The House of Favourite Newspapers

Msala Mpya! Mondi Kortini Tena

0

DAR: Huu ni msala mpya! Baada ya miaka miwili iliyopita kupandishwa kizimbani akidaiwa matunzo ya mtoto aliyezaa na mwanamitindo Hamisa Mobeto, staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ ameburuzwa kortini kwa mara nyingine.

 

Habari za uhakika zinaeleza kuwa, Diamond au Mondi ameburuzwa kortini huku tuhuma za mamilioni zikitajwa.

 

Habari zinaeleza kuwa, Mondi alipelekwa kortini kutokana na tuhuma za uharibifu wa mali ndani ya nyumba aliyokuwa amepanga kwa ajili ya studio maeneo ya Kijitonyama jijini Dar kabla ya kuhamia Mbezi-Kwa Zena jijini Dar zilipo ofisi za Wasafi kwa sasa.

 

Diamond baada ya kuhama hapa, ndani ya nyumba waliyokuwa wameweka studio, kuna uharibifu mkubwa sana kuanzia milango, madirisha mpaka taa, jambo ambalo limesababisha mwenye nyumba aende mahakamani, mtafuteni mtapata habari nzima,” alisema mtoa habari wetu ambaye yupo karibu na nyumba hiyo.

 

MWENYE NYUMBA SASA

Baada ya kunyetishiwa habari hiyo, Gazeti la IJUMAA WIKIENDA lilimtafuta mwenye nyumba ambaye alijitambulisha kwa jina la Maulid Wandwi ambaye alikiri tukio hilo kuwepo na kueleza ilivyokuwa.

 

Mwenye nyumba hiyo yenye kiwanja No.556, Kijitonyama Block 47, alisema mwaka 2016 aliingia mkataba na Mondi na kumpangishia nyumba yake ikiwa kamili, yaani mita ya umeme, maji, madirisha, milango, AC (Air Condition), feni na kila kinachohitajika ndani ya nyumba.

 

Alisema kuwa, alimpangishia kwa kodi ya shilingi milioni moja kwa mwezi ambapo alilipa shilingi milioni 12 ya mwaka mzima na nyumba hiyo akawa anaitumia kwa ajili ya shughuli zake za kimuziki, ikiwemo studio.

 

APATA TAARIFA KWA JIRANI

Mwanzoni mwa mwaka 2019, Wandwi alipata taarifa kutoka kwa jirani yake anayeitwa Ramadhani kuwa, kwenye nyumba yake kunaonekana mlango wa uani umevunjwa na hakuna hata dalili za watu kuwepo kama ilivyokuwa awali.

 

“Baada ya jirani kuja kunipa taarifa maana mimi ninaishi Kinondoni, nilikuja nikakuta geti limefungwa. Hivyo ikabidi niende kutoa taarifa kwa Serikali ya Mtaa wa Mpakani B, Kata ya Kijitonyama, nikaja nao ambapo mmoja wa watu niliokuja nao aliruka ukuta maana geti lilikuwa limefungwa kwa nje na Diamond hakuwa amenirudishia ufunguo mpaka sasa.

 

“Aliyeruka ukuta alivunja geti kwa ndani, tukaweza kuingia na kukutana na uharibifu mkubwa huku majani na takataka kibao zikiwa zimetawala ndani ya nyumba.

 

“Viongozi hao wa mtaa walifanya ukaguzi wao kisha baadaye tukaenda kuripoti Polisi huku nikiendelea kumtafuta Diamond, lakini akawa hapokei simu wala kujibu meseji zangu mpaka sasa.

“Nilijaribu kumtafuta meneja wake, Babu Tale, lakini naye amekuwa akiahidi tu na kunipiga chenga kila kukicha,” alidai Wandwi.

 

ATINGA KORTINI

Kutokana na kwamba Mondi aliitwa Polisi, lakini akashindwa kufika, kesi hiyo ilipelekwa katika Mahakama ya Ardhi Wilaya ya Kinondoni na kufunguliwa faili namba 394 ambako imeshatajwa zaidi ya mara tatu, lakini Diamond hajawahi kufika.

 

“Kesi imekuwa ikitajwa tu zaidi ya mara tatu tangu mwaka jana, lakini Diamond haonekani, wanaokuja ni mawakili wake ambao kila wakihudhuria wanasema yupo Ulaya.

 

AOMBA HAKI ITENDEKE

“Naomba nisaidiwe ili haki itendeke kwani hapa nilipo nina matatizo ya moyo, kansa na hivi karibuni nilifanyiwa upasuaji wa macho, sioni. Hivyo, hii nyumba ndiyo ninaitegemea kwa ajili ya kuendesha maisha,” alisema Wandwi kwa shida huku akitetemeka kutokana na matatizo aliyonayo.

 

TUHUMA ZA MAMILIONI

Kwa mujibu wa wasanifu majengo waliofanya uchunguzi wa vitu vilivyoharibika, walionesha kuwa vina thamani ya shilingi milioni 33, 742,100 ambazo Mondi anatakiwa azilipe.

 

Vitu ambavyo vilionekana kuibiwa au kutokuwepo ni milango yenye vitasa 11, air condition 4 aina ya Sanyo, sinki la jikoni, water pump, taa zote, luku, baadhi ya soketi za umeme na waya za umeme, milango ya makabati ya jikoni (7), kikabati cha ukutani (jikoni), kioo cha chooni (juu ya sinki), mlango mmoja wa grili, koki za maji (nje ya nyumba) na feni moja (nyumba ndogo ya uani.

 

Pia karatasi ya ukaguzi huo wa Serikali ya Mtaa inaonesha kuwa walikuta nyumba ikiwa kwenye hali ya uchafu ndani na nje ya nyumba kitu kilichothibitisha kutokuwepo kwa watu muda mrefu.

Tofauti na vitu hivyo ambavyo havikukutwa ndani, pia bili ya maji inaonesha kuwa ni zaidi ya laki sita.

 

DIAMOND ANASEMAJE?

Ili kuleta usawa wa habari, Gazeti la IJUMAA WIKIENDA lilimtafuta Mondi kwa njia ya simu, lakini simu yake iliita bila kupokelewa.

 

MENEJA WAKE ANENA

Baada ya Mondi kukosekana, walitafutwa mameneja wake, kuanzia Sallam Sk ambaye alikuwa hapatikani hewani, Said Fela ambaye simu iliita bila kupokelewa na Tale ambaye alipatikana hewani.

Tale alisikiliza maelezo yote juu ya madai ya mzee huyo ambapo awali akakanusha habari hizo, lakini baadaye akajibu kuwa hawezi kuzungumza kitu ambacho kiko mahakamani kwa sababu anaweza kujikosesha haki yake.

 

“Kwanza hiyo habari siyo ya kweli, halafu kitu kikiwa kipo kisheria huwezi kukizungumzia au kusambaza mtandaoni. Kwa hiyo siwezi kuzungumzia maana ni jambo la kisheria, unaweza kujikosesha haki ya msingi,” alisema Babu Tale.

 

SI MARA YA KWANZA

Si mara ya kwanza kwa Mondi kuburuzwa kortini, kwani mbali na Mobeto kumpandisha kizimbani akidai matunzo ya mtoto, pia aliwahi kufikishwa kortini na Bendi ya Msondo Ngoma akidaiwa kutoa Wimbo wa Zilipendwa alioiga melodi za bendi hiyo bila ruhusa yao.

Leave A Reply