Mrisho Ngassa Ajifua Na Pamba

ALIYEKUWA kiungo mshambuliaji wa timu ya Yanga ambaye kwa sasa anakipiga Mbeya City, Mrisho Ngassa, ameonekana akifanya mazoezi ya kujiweka fiti kuelekea ligi kuu msimu ujao akiwa na Pamba FC.
Ngassa ambaye ni kati ya wachezaji ambao wamewahi kuitumikia timu ya taifa, Taifa Stars, kwa mafanikio makubwa alionekana akifanya mazoezi hayo kwenye Uwanja wa Ndege wa jijini Mwanza.
Ngassa ameonekana akifanya mazoezi na timu ya Pamba ambapo baadhi ya mazoezi aliyofanya ni pamoja na kukimbia, kunyoosha viungo, kucheza mechi ambayo ilidumu kwa dakika 75.
Ngassa ameliambia Championi Jumatano, kuwa lengo la kufanya mazoezi na Pamba siyo kwamba amesajiliwa bali anauweka fiti mwili wake kuelekea Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.
“Kimsingi nilikuja Mwanza kwa matatizo ya kifamilia na nikaona ni vyema nifanye mazoezi na Pamba na lengo la kufanya hivyo ni kuweka mwili wangu kuwa katika hali nzuri ili niisaidie timu yangu ya Mbeya City iweze kufanya vizuri katika ligi ya msimu ujao,” alisema.
Ikumbukwe kuwa Pamba kwa sasa inajiandaa na Ligi Daraja la Kwanza ambapo tayari imeanza mazoezi yake na matarajio yake ni kuhakikisha kuwa timu hiyo inapanda daraja kucheza ligi kuu msimu ujao.

