The House of Favourite Newspapers

Mrisho Mpoto: Atumiwa pesa na Wazungu kujifunza Kiingereza, azila

0

????????????????????????????????????

MPENZI msomaji wiki iliyopita katika simulizi hii tamu ya Mrisho Mpoto tuliishia mwaka 2001 alipofanyiwa mpango wa kwenda Marekani kushiriki projekti ya One Hand, Fingers ambayo ilikuwa ikihusisha nchi nyingine kama Kenya, Uganda, Tanzania, Marekani na Poland. Safari yake imekuwaje?

Tambaa nayo mwenyewe…

“Nikaenda na kufikia sehemu moja Marekani inaitwa Baltimore, Maryland katika Chuo Kikuu cha Towson. Nikakaa pale kama miezi sita hivi, nikarudi tena Tanzania.”

Kwa hiyo ukaribu wako na wale Wazungu uliendelea au ilikuwaje? Namchokonoa kujua zaidi.

“Wale wazungu walikuwa wakinifuatilia maisha yangu kwa ukaribu sana kupitia mawasiliano ya simu pamoja na e-mail.”

Kuna kitu amenitatiza na inabidi anipe ufafanuzi, namuuliza jambo hilo kwamba ilikuwaje katika mawasiliano, nani aliyekuwa akimsaidia kutuma e.mail na kuwasiliana kwa kutumia lugha ya Kiingereza, au aliingia kozi fupi?

(Anacheka kwa sauti ya juu, kisha anaendelea…)

“Nisome kozi fupi wapi Mpoto mimi? Kulikuwa na kaka yangu mmoja ambaye anaitwa Remmy Jusi Nyoni, yeye ndiye alikuwa akijibu e-mail zangu zote sambamba na kuwasiliana nao kwa njia ya simu. Tulikuwa tunaenda naye pale Cyber Cafe (Magomeni Mapipa, jijini Dar) anawatumia e-mail na hela zikitumwa natumia, nikitumiwa nakula na nyingine namtumia mama yangu, maisha yanasonga.”

Dah wewe Mrisho kweli noma, sasa vipi na ulivyoenda Marekani, nani alikuwa akikusaidia maongezi maana ni hatari sana, au uliumbuka?

“Haa haa kule Marekani niliongozana na Mkenya mmoja anaitwa Samweli Mwangi ambaye walimtafuta Wazungu wenyewe ambao alinisaidia sana kila nilipokuwa nasema yeye anatafsiri na kiukweli sikuwa najua kusema neno lolote la Kiingereza.

“Niliporudi niliendelea na kundi langu la Parapanda, nakumbuka kipindi kile ukatokea msiba mkubwa wa Taifa kwa kumpoteza mkombozi wa Taifa letu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kama utakumbuka kulikuwa hakuna wimbo wowote wa burudani zaidi ya maombolezo. Tukaitwa kurekodi Wimbo wa Nenda Mwalimu (Nyota) ambao kwa kiasi kikubwa naweza kusema ndiyo ulioninyooshea njia na kujulikana hadi hivi sasa.”

Vipi kuhusiana na mahusiano, hukuwa na mwanamke yeyote kwa kipindi hicho?

“Nilijisahau, wakati nimetoka kule Kigoma na kuingia rasmi Dar, pale nilipata kufahamiana na mwanamke mmoja anaitwa Mariam ambaye alikuwa akiimba sana nyimbo za dini ya Kiislamu. Mariamu alinifanya niipende sana dini ya Kiislamu kwa sababu kila kulipokuwa na mihadhara ya dini ya Kiislamu na Kikristo nilikuwa nikiambatana na kusikiliza ndiyo furaha yangu inaishia hapo, lakini kipindi chote hicho alikuwa ni mchumba tu.”

Tuendelee sasa, baada ya kuibuka na Wimbo wa Nenda Mwalimu na kukuweka katika ramani ya muziki, nini kilifuatia?

“Msiba wa taifa ulipopita, nikaendelea kupata ziara nchi nyingi sana za Ulaya kama vile Marekani zaidi ya mara tatu, Sauz Afrika nikapelekwa kusoma Story Telling na Poetry, Sweden, Scotland na nyingine nyingi.

Ebu nifafanulie hapo ulipoenda kusoma Story Telling Poetry ilikuwaje?

“Kwa kuwa nilikuwa nimeenda Ulaya mara nyingi, nikawa na uzoefu wa kuanza kuelewa lugha ya Kiingereza. Na nilipotua Johannesburg, Afrika Kusini nilifikia Chuo Cha Marketing Theatre Laboratory na kufundishwa jinsi ya kutohoa na kughani.”

Bado simulizi hii inaendelea kuwa tamu zaidi, Mrisho amepata shavu la kwenda nchi kibao kama Marekani, Scotland na sasa amefikia chuo cha Marketing Theatre, je? Nini kiliendelea?

Tukutane wiki ijayo kwenye gazeti hilihili.

Leave A Reply