The House of Favourite Newspapers

Mshahara wa Chama Simba ni Kufuru

0

KESI imeisha sasa! Ndiyo kauli ambayo unaweza kusema baada ya kiungo mshambuliaji wa Simba, Clatous Chama kuamua kusaini mkataba mpya wa miaka mitatu wa kuendelea kubakia klabuni hapo na kuziacha baadhi ya ofa ambazo alizipata.

 

Miongoni mwa ofa ambazo Chama alizipata ni kutoka kwa Yanga lakini bosi Tajiri Mohamed Dewji ‘Mo’ ameamua kumaliza kazi kwa kumpa mshahara wa kufuru na kumsainisha mkataba wa miaka mitatu kwa milioni 500.

 

Chama amepewa mshahara wa shilingi milioni 18 kwa mwezi ambapo kwa mwaka atavuna Sh milioni 216 na kwa miaka mitatu atakayokaa klabuni hapo atakunja Sh milioni 648 kwenye mshahara tu.

 

Mshahara huo wa Chama, unalipa wachezaji watatu mastaa wa Yanga kila mwezi na chenji inabaki, ambao ni washambuliaji Yacouba Songne na Michael Sarpong wanaokunja Sh milioni 7 kila mmoja kwa mwezi, pamoja na Deus Kaseke ambaye anakomba mil 3 kila mwezi.

Kiungo huyo mzaliwa wa Zambia, mshahara wake umeongezwa kwa kuwa katika mkataba wa awali, alikuwa akilipwa Sh mil 13 kwa mwezi.

 

Hii maana yake ni kwamba, Chama ambaye mkataba wake mpya unamalizika mwaka 2023, sasa ndiye mchezaji anayelipwa kuliko wote Bongo.Chanzo kutoka Simba kimeliambia Championi Jumatatu, kuwa kiungo huyo amefurahi kuendelea kubaki kuichezea Simba.

 

“Suala la mkataba hilo siyo ishu kwa sababu alishasaini tangu mwaka jana na hata zile picha ambazo zimetoka kwenye mtandao ni za muda, wala siyo mpya.“Ishu ni kwamba kwenye mkataba wa sasa atachukua kitita cha milioni 18 ambazo kwa hapa Tanzania hakuna ambaye anachukua kwa upande wa wachezaji na kumfanya kuwa mchezaji anayevuta kitita kikubwa zaidi kwa mwezi.

 

“Awali kabla ya kusaini, alikuwa anavuta mil 13 kwa mwezi, hivyo kwa hesabu za haraka katika mkataba huo wa miaka mitatu ambao utaisha 2023, atavuna milioni 648 ndani ya muda wa mkataba wake wote,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:“Kwa sasa mtu ambaye anafuata kuongeza mkataba ni Jonas Mkude kwa sababu kulishakuwa na maongezi ya muda mrefu tangu Chama alivyosaini.“

 

Muda siyo mrefu naye atasaini mkataba wake mpya kwa sababu walikuwa wamefikia sehemu nzuri kwa pande zote mbili,” kiliweka nukta chanzo hicho.Aidha, taarifa zinasema hivi sasa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Mohamed Dewji ‘Mo’ amepata jeuri za kumuongezea mkataba huo kutokana na fedha za Caf ambazo ni Sh bilioni 1.5 watakazozipata baada ya kufuzu hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa.“

 

Mo ametumia kufuru ya kumuongezea mkataba Chama baada ya kupata uhakika wa kuzipata Sh bilioni 1.5 kutoka Caf, hivyo akatumia umwamba wake wa kumpa kitita hicho cha pesa ambacho kitarudi kwenye akaunti yake baada ya timu hiyo kukabidhiwa bilioni hizo,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Mo hivi karibuni alithibitisha kufikia makubaliano mazuri na Chama kwa kumuongezea mkataba huku akitamba kutoruhusu mchezaji yeyote anayehitajika kuondoka baada ya mkataba wake kumalizika.“

 

Niwaahidi Waandishi wa Habari kuwa, Simba haitakubali kumuachia mchezaji yeyote atakayehitajika katika timu, tupo tayari kumbakisha yeyote tutakayemuona anafaa kwa faida ya timu,” alisema Mo.

Waandishi: Marco Mzumbe, Said Ally na Wilbert Moland

Leave A Reply