MSANII APIGWA MIMBA YATOKA

DAR ES SALAAM: MAMBO mengine yanatafakarisha! Hivi inawezekanaje umkataze mtu atukane halafu ageuke mbogo na baadaye kukushushia kipigo hadi ujauzito uharibike? Amani limepokea kisa hiki na linakupakulia. 

 

Msanii wa filamu Bongo, Nia Jastine ‘Mama Cheni’, mkazi wa Tabata-Kimanga jijini Dar es Salaam amedai kupigwa na mwanamke mwenzake akishirikiana na rafiki zake hadi mimba ikaharibika katika tukio lililotokea Julai 3, mwaka huu.

 

Akieleza kisa cha kipigo hicho huku akimtuhumu mwanamke aliyemtaja kwa jina moja la Mwamvua ambaye ni jirani yake, msanii huyo alisema: “Nilikuwa nimekaa nyumbani kwangu, Mwamvua akaanza kutukana matusi mazito kwa sauti kubwa, nikatoka kumkataza kwa kuwa mimi nina watoto nikamwambia watasikia na kujifunza tabia mbaya.”

 

Msanii huyo anaeleza kuwa, Mwamvua hakupendezwa na kitendo cha yeye kukatazwa asitukane na hivyo kuanza chokochoko za maneno ambayo baadaye yalizaa ugomvi. Nia alisema, baada ya kuona kuna shari inatengenezwa na Mwamvua aliamua kurudi kwake na kumwacha akiendelea kutukana.

 

Aliongeza kuwa, baadaye Mwamvua anadaiwa kuwaita rafiki zake wengine watatu ambao ni Hamissa, Mama Aklam na mwingine hakufahamika na kuwasimulia jinsi Nia alivyomkanya matusi na hivyo kupanga njama za kumshikisha adabu.

 

Nia alisema kuwa, baada ya vuguvugu la ugomvi kutulia alidhani yamekwisha na hivyo aliamua kutoka kwake na kwenda kwa fundi nguo ambako anadai kufuatwa na Hamissa ambaye ni rafiki wa Mwamvita na kupigwa na kitu kizito tumboni. “Nikashangazwa na kitendo hicho ikabidi niondoke kurudi nyumbani huku nikiwa na maumivu tumboni.

 

Msanii huyo anaendelea kudai kwamba, baada ya kurudi kwake, Mwamvua na wale rafiki zake wengine walimvamia na kuendelea kumpiga hadi alipokuja kuokolewa na mumewe baada ya kurudi. “Mume wangu alituamua na kuniambia twende Kituo cha Polisi Tabata Shule ambako tulipewa PF3 (Fomu namba tatu ya polisi kwa ajili ya matibabu).

“Pia tulifungua jalada la kesi lenye namba TBT/ RB/3461/2019 na kuondoka kwenda hospitali, daktari aliponipima kwa sababu nilikuwa na mimba ya miezi mitatu akasema imeharibika.

 

Kwa kuwa Kamanda wa polisi Mkoa wa Ilala, Zuberi Chembela hakupatikana kuzungumzia tukio hilo lakini chanzo kutoka ndani ya jeshi la polisi kinasema mtuhumiwa mmoja amekamatwa na wengine wanaendelea kusakwa baada ya kutoroka.

 

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Tabata- Kimanga ambaye pia ni Diwani, Manase John Mjema amethibitisha kutokea kwa tukio hilo. “Hao watuhumiwa wachukuliwe hatua za kisheria, hivi ninavyokuambia mmoja kati ya hao (hakumtaja jina) aliwahi kunitukana hata mimi wakati nafanya kazi yangu, hapa nina RB yake nakwenda kuunganisha mashtaka ili kesi iende mahakamani,” alisema diwani huyo.

 

AMANI LACHIMBA ZAIDI KISA

Kutokana na kisa cha kupigwa kilichotajwa na Nia kuwa na maswali mengi na upande wa pili kukosekana kuelezea tukio, Amani liliingia kazini kuchimba uhusiano wa wanawake hao na kubaini kuwa wamekuwa katika ugomvi wa muda mrefu unaotokana na masuala ya mapenzi.

 

“Mwamvita anatembea na mdogo wa Nia ambaye amekuwa akidaiwa kukatazwa na dada yake kutembea na Mwamvita na hivyo kuleta chuki kati yao,” chanzo cha karibu na wanawake hao kilidai.
Toa comment