Mrisho Gambo Kugawa Majiko 5,000 ya Gesi kwa Walimu Jiji la Arusha
MBUNGE wa Jimbo la Arusha Mjini, Mhe Mrisho Mshaka Gambo ameendelea kuonesha kuyajali makundi mbalimbali katika jimbo lake na sasa ni zamu ya walimu wa shule za sekondari na msingi wanaofundisha shule za private na za serikali.
Gambo ameamua kuitumia Siku ya Mwalimu Duniani, Jumamosi ya Oktoba 5, mwaka huu 2024 ili kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kwenye kampeni ya #NishatiSafi ya kupikia ambapo kwa kushirikiana na kampuni ya Oryx, Exim Bank na Ubalozi wa China atagawa majiko 5,000 ya gesi kwa walimu wote jijini Arusha.
Maadhimisho hayo yatafanyika siku hiyo kwenye Uwanja wa General Tyre Jijini Arusha kuanzia saa 3:00 asubuhi ambapo kauli mbiu itakuwa ni “Mwalimu ni Balozi wa Rais Samia kwenye kampeni ya Nishati Safi ya Kupikia”.
Wakizungumza kuelekea tukio hilo, walimu wamemshukuru Mbunge huyo kwa ubunifu huo wa kuwapatia motisha walimu wote bila ubaguzi, huku wakieleza kuwa, majiko hayo yatawasaidia kwa kiasi kikubwa katika shughuli zao za nyumbani na kuondokana na adha ya kuni na mkaa ili kulinda mazingira.