The House of Favourite Newspapers

Mrembo auawa kwa risasi

0

Imelda Mtema na Mayasa Mariwata

MAJONZI! Msichana Mtanzania mwenye umri wa miaka 27, Shamsa Abdul Mshana mkazi wa Magomeni Mikumi jijini Dar, ameuawa kwa kupigwa risasi huko Lumbumbashi, nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo Jumamosi iliyopita na watu wasiojulikana.

Mdogo wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Sheila Mshana, alisema Shamsa aliyekwenda nchini humo kwa shughuli zake za kibiashara, alipigwa risasi usiku saa saba akiwa kwenye gari sambamba na mwenyeji wake, aliyetajwa kwa jina la Pipen, ambaye alinusurika baada ya kujificha kwa kuinama.
“Ni tukio la kuhuzunisha kwa kweli, maana tukitafakari tukio lilivyokuwa tunashindwa kupata majibu kama alimkosea mtu au ni mambo ya wivu wa binadamu, ndugu yetu alikuwa ni mfanyabiashara akichukua nguo hapa na kwenda kuuza huko na biashara ilikuwa inamuendea vizuri, huenda wenzake walimuonea donge.”

“Hii siyo mara ya kwanza kwenda ni safari yake ya pili na tangu aende kamaliza wiki tu, alipofika huko akapokelewa na huyo Pipen ambaye ni rafiki yake wa kawaida tu, si kwamba wana uhusiano wa kimapenzi na ni mtu mstaarabu, sasa kwa kuwa Shamsa alifia palepale hakuwa na uwezo wa kumuwahisha hospitali, polisi walivyofika ndiyo wakamkamata yeye kwa kuwa ndiye waliyemkuta naye na mpaka sasa bado anashikiliwa na polisi kwa uchunguzi zaidi,” alisema.

Alisema baada ya kupata habari za tukio hilo, walianza kushughulikia hatua za kuchukua mwili ili kuurejesha nyumbani, lakini zoezi hilo limekuwa gumu kwa serikali ya huko inataka ndugu wa damu ili kuthibitisha kama mwili huo ni wake.

“Hata baada ya kumpeleka ndugu yetu bado imekuwa ni tatizo, mambo hayaendi haraka licha ya kuongea na balozi wa DRC aliyepo nchini, ugumu unatokana na taratibu za uchunguzi na sheria zao zinasema baada ya maiti kukaa siku saba watazika wenyewe huko huko,” alisema.

Leave A Reply