Mrundi wa Mbao aanza kuiwinda Simba mapema
Ibrahim Mressy|CHAMPIONI|GPL
KATIKA soka la Tanzania, imebaki mechi moja tu kubwa, nayo ni fainali ya Kombe la FA kati ya Mbao FC na Simba itakayochezwa Jumamosi ijayo. Mbao baada ya juzi kuichapa Yanga na kusalia kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu, imeitangazia vita Simba.
Kocha mkuu wa kikosi hicho ambacho kimeishangaza Tanzania kwa kuifunga Yanga mara mbili msimu huu, mara moja ikiwa ni kwenye nusu fainali ya Kombe la FA, Mrundi, Ettiene Ndayiragije, amesema anaanza mara moja kuiwinda Simba watakayocheza nayo Jumamosi ijayo.
Mbao ambayo iliifunga Yanga bao 1-0, Jumamosi ijayo itapambana
na Simba ukiwa ni mchezo wa fainali ya Kombe la FA utakaopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma. Ikumbukwe kuwa, timu
hiyo iliifunga Yanga bao 1-0 kwenye mchezo wa nusu fainali ya Kombe la FA na kuitupa nje ya michuano hiyo. Lakini katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa ligi, Yanga ilishinda 3-0.
Ndayiragije amesema kuwa kitendo cha kuifunga Yanga mara mbili kinamfanya aingie kuikabili Simba akiwa na matumaini makubwa, hivyo anaanza mapema kuwaandaa vijana wake kuibuka na ushindi na kuwa mabingwa wa FA.
“Kitendo cha kumfunga bingwa mtetezi mara mbili kwenye uwanja wetu wa nyumbani ni jambo zuri ambalo linatupa morali ya kuendelea kupambana zaidi na zaidi katika mchezo wetu ujao dhidi ya Simba.
“Ligi imeisha, hivyo tunaanza haraka maandalizi ya mchezo huo ambapo imani yetu kubwa ni kuibuka na ushindi na kuchukua ubingwa huo, niwaombe mashabiki wa Mbao waje kwa wingi kutusapoti siku hiyo,” alisema Ndayiragije.