DAR: Kile kitendawili cha mrithi wa usimamizi wa Makanisa ya Mlima wa Moto- Mikocheni B Assemblies Of God, yaliyokuwa chini ya Askofu Dk Getrude Pangalile Rwakatare ‘Mama Rwakatare’ nchini, kimeteguliwa ambapo sifa zake zimewekwa bayana, Risasi limetonywa.
Hatua hiyo inakuja kufuatia kifo cha ghafla cha mchungaji Rwakatare ambaye juzi Alhamisi, mwili wake ulipumzishwa pale Makao Makuu ya Makanisa ya Mlima wa Moto- Mikocheni B Assemblies Of God lilipo jijini Dar es Salaam.
Baada ya kifo hicho ambacho ni pigo kubwa kwa waumini wa kanisa hilo na Watanzania kwa ujumla, baadhi ya waumini wa Makanisa ya Mlima wa Moto yaliyotapakaa nchi nzima, wamekuwa njia panda juu ya nani atakayekalia kiti cha Mama Rwakatare na kuleta huduma bora ya kiroho kama ilivyokuwa awali.
Wakizungumza na gazeti hili juzi kanisani hapo, baadhi ya waumini waliojitokeza kumuaga mpendwa wao huyo, lakini ikashindikana kutokana na utaratibu wa Serikali ambapo kulikuwa na ulinzi mkali, walionesha wasiwasi wao juu ya nani ataweza kuchukua nafasi hiyo.
Katika mjadala na waumini tofautitofauti wa Mlima wa Moto, baadhi ya wachungaji kumi na wawili wa Mama Rwakatare walitajwa.
Hata hivyo, katika wachungaji hao kumi na wawili ambao mwenyewe alipenda kuwaita “Thenashara”, majina matano yalitajwa zaidi.
Miongoni mwa waliotajwa zaidi na waumini hao kuwa wanaweza kumrithi Mama Rwakatare ni pamoja na Mchungaji Sylvester Komba, Mchungaji Stanley Nnko, Mchungaji Janeth, Mchungaji Prisca Charles na Mchungaji Dickson.
Baadhi ya waumini hao walikwenda mbali zaidi na kumchambua mmojammoja kwa kutazama sifa za anayefaa zaidi kuwaongoza katika safari yao ya kumtafuta na kumtumikia Mwenyezi Mungu.
MCHUNGAJI SYLVESTER KOMBA
Wakimzungumzia Mchungaji Komba ambaye wengi walimsifu na kusema si mchungaji, tu bali ni askofu ambaye amekuwa mfano wa kuyaongoza makanisa hayo kwa upande wa Kanda ya Kati ambapo makao yake makuu yapo mkoani Dodoma na Kanda za Juu-Kusini.
Pia Mchungaji Komba amekuwa akitumiwa na Mama Rwakatare hasa alipokuwa na matukio makubwa na semina za mara kwa mara.
Walisema, Mchungaji Komba amefanyika baraka kwa walio wengi kwa kuwalisha neno lenye kufariji na kuinua kiroho. “Namkumbuka mno wakati wa ibada za kuinuliwa, huwa anaombea wenye mahitaji mbalimbali na kuwatamkia maneno ya baraka, na kweli baadaye watu kushuhudia kufanikiwa,” alisema mmoja wa waumini hao bila kutaja jina.
MCHUNGAJI STANLEY NNKO
Ilielezwa kuwa, huyu amekuwa akitumika kwenye Makanisa ya Mlima wa Moto na kuonesha cheche zake kiasi cha Mama Rwakatare kumtumia kwenye semina na hamasa mbalimbali ambazo hufanyika baraka mno kwa waumini wake.
“Huyu huwa anatoa ‘dozi’ ya uhakika ya neno, kama umefuatilia semina mbalimbali utaona baadhi ya watu waliweza kuleta vitu mbalimbali ili kuombewa kama vile maji, picha, nguo, mafuta, daftari, kalamu na vingine, kisha walikuja kutoa ushuhuda kwamba Mungu amewatendea makuu,” alisema muumini huyo.
MCHUNGAJI JANETH
Wakimzungumzia Mchungaji Janeth, waumini hao walisema ni mmoja wa wale Thenashara wa Mama Rwakatare ambaye amekuwa msaidizi wake wa karibu, hivyo kuwa na uzoefu wa kutosha.
“Huyu, mbali na kuwa na elimu kubwa ya kidunia, pia yupo vizuri kwenye elimu ya theolojia (Biblia),” alisema.
MCHUNGAJI PRISCA CHARLES
Taarifa zilizopatikana kanisani Mlima wa Moto zilieleza kuwa, huyu amekuwa akiongoza vipindi vya maombezi akishirikiana na jopo la wachungaji wa Kanisa la Mlima wa Moto.
