanganyiko kuwa walimuona Mr. Nice usiku akiwa katika ukumbi mmoja wa starehe uliopo Kinondoni, ambako Bendi ya Muziki ya Mapacha Watatu ilikuwa ikitumbuiza.
Mmoja wa wakurugenzi wa bendi hiyo, ambaye pia ni mwimbaji nyota, Jose Mara inasemekana alimuita juu ya jukwaa Mr Nice na kumtaka kuwasalimia mashabiki wake ambao wamem-miss kwa muda mrefu.
APANDA JUKWAANI, MMMH!
Chanzo chetu kilichokuwa ndani ya ukumbi huo, kinasema mkali huyo wa muziki, aliitika wito na kupanda jukwaani, lakini katika kuwasalimia mashabiki, inadaiwa kidogo ilikuwa ni shida kwa kuwa alikuwa ameburudika vya kutosha.
AONDOKA USIKU MNENE NA ‘MZIGO’
Chanzo chetu kinaeleza kuwa baada ya kuburudika vya kutosha katika ukumbi huo, usiku mnene, Mr Nice ambaye inadaiwa hali yake ya kifedha imeanza kurejea kuwa nzuri, aliondoka akiwa ameambatana na msichana ambaye jina lake halikufahamika mara moja.
Safari yake na mwanamke huyo, iliwafikisha katika nyumba moja ya kulala wageni iliyopo Uwanja wa Fisi, Manzese ambako walichukua chumba na kuingia ndani.
SAA TANO ASUBUHI
Shuhuda wetu aliyekuwa miongoni mwa watu waliokuwepo eneo la baa hiyo, anadai ilipofika saa tano asubuhi, Mr Nice aliamka, lakini mwanamke aliyekuwa naye hakuwepo.
Hali hiyo ilimpa wasiwasi msanii huyo, aliyeanza kujisachi na kugundua kuwa kiasi cha shilingi 230,000 hakikuwepo mfukoni mwake, ikiwa ni pamoja na simu yake aina ya Apple na mazagazaga mengine kadhaa.
AANGUA KILIO, AJAZA WATU
Bila kujali ustaa wake, inadaiwa Mr Nice aliangua kilio kikubwa kilichosababisha watu kujaa ili wajue kulikoni.
Msanii huyo mwenye rekodi ya kuwahi kushika pesa nyingi kupitia muziki, aliwaeleza watu kilichomsibu hivyo kuwaomba vijana wanaomfahamu msichana aliyekuwa naye, wamtafute kwa udi na uvumba na kuwaahidi kama wangempata, angewapa kitu kidogo.
DEMU ASAKWA, AIBULIWA
Vijana wa maeneo hayo ambao wanamfahamu msichana huyo, walimtaja kuwa ni Happy baada ya kupewa tenda hiyo, walianza kumsaka kwa bidii na kufanikiwa kumnasa muda mchache baadaye ambako walimpeleka kwa mkali huyo wa muziki aliyetamba sana enzi zake.
MR NICE ALIANZISHA, POLISI WAITWA
Baada ya msichana huyo kuletwa mbele ya Mr Nice akiwa na simu aliyoondoka nayo, msanii huyo alianzisha vurugu kubwa kwa dada huyo, kiasi cha kuwapa hofu baadhi ya watu, ambao waliwapigia simu polisi waliowasili muda mchache baadaye na kuweza kutuliza hali ya hewa.
Wanausalama hao walipofika eneo hilo walimtaiti Mr Nice ambaye wakati huo alionekana kuwa bado amechangamka.
Kuona hivyo, polisi walimchukua na msichana huyo pamoja na watu wengine kadhaa waliokutwa wakiwa wanapata ‘kiburudisho’ ndani ya gesti hiyo na kwenda nao Kituo Kidogo cha Polisi Tandale ambako walifunguliwa jalada la kunywa pombe wakati wa muda wa kazi.
ANG’ANG’ANIWA, DEMU AACHIWA
Mwanamuziki huyo akiwa kituoni hapo, alianza kulia kwa sauti na kuwaomba askari wamsamehe, huku akisisitiza kuwa yeye ameshamsamehe msichana aliyemuibia fedha zake kwa kuwa shida yake kubwa ilikuwa ni kupata simu yake.
Licha kusema amemsamehe mwanamke huyo, lakini walimng’ang’ania kwa kosa la kunywa pombe asubuhi. Happy aliachiwa na polisi baada ya kujitetea kuwa aliichukua simu hiyo kwa kuwa ni ya mpenzi wake na hakuwa na nia ya kuiiba isipokuwa alitoka kidogo kwenda kununua dawa, kitu kilichomfanya mpenzi wake huyo aamini aliachwa kwenye mataa.
AHAMISHIWA MAGOMENI
Risasi Mchanganyiko ambalo lilifika kituoni hapo na kumshuhudia msanii huyo akiwa ndani ya kituo, lilimuona akiondolewa kituoni hapo huku baadhi ya askari wakidokeza kuwa alipelekwa Kituo cha Polisi Magomeni.
Mr Nice ni msanii aliyetamba vilivyo katika miaka ya mwanzoni mwa 2000, akiimba vibao kama Kikulacho, Rafiki, Kidali Poo, Fagilia, King’asti na nyingine kadhaa.
RICHARD BUKOS, RISASI MCHANGANYIKO