Mradi wa Phoenix Condos Watarajiwa Kubadilisha Taswira ya Nyumba za Jiji la Dar
Dar es Salaam, Ijumaa Julai 19, 2024: Mradi mpya wa nyumba unaoendeshwa na kampuni ya Phoenix Condos na ambao umezinduliwa hivi karibuni unatarajiwa kubadilisha muonekano wa nyumba Jijini Dar es Salaam, huku milango ya uwekezaji ikifunguliwa rasmi
Akizindua mradi huo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Majengo katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk.Upendo Matotola aliipongeza kampuni ya TT Investments kwa kuanzisha mradi huo, ambapo pia aliipongeza kampuni ya REMAX Coastal Reality ambayo inashughulikia masoko na maendeleo ya mradi huo wa nyumba.
“Ahadi yetu ni kuhakikisha uwekezaji wa aina hii hauyumbi; tunajivunia kuwa na uwekezaji wa aina hii ambao unakuza na kustawisha mazingira ya uwekezaji kwa mali zisizohamishika”, alisema na kuongeza, serikali kupitia sekta ya ardhi itaendelea kudhibiti, kuratibu na kukuza sekta ya mali zisizohamishika.
Alibainisha zaidi kuwa uwekezaji uliofanywa na kampuni ya Phoenix Condos ni zaidi ya nyumba za kifahari na kwamba pia unaakisi kiwango kipya cha ubora majengo katika jijini la Dar es Salaam. “Muundo wa mradi, eneo na vistawishi vyote vinachangia hali bora ya maisha, inayoakisi viwango vya juu tunavyokuza katika tasnia”, alisema.
Kulingana na Mkurugenzi huyo, ushiriki wa chapa ya REMAX katika mradi huo umesaidia sana katika kuwahakikishia wawekezaji na wateja uwazi na uadilifu katika miradi inayohusiana mali zisizohamishika.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uwekezaji wa TTiNvestments, Bw. Yong Jun Liu alisema kinachoifanya Phoenix Condos kuwa kinara katika uwekezaji si ubunifu tu, bali ni ahadi ya maisha bora kwa wateja wao. “Wakati bei za bidhaa zake zikizuingatia ubora wa bidhaa zake, Phoenix Condos pia inahakikisha ubora wa bidhaa ambazo hutokana na matumizi ya vifaa vya kisasa vyenye viwango vya hali ya juu”, alibainisha.
Bw.Liu aliendelea kusema kuwa kampuni ya Phoenix Condos, pia inayo miradi mingine ya kimaendeleo ambayo ni pamoja na Mnara wa Mwenge, Mnara wa Tanzanite uliopo kando ya barabara ya Sam Nujoma njia ya kuelekea Mlimani City, jengo la Ofisi ya Tanzanite Park lililopo eneo la Victoria, majengo ya makazi ya ghorofa ya Tanzanite, majengo ya makazi 102 ya Phoenix City yaliyoko eneo la Oyster Bay na pamoja na miradi mingine mingi ambayo inatarajiwa kuekelezwa wakati ujao.
Nae Bi Happiness Watimanywa kutoka kampuni ya REMAX Coastal Reality, alisema wanajivunia kuwa sehemu ya mafanikio ya kampuni hya Phoenix Condos na kwamba wana imani kuwa maendeleo haya yatachangia kubadilisha viwango vya maisha kwa ngazi ya makazi na majengo kwa ujumla Jijini Dar es Salaam.
“Maendeleo kama yale yanayofanywa na kampuni ya Phoenix Condos hayahusu ujenzi wa nyumba nzuri za kuishi tu bali pia yanachangia kukuza sekya ya ujenzi na ukuaji wa uchumi wa Taifa kwa ujumla”, alisema.
Tukio hilo la kupendeza la uzinduzi, ambalo lilihudhuriwa na viongozi na wadau mbalimbali wa sekta za nyumba na seka ya majengo kwa ujumla, liliashirikia na kuweka msisistizo dhamira kuu inayolenga kuboresha tasnia ya ujenzi wa nyumba bora sambamba na kuleta mabadiliko katika sekta inayohusiana na mali zisizohamishika kwa ujumla.