The House of Favourite Newspapers

MSALA! MAMA MBARONI KWA KUUA KICHANGA CHAKE

Amina Keneth

MWANAMKE mmoja aliyefahamika kwa jina la Amina Keneth (26), mkazi wa mtaa wa Mwasanga, Kata ya Itiji jijini Mbeya, ametiwa mbaroni kwa tuhuma za kujifungua mtoto jinsi ya kike mwenye umri wa siku moja kisha kumtumbukiza kwenye mfuko wa sandarusi (rambo) kisha kumtupa mita sabini kutoka nyumbani kwake.  Akizungumza mara baada ya kukamatwa na polisi, Amina alisema, sababu za kumtupa mtoto huyo ambaye alikutwa amefariki ni ugumu wa maisha na kutomtambua mwanaume aliyempa ujauzito.

Tetesi za kutupwa kwa kichanga hicho ziliibuliwa na baadhi ya wanawake mtaani hapo ambao walifanya uchunguzi na kubaini Amina kuhusika na tukio hilo ambapo katika mahojiano alikiri kuhusika na tukio hilo.

“Nilipojifungua nikaona sina mtu wa kunisaidia kumlea mtoto na baba yake simfahamu nilisubiri ilipofika usiku nilimviringisha kwenye shuka nikamweka kwenye rambo nikaenda kumtupa ingawa moyo ulikuwa unaniuma,” alisema Amina huku akibubujikwa na machozi. Hata hivyo, tangu kujifungua Amina alikuwa hajala wala kuoga ambapo wasamaria wema ambao hawakupenda kutajwa majina yao walijitolea kumuogesha na kumpa kikombe cha uji.

Jonas Mwasanga ambaye ni Mwenyekiti wa Mtaa Mwasanga, alisema baada ya kupata taarifa za tukio hilo, alitoa taarifa Kituo Kikuu cha Polisi ambapo polisi wa kitengo cha Dawati la Jinsia walifika na kuuchukua mfuko wa sandarusi uliokuwa na mwili wa mtoto huyo na kwenda nao kituoni kwao kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Mwenyekiti Mwasanga alimteua Brandy John kuongozana na Amina Hospitali ya Wazazi Meta kwa ajili ya matibabu. Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na wanafanya uchunguzi na wakikamilisha watamfikisha mtuhumiwa mahakamani

Comments are closed.