“Hakika vipindi vya maombezi hujawa na upako wa aina yake na nguvu za Mungu na uwepo wake. Maelfu ya watu hujikuta wakimpigia Mungu magoti na kutubu dhambi zao chini ya Mchungaji Prisca ambaye ameandika Kitabu cha Nguvu ya Kuabudu kilichogusa mioyo ya wengi kanisani hapo.
MCHUNGAJI DICKSON
Inaelezwa kwamba, huyu naye ni miongoni mwa wale Thenashara wa Mama Rwakatare ambaye alikuwa naye bega kwa bega katika kumtumia kwa ajili ya kuhudumia watu wa Mungu.
“Hata pale mama alipokuwa hayupo, Mchungaji Dickson alifanya kazi yake kwa weledi mkubwa Kibiblia na kufanyika baraka kwa kanisa,” alisema muumini mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la Walter, mkazi wa Kawe jijini Dar.
KURA NYINGI ZAMWANGUKIA HUYU
Hata hivyo, kwa mujibu wa waumini wengi, kura nyingi zilikwenda kwa Mchungaji Komba huku wakiweka wazi kwamba ndiye mwenye sifa za kuweza kuvaa viatu vya marehemu mama Rwakatare.
Hata hivyo, wengi walisema kuwa suala la mtu kupewa nafasi ya uaskofu litahitaji kufunga na kuomba ili Mungu aoneshe ni nani chaguo sahihi la kumrithi Mama Rwakatare.
“Wanadamu wanaweza kuchagua kwa kutumia macho lakini Mungu huchagua kwa roho, atakayechaguliwa na Mungu ataliongoza kanisa la Bwana,” alisema muumini mmoja wa kanisa hilo aliyejitambulisha kwa jina moja la Devota mkazi wa Sinza jijini Dar.
SIFA ZA MRITHI WA MAMA RWAKATARE
Mmoja wa wachungaji waliozungumza na gazeti hili juu ya sifa za askofu atakayemrithi Mama Rwakatare aliyeomba hifadhi ya jina, alikuwa na haya ya kusema;
“Kwa kufuata misingi ya Biblia, sifa za mtu anayefaa kuwa askofu zipo wazi kabisa, zimeainishwa kwenye Kitabu cha 1Timotheo 3:1-7 ambapo maandiko yanasema: Ni neno la kuaminiwa, mtu akitaka kazi ya uaskofu, atamani kazi njema.
Basi imempasa askofu awe mtu asiyelaumika, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi na busara, mtu wa utaratibu, mkaribishaji, ajuaye kufundisha si mtu wa kuzoelea ulevi, si mpiga watu; bali awe mpole, si mtu wa kujadiliana, wala asiwe mwenye kupenda fedha, mwenye kuisimamia nyumba yake vema, ajuaye kutiisha watoto katika ustahivu (yaani, mtu asiyejua kuisimamia nyumba yake mwenyewe, atalitunzaje Kanisa la Mungu?)
“Wala asiwe mtu aliyeongoka karibu, asije akajivuna akaanguka katika hukumu ya Ibilisi. Tena imempasa kushuhudiwa mema na watu walio nje ili asianguke katika lawama na mtego wa Ibilisi,” alisema mchungaji huyo kwa sharti la kutotajwa jina na kuongeza:
“Sasa wataamua wenyewe wenye kanisa lao juu ya ni nani mwenye sifa hizo.”
MAMA RWAKATARE KWA UFUPI
Mama Rwakatare alikuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Mlima wa Moto.
Alikuwa ni mwanasiasa na mwanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Mbunge wa Viti Maalum huko Mvomero kuanzia mwaka 2008 hadi mwaka 2015 na baadaye aliteuliwa na Rais wa Awamu ya Nne, Dk Jakaya Kikwete kuwa Mbunge wa viti maalumu.
Mama Rwakatare aliyezaliwa Desemba 31, 1950, mwaka 1987 alianzisha mtandao wa Shule za St Mary kuanzia shule za awali, sekondari hadi vyuo. Alichangia mno kuinua sekta ya elimu nchini Tanzania.
Mwaka 1995 alianzisha Makanisa ya Mlima wa Moto yenye makao yake makuu, Mikocheni B jijini ambayo yamekuwa na waumini wengi nchini Tanzania. Mwaka 2006 alianzisha Kituo Kikubwa cha Watoto Yatima kilichokuwa na uwezo wa kuwapokea na kuwalea watoto 700. Kituo hiki kinajulikana kwa jina la Bright Future.
Akiwa na umri wa miaka 69, Mama Rwakatare alizikwa juzi Aprili 23, 2020 kwenye eneo la kanisa hilo Mikocheni B.
STORI: MWANDISHI WETU, RISASI


