The House of Favourite Newspapers

Mshahara wa Kaze Wamfunika Bongo

0
Kocha Mkuu wa Yanga Mrundi Cedric Kaze.

ACHANA na rekodi nzuri aliyoanza nayo kwenye raundi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara, Kocha Mkuu wa Yanga Mrundi Cedric Kaze ameweka rekodi nyingine ya kuwa kocha anayelipwa mshahara mkubwa zaidi ya makocha wote Bongo.

 

Kaze alijiunga na Yanga katikati ya raundi ya kwanza ya ligi akichukua nafasi ya Mserbia Zlatko Krmpotic, aliyesitishiwa mkataba wake na waajiri wake kutokana na mwenendo mbaya wa michezo minne ya ligi ya mwanzoni.

 

Kocha huyo alianza vizuri ligi kwa kucheza michezo 11 ya ligi bila ya kufungwa tangu alipokabidhiwa kikosi hicho kinachoongoza katika msimamo kikiwa na pointi 43, kikicheza michezo 17.

 

Mrundi huyo kwa sasa hakamatiki kwa mshahara kwani ndiye anayechota mkwanja mkubwa ndani ya Bongo na inadaiwa analipwa kitita cha dola 10, 000 ( zaidi ya Sh 22Mil), kutoka kwa mdhamini wao Bilionea Gharib Said Mohammed (GSM).

Kaze anadaiwa anapokea mshahara huo tofauti na posho ambazo anazichukua kila timu inapopata matokeo mazuri ya ushindi katika michezo yake ya ligi na Kombe la FA.

 

Kocha wa Simba Mbelgiji, Sven Vandenbroeck ndiye anayemfutia Kaze ambaye yeye anachota kitita cha dola 9,000 ambazo ni sawa na Sh 20Mil kwa kila mwezi.Simba wao wana jeuri ya kumlipa kocha huyo kiwango hicho cha mshahara kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Bilionea Mohammed Dewji ‘Mo’ ambaye yeye ndiye anayetoa fedha ya usajili ya wachezaji kimataifa na kitaifa.

 

Awali, Sven ndiye alikuwa akiongoza kwa makocha wanaolipwa mishahara mikubwa Bongo kabla ya Kaze kujiunga na Yanga katika msimu huu.Kocha anayefuatia ni Mzambia, George Lwandamina, aliyejiunga na Azam FC wiki iliyopita akimrithi Mromania Aristica Cioaba, ambaye ameondolewa katika timu hiyo kutokana na mwenendo mbaya wa matokeo ya michezo iliyopita ya ligi.

 

Yeye anakunja kitita cha dola 9,000 ambazo ni sawa na Sh 20Mil kwa mwezi.Mromania huyo alianza kwa kasi kubwa katika kikosi hicho ikiwemo kuongoza ligi kabla ya kushushwa na Yanga kileleni kwa kucheza mechi saba mfululizo na kupata ushindi.

 

Mecky Maxime wa Kagera Sugar anachukua nafasi ya nne bora ya makocha wanaolipwa mshahara mkubwa katika msimu huu akilipwa Sh 5Mil.

Ni kati ya makocha bora katika ligi ya hapa nyumbani.Kocha huyo ameiongoza vizuri timu yake ya Kagera ambayo hivi sasa ipo katika nafasi ya saba katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 22, ikicheza michezo 17.

 

Kocha wa Ruvu Shooting Charles Mkwasa, anashika nafasi ya tano katika orodha ya makocha wa Bongo ambaye yeye kila mwisho wa mwezi akaunti yake inasoma Sh 3.5Mil.

 

Alijiunga na Ruvu baada ya kuachana na Yanga katikati ya msimu huu ambaye tangu ametua hapo ameonekana kuibadilisha timu hiyo huku akifanikiwa kuwafunga Simba bao 1-0 katika mchezo wa ligi.

 

Ruvu ambayo hivi sasa inaitwa Barcelona ya Bongo kutokana na soka safi la pasi wanalolicheza ipo nafasi ya tano katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 25 katika msimamo.

Stori: Wilbert Molandi na Khadija Mgwai,Dar

Leave A Reply