MREMBO AJIRUSHA GHOROFANI AFARIKI DUNIA KIKATILI

MREMBO aliyefahamika kwa jina moja la Khadija anadaiwa kujirusha kutoka ghorofani na kufariki dunia ambapo mpenzi wake aliyetajwa kwa jina la Ally Mansur anashikiliwa kutokana na tukio hilo. 

 

Inaelezwa na vyanzo mbalimbali kuwa mapema Jumapili iliyopita wawili hao walikodi chumba katika nyumba ya kulala wageni iitwayo Pasific yenye ghorofa tatu iliyopo Magomeni Mapipa Dar kabla ya mwanamke huyo kufikwa na balaa hilo majira ya saa nane usiku.

 

ILIKUWAJE AJIRUSHE?

Vyanzo vimeshindwa kubainisha kilichotokea chumbani kati ya wawili hao na hivyo kuacha utata kwa baadhi ya vyanzo kusema alijirusha na vingine kudai alirushwa. Kwa nini ajirushe au arushwe na kupoteza maisha? Hayo yanabaki kuwa ni maswali tata yanayosubiri mamlaka za uchunguzi kuja na majibu sahihi.

HUYU HAPA  MENEJA WA HOTELI

Kufuatia tukio hilo mwanahabari wetu alifika hotelini hapo na kuzungumza na meneja wa hoteli hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Venance Emmanuel ambaye alikuwa na haya ya kusema:

 

“Wakati tukio linatokea mimi sikuwepo lakini nilipigiwa simu na mlinzi wangu aliyenijulisha kuwa kuna mteja kaanguka kutoka ghorofa ya tatu na wanahisi amekufa hapohapo, hivyo nilitakiwa kufika haraka. “Nilipofika nilikuta watu wamejaa na mtuhumiwa ambaye ndiyo huyo mpenzi wake walikuwa wameshamdhibiti baada ya kutaka kutoroka.

“Nilichofanya niliwapigia simu polisi ambao walifika na kuondoka na mwili pamoja na mtuhumiwa.” Kufuatia sakata hilo mwanahabari wetu alimpigia simu Kamanda wa mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ACP Mussa Taibu ambapo alipokea msaidizi wake na kukiri kutokea tukio hilo na kusema mtu mmoja anashikiliwa na jeshi hilo na uchunguzi zaidi unaendelea.

 

Msaidizi huyo alipoombwa kutaja jina na nafasi yake kazini ikiwemo cheo alikataa kutoa ushirikiano huo na kusema: “Hayahaya maelezo nimekusaidia tu, vingenevyo ningekuambia RPC mwenyewe hayupo.” Uwazi bado linaendelea kuchimba tukio hili lenye utata na kwamba mapya yakipatikana yatawekwa haradhani.

Stori: RICHARD BUKOS, DAR ES SALAAM


Loading...

Toa comment