MREMBO ADAIWA KUMUUA MCHUMBA WAKE!

MREMBO ambaye ukimuona unaweza kusita kuamini anachodaiwa kukifanya, yuko mikononi mwa polisi akituhumiwa kumuua mchumba wake aitwaye Erick Msodiki mkazi wa Malandizi mkoani Pwani.

 

Kisa cha mauaji kimetokea hivi karibuni ambapo mashuhuda wa tukio wanasema hakuna aliyetarajia kuwa Msodoki angepoteza maisha katika ugomvi uliohusisha wivu wa kimapenzi baina yake na mchumba wake aliyetajwa kwa jina moja la Maya.

 

“Mchana tulikuwa naye freshi tu, alipita nyumbani akaniambia anaenda kwa mama yake mkubwa na kwamba tungeonana jioni. “Usiku nimekaa zangu maskani na washikaji nikapigiwa simu kuwa Erick amefariki, sikuamini lakini ukweli ndiyo uko hivyo,” alisema kijana mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Peter ambaye anatajwa kuwa rafiki wa marahemu.

 

HABARI KUTOKA ENEO LA TUKIO

Inadaiwa na mama mkubwa wa marehemu Erick kuwa kijana huyo amekuwa na mahusiano ya kimapenzi na Maya kwa muda mrefu na kwamba walikuwa wakiishi kama mume na mke.

 

“Huyu ni mwanangu, mtoto wa ndugu yangu, amepanga chumba pembeni kidogo na hapa ninapoishi. “Lakini kazi alikuwa anafanya hapa dukani kwangu, siku ya tukio alikuja nikamtuma kunifanyia manunuzi ya bidhaa za dukani akafanya hivyo, baadaye akasema anakwenda nyumbani kwake.

 

“Tuliagana akaondoka, baadaye nikapigiwa simu na rafiki yake akinijulisha kuwa Erick ni mgonjwa amepelekwa hospitalini. “Nikashtuka sana, mtu tulikuwa naye hadi jioni kaugua nini cha kukimbizwa hospitalini, nikasema ndiyo ubinadamu ikabidi niende hospitalini nilipoelekezwa,” anasimulia mama huyo aliyejitambulika kwa jina mama Erick.

 

Aliongeza kuwa baada ya kufika hospitalini alipokelewa na daktari wa zamu alipouliza habari za mgonjwa akaambiwa atulie kwanza.

“Nikaona daktari ananipeleka kwenye chumba kingine, nilipofika huko nikamuuliza mbona mgonjwa wangu simuoni akasema nikae tu kwanza atanionesha. “Baadaye akaja mjomba wake hapo sasa ndiyo tukaambiwa kuwa Erick alikuwa amefariki kutokana na ugomvi kati yake na Maya ambaye ni mchumba wake,” alidai mama huyo.

 

ERICK ALIKUFAJE?

Chanzo cha habari kutoka eneo la tukio kinadai kuwa mara baada ya marehemu Erick kurejea kutoka kazini alimkuta mchumba wake na kwamba walianza mzozo uliojaa tuhuma za kusalitiana. “Maya alichukua simu ya marehemu akawa anaipekua, sijui aliona nini ndiyo akaanza kumuuliza mwenzake huyu nani.

 

“Baadaye ukatokea ugomvi mkubwa lakini kwa kuwa sisi kama majirani tulishawazoea kutokana na tabia yao ya kupiganapigana tukapuuzia. “Zilipita dakika nyingi; kukawa na ukimya tukajua wamemalizana kumbe haikuwa hivyo, tatizo lilikuwa limetokea,” alisema jirani wa marehemu ambaye hakupenda kutaja jina lake.

 

Aliongeza kuwa mara walimuona msichana huyo kama amepagawa akijaribu kupiga simu huku na kule ndipo walipokusanyika majirani kumuuliza kulikoni? Wengi kati ya majirani waliofika macho yaliwaambia tatizo lililokuwa mbele yao lakini kisa cha Erick kuvuta pumzi kama mtu anayekata roho kilikuwa hakijajulikana.

 

Katika hali ya kudodosa ndipo msichana huyo aliwaambia majirani kwamba mchumba wake aliteleza na kuanguka wakati wakigombania simu ya marehemu ambayo Maya anadai kuona meseji za mapenzi za msichana mwingine. “Alituambia alikuta meseji kuna msichana walikuwa wanachati na marehemu mambo ya mapenzi, alipomuuliza akawa mkali ndipo ugomvi ukaanza. “Alisema wakati wagombana ndiyo akamuona mwenzake kadondoka na kuanza kutapatapa,” chanzo kilidai.

MAREHEMU AKIMBIZWA HOSPITALI

Mara baada ya majirani kukusanyika walikodi pikipiki kwa lengo la kumuwahisha marehemu hospitali kujaribu kuokoa maisha yake lakini mwendesha pikipiki alipofika hakuweza kumchukua mgonjwa kwa madai kuwa asingeweza kukaa vizuri kutokana na hali mbaya aliyokuwa nayo.

 

Aidha marafiki walipojadiliana walikubaliana kukodi taksi ili imsaidie mgonjwa kufika kwenye tiba. Inadaiwa mara baada ya kufika hospitalini, vipimo vya daktari vilionesha kuwa Erick alikuwa amekata roho, jambo ambalo liliwalazimu rafiki wa marehemu kumuweka chini ya ulinzi Maya ambaye wakati huo alikuwepo hospitalini hapo akiomba dua mabaya yasimtokee mchumba wake jambo ambalo halikuwezeka.

 

Simanzi vilio na machozi vilitawala hospitalini Mlandizi ambapo baadaye polisi walifika na kumchukua mtuhumiwa pamoja na mwili wa marehemu kwa ajili ya uchunguzi.

 

KAMANDA ATAFUTWA

Kutokana na chanzo cha kifo kutowekwa wazi gazeti hili lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Wankyo Nyigesa ili kujua undani zaidi lakini bahati mbaya hakuweza kupatikana kutokana na simu yake kupokelewa na msaidizi wake.

 

“Mimi ni msaidizi wake, kamanda yuko kwenye majukumu mengine, kama unaweza piga simu baada ya saa mbili kupita.” Mwili wa marehemu Erick ulizikwa Novemba 8 mwaka huu, nyumbani kwao Mlandizi siku mbili baada ya tukio la mauaji kutokea na kwamba Maya alikuwa mikononi mwa polisi akisubiri taratibu za kisheria zifuate.

 

Wimbi la mauaji limetikisa karibu wiki nzima ambapo takriban watu saba wakiripotiwa sehemu mbalimbali nchini kuuawa huku wengi chanzo kikiwa ni wivu wa kimapenzi. Soma makala ukurasa wa pili.

STORI: MWANDISHI WETU, UWAZI

Je Rais Magufuli ‘Atawatumbua’ Maafisa Hawa?

Loading...

Toa comment