The House of Favourite Newspapers

Mshahara wa Kichuya Kwa Waarabu Usipime

Mshambuliaji Shiza Kichuya.

WAARABU wanapotaka mafanikio hawataki utani kwani katika usajili wao wa hivi karibuni kwa mshambuliaji Shiza Kichuya wamekubali kulipa mshahara wa dola 9,000 (Sh mil 21) kwa mwezi.

 

Championi linajua kwamba mastaa Kichuya aliowaacha Simba, Emmanuel Okwi analipwa Mil 14 Simba huku Meddie Kagere akikinga Mil 12.

 

Kichuya alijiunga na Pharco FC ambayo inashiriki Ligi Daraja la Kwanza Misri na baadaye akatolewa kwa mkopo kwenda timu ya ENPPI inayoshiriki ligi kuu ya nchini humo.

 

Kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika ambacho ni mtu wa karibu na Kichuya, ameliambia Championi Jumamosi kuwa, Kichuya analipwa mshahara wa dola 9,000 kwa mwezi ambapo akiwa Simba alikuwa akilipwa Sh mil 5.

 

Kilisema kutokana na kutangaziwa dau hilo Kichuya alikubali na hata Simba hawakuwa na kinyongo naye kwani walionyesha mapema nia ya kutaka kuona mchezaji huyo akipiga hatua kimataifa. “Kichuya ana bahati sana
mchezaji anasajiliwa daraja la kwanza na analipwa kiasi cha dola 9,000 sio jambo dogo na hili linaweza kuwapa nafasi hata wachezaji wenzake waliopo hapa Bongo kuweza kuweka bidii na kupata nafasi za kucheza nje.

 

“Sababu Kichuya kafanikiwa kutoka nje kutokana na uwezo wake na kuonekana kwenye mechi hizi za kimataifa hivyo wachezaji wengine ni wao kuongeza bidii hasa kama hawa wa Simba wanaoshiriki michuano ya kimataifa,” kilisema chanzo cha kuaminika.

 

Championi Jumamosi lilimtafuta Kichuya azungumzie ishu hiyo alipatikana na kugoma kuweka wazi. Mpaka sasa Kichuya tangu atue ENPPI amefanikiwa kucheza mechi mbili dhidi ya Al Ahly ambayo alianza kikosi cha kwanza na ile ya pili alitokea benchi mbele ya Zamalek.

MARTHA MBOMA, CHAMPIONI

Comments are closed.