The House of Favourite Newspapers

MREMBO ACHUNGULIA KIFO LIVE!

 

KAMA siku yako ya kifo haijafika, haijafika tu, utadhurika na kuteseka ila hufi! Ndivyo walivyokuwa wakisema baadhi ya mashuhuda wa tukio la mrembo Joyce Mwane ambaye amejikuta akiangua kilio hadharani baada ya kuchungulia kifo ‘live’ kwa macho yake, Risasi Mchanganyiko linakujuza.

HAWEZI KUSAHAU

Ni baada ya gari kubwa aina ya lori kumshinda dereva na kuhama barabara kisha kuzama ndani ya duka la dawa alilokuwa akiuza na kumwacha na wenge ambalo hatakaa hasahau maishani mwake.

Tukio hilo lililojaza umati mkubwa na kufunga mtaa kutokana na taharuki ya hofu ya vifo lilijiri Jumatatu iliyopita, majira ya asubuhi maeneo ya Mazimbu mjini hapa.

 

MASHUHUDA SASA

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo waliozungumza na gazeti hili muda mfupi baada ya balaa hilo, Regina Makusi na Recho Temu, kila mmoja alisimulia alichokiona;

“Yaani Mungu ni mkubwa sana. Mimi na mwenzangu, mama Mery tulikuwa tunavuka barabara, tunakuja dukani kwangu. Mimi duka langu ni hili hapa la vyakula (akionesha duka lake). Ile tunamaliza tu kuvuka barabara ndipo tukashuhudia hili lori likitokea upande wa mjini linashuka kwa kasi ya ajabu kwenye hiki kimteremko cha lpo-lpo huku linayumba.

“Ghafla nilishtuka kuona likimkumba mama Mery na kumjeruhi ambaye kwa sasa amekimbizwa hospitalini kisha lori hilo lililokuwa linaendeshwa na Mwarabu, likatumbukia kwenye duka hili la dawa,” alisema Recho, mmiliki wa duka Mazimbu.

 

Kwa upande wake Regina Makusi alisimulia alichokishuhudia:

“Nilikuwa huku ng’ambo, nilishuhudia ‘live’ lori hilo lililokuwa kwenye mwendokasi likiyumbayumba kama mlevi na kumshinda dereva baada ya kufeli breki.

“Salama pekee ya dereva huyo ilikuwa ni kuamua kulielekeza kwenye haya maduka na kutumbukia katika duka hili la dawa.

“Ni jambo la kumshukuru Mungu kwani ndani ya duka hili la dawa hakuna aliyekufa ingawa baadhi ya watu wamejeruhiwa akiwemo Mwarabu mwenyewe ambaye baada ya kuchomolewa alivishwa pingu na polisi kisha kukimbizwa hospitalini.”

Kwa upande wake, Joyce aliyekuwa ndani ya duka hilo la dawa akiuza alisimulia alivyokiona kifo kwa macho yake ambapo alikuwa na haya ya kusimulia huku akiangua kilio mbele ya gazeti hili;

“Kwangu naona kama muujiza kupona kwenye tukio hili pamoja na kwamba nimepata majeraha kama unavyoniona, lakini kikubwa ni uhai.

 

“Kipekee ninamshukuru sana Mungu kwa kuninusuru na tukio hili. Sina maelezo zaidi ya tukio hili kwani nilikuwa ndani ya duka na ghafla nilipogeuka, nilishangaa kuona lori kubwa likinivamia dukani.

“Ni kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu tu nimefanikiwa kutoka kwa kulikwepa na kukimbia nikiwa sijielewi wala siamini kilichotokea. Lazima nikamtolee Mungu sadaka ya shukurani.”

Mara baada ya kutokea kwa tukio hilo, Askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani na wenzao wa Kikosi cha Zima Moto na Uokoaji wakisaidiana na na wafanyakazi wa Shirika la Umeme (Tanesco), walifanya kazi ya ziada kuokoa watu waliokuwa kwenye maduka hayo kama wauzaji na wanunuaji.

MAGARI MAWILI YAGONGWA

Katika hatua nyingine, wakati lori hilo likivutwa na lori la Manispaa ya Morogoro ili kuchomolewa ndani ya duka hilo, lilipofika njiapanda ya Ipo-Ipo liliyumba na kuyagonga magari mawili aina ya Toyoya Noah na lsuzu ‘kirikuu’ na kuibua taharuki nyingine.

Kufuatia tukio hilo, Askari wa Usalama Barabarani, waliamua lori hilo kutoendelea kulivuta na badala yake walikwenda kuliweka eneo la Modeko-Reli ya Kwanza kusubiri utaratibu mwingine wa kulipeleka kituo cha polisi huku Mwarabu huyo aliyetaka kumuua Joyce akiishia kwenye mikono ya polisi.

KAMANDA MATEI

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Ulrich Matei alithibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo watu watatu walijeruhiwa, lakini hakukuwa na mtu aliyepoteza maisha.

 

 

STORI: Dustan Shekidele, Risasi Mchanganyiko

Comments are closed.