The House of Favourite Newspapers

Mrema Ataka Wafungwa Waliolipiwa Faini Waachiliwe

1Mwenyekiti wa Bodi ya Parole Taifa Dk. Augustine Lyatonga Mrema akisoma taarifa yake.2 …Akionyesha nakala za malipo ya benki.3
 Nakala za risiti za malipo ya benki ya kuwatoa wafungwa.

MWENYEKITI wa Bodi ya Parole Taifa, Dk. Augustine Lyatonga Mrema, amemwangukia Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa, akimtaka kuingilia kati suala la mpango wake wa kuwatoa wafungwa 43 aliowalipia Sh. 12,840,000 walizokuwa wakidaiwa kupitia mfadhili wake Mchungaji Getrude Lwakatare wa Kanisa la Assemblies Of God ’Mlima wa Moto’.

Ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na wanahabari kwamba ameamua kumwandikia barua Majaliwa ili waliokwamisha zoezi hilo wachukuliwe hatua.

Mrema amesisitiza kwamba azima ya kuwatoa wafungwa magerezani ilikuja baada ya Majaliwa kutembelea Gereza Kuu la Isanga na kukuta msongamano mkubwa wa wafungwa, na katika magereza sita aliyotembelea idadi ilizidi kwa asilimia 16 ambapo palitakiwa kuwa wafungwa 1,552 lakini wakawepo 1,795.

Amefafanua kuwa kutokana na hali hiyo Majaliwa baada ya kusomewa hotuba na mkuu wa magereza Mkoa wa Dodoma aliamua kumwagiza Mrema kufuatilia ili aweze kutatua tatizo la msongamano ndani ya magereza hayo.
“Nilianza kutekeleza maagizo ya waziri mkuu lakini kwa kuwa bodi ya parole haina fedha za kutosha kutokana na ufinyu wa bajeti, ilinibidi kutafuta wafadhili na wahisani ili nikamilishe mchakato huo.

“Miongoni mwa wafadhili waliojitokeza ni Mchungaji Dk. Getrude Lwakatare wa Kanisa la Assemblies Of God ’Mlima wa Moto’ ambaye alikubali kutoa Shilingi 12,840,000 ili kuwalipia faini wafungwa 43 wenye makosa madogo waweze kutoka magerezani na fedha hizo zilitokana na michango ya waumini wa kanisa lake.”

Alieleza kuwa baada ya mchakato wote kukamilika Oktoba 21 mwaka huu fedha za kuwatoa wafungwa hao zililipwa katika benki lakini akasikitishwa kwamba licha ya wafungwa hao kulipiwa hadi sasa hawajatolewa.

“Ninaamini kwamba kitendo hicho cha kutowatoa wafungwa hao wenye makosa madogo waliofungwa kwa kukosa kulipa faini wanazodaiwa ni kinyume cha utawala wa sheria na pia ni ukiukwaji wa amri za mahakama ambazo zilieleza wazi kwamba endapo washitakiwa watalipa au kulipiwa faini waachiwe huru,” alisema Mrema.

Aidha aliongeza kuwa mbali ya kutopewa sababu zozote kwa maandishi zinazokwamisha wafungwa waliolipiwa faini wasiachiwe, anasikia tetesi kupitia vyombo vya habari kwamba zoezi hilo limesitishwa na Jeshi la Magereza.

Na Denis Mtima/Gpl

1 2 3 4

halotel-strip-1

Comments are closed.