MREMBO AMTIA ADABU ZARI

DAR ES SALAAM: Maji yamekorogeka! Upepo bado siyo mzuri kabisa kwa upande wa mwanamama Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ kwani ameendelea kunyooshwa huko nchini kwao, Uganda, Gazeti la Ijumaa limekukusanyia habari mpya. Kama unakumbuka, mwishoni mwa wiki iliyopita, Zari ambaye ni mama wa watoto watano alijikuta kwenye wakati mgumu baada ya kushambuliwa na mashabiki wa mzazi mwenzake, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ au Mondi ambaye alimuabisha kwa kupata mapokeo mazuri nchini Uganda tofauti na matarajio ya wengi.

MREMBO ANITA AKINUKISHA

Baada ya Diamond kutinga nchini humo na kupiga shoo baab’kubwa huku Zari aliyekuwa nchini humo akipata mapokezi ya kawaida alipokuwa kwenye shoo ya Miss Uganda 2019 katika Ukumbi wa Hoteli ya Sheraton iliyopo Kampala, mrembo aitwaye Anita Kyalimpa a.k.a Anita Fabiola, 25, alikinukisha baada ya kumuita Zari ‘mama’.

MOTO WAKOLEA

Ukumbini humo mambo yalikuwa moto baada ya wawili hao kuonekana kurushiana maneno hadharani, jambo ambalo liliibua mjadala hata baada ya shoo hiyo kuisha na mrembo Oliver Nakakande, 24, kuvishwa Taji la Miss Uganda 2019.

MAFAILI YAFUKULIWA

Mitandaoni kulichafuka ambapo ‘mafaili’ mbalimbali yalianza kufukuliwa.Mitandao mbalimbali nchini humo ilimpa ushindi Anita kwa kusema amemnyoosha Zari ambaye ki-umri ni mkubwa kuliko Anita.Kwa sasa Zari ana umri wa miaka 40.“Zari alifikiri akimchezea Anita kwa kuwa yeye ni mkubwa na ana watu wengi kwenye mitandao ya kijamii hususan Instagram, angeweza kumficha, sasa aibu imekuwa kwake, Waganda wanamshambulia kwelikweli,” alichangia mdau mmoja kwenye mtandao wa nchini Uganda.

Hoja ya umri ndiyo iliyoshikiwa bango na wengi waliokuwa wanamtetea Anita mitandaoni wakieleza kuwa, mrembo huyo ni mdogo, lakini anafanya mambo makubwa kwenye jamii hivyo atakapofikia umri kama wa Zari, atakuwa ni moto wa kuotea mbali.

SILAHA ZAO…

Nyundo nyingine waliyoitumia mashabiki hao wa Anita kumgongea Zari ni kwamba walisema mrembo huyo ni mzuri kuliko Zari kwa kuzingatia ndiyo kwanza hajazaa hata mtoto mmoja hivyo uzuri wake hauna kifani huku pia wakisema Anita akivaa anapendeza kuliko Zari.

AHUSISHWA NA MONDI

Mashabiki hao wa Anita walikwenda mbali zaidi kwa kujiongeza kuwa eti hawaoni kipya kwa Zari kwani hata Mondi aliyewahi kuwa na Zari, aliwahi pia kuhusishwa na Anita miaka ya nyuma ambapo walifukua makaburi kwa kutupia picha iliyosemekana mrembo huyo mwenye mvuto wa kipekee alikuwa kwenye mawindo ya kumuingiza kingi Mondi.

WENGINE WAMTETEA ZARI

Licha ya mashambulizi kuwa makali sana kwa Zari kwenye mitandao ya Uganda, bado walikuwepo mashabiki wachache ambao walimtetea mrembo huyo kwa kusema kamwe Anita hawezi kumfikia hata afanye nini.

Hata hivyo, ukitazama maoni ya wengi kwenye mitandao mbalimbali ya nchini humo, utabaini kwamba Anita amemnyoosha Zari kwani watu wengi wameonekana kumkubali zaidi Anita na hivyo ugomvi ambao si wa kitoto aliouanzisha Zari kuonekana kama umemtokea puani ambaye alionekana kukaa kimya.

Wengi wamemsema Zari kwamba alipaswa kuwa mpole hata kama ana kinyongo na Anita kwani katika shoo hiyo, hakuambiwa neno baya lolote zaidi ya hilo la kuitwa mama wakati kiuhalisia yeye ni mama wa watoto watano.

ANITA NI NANI?

Anita ni binti mrembo mwenye figa matata ambaye umaarufu wake nchini Uganda upo katika vipengele vya; uigizaji, ubalozi wa utalii, mshereheshaji wa shughuli mbalimbali, mfanyabiashara na mtu wa kujitolea kwa jamii ambaye kutokana na umaarufu wake, amekuwa akipewa dili kubwakubwa za kuendesha shughuli za kitaifa nchini Uganda.


Loading...

Toa comment