The House of Favourite Newspapers

MSIMAMO; SILAHA KUBWA YA MAFANIKIO PENZINI

JUMATATU nyingine nzuri imewadia. Mungu ametupa upendeleo mimi na wewe kuiona siku hii. Ni vyema tumshukuru yeye kwa zawadi hii ya uhai. Kama afya kidogo inakuletea changamoto usijali, Mungu wetu ni mkuu atakupigania utapona.  Nikirudi kwenye mada yangu ya leo kama inavyojieleza hapo juu. Kwenye ulimwengu wa masuala ya mahusiano hakuna kitu kina umuhimu mkubwa sana kama msimamo. Msimamo ndio unaoamua hatma ya maisha yako katika safari ya mahusiano.

Mimi na wewe ni mashahidi katika hili, mtu anapokuwa kwenye hatua ya kutafuta mwenza wa maisha kuna ile hali ya kutapatapa. Unasema labda huyu ni mtu atakayenifaa, unakutana na mwingine naye unamuona bora zaidi ya yule wa awali. Hapo ndipo baadhi ya watu wanapochanganyikiwa na kujikuta wakiyumbayumba. Wanapoteza uelekeo katika uhusiano na kujikuta hata akiwa na mahusiano mengi tofauti. Anakuwa na wapenzi wawili au hata zaidi huku akishindwa kujua abaki na nani.

Anahangaika kwamba huyu ana fedha lakini hana mapenzi ya dhati. Mwingine ana mapenzi ya dhati lakini labda pengine ni mlevi. Mwingine anaweza kuwa na tabia mbaya au pengine hajatulia ni malaya, hawezi kuwa na mpenzi mmoja. Unakuta mtu kichwa kinamzunguka tu hajui cha kufanya. Na hapo ndipo unapoona mtu anapoteza uelekeo na kuwa na uhusiano zaidi ya mmoja ili tu aweze kumtafuta yule ambaye ni sahihi.

Bahati mbaya sana asipoangalia atajikuta anatembea kila siku na watu tofauti. Ndugu zangu hili ni jambo baya, kuwa na wenza zaidi ya mmoja ni hatari. Unapaswa kuwa na msimamo ili uweze kwenda vizuri. Kabla ya kuingia kwenye uhusiano wowote ule unapaswa kumjua huyo mtu kwa maana ya tabia na mambo mengine. Hakuna mwanadamu aliyekamilika lakini angalau ukishaona ana sifa baadhi ya unazozitaka wewe basi fanya maamuzi sahihi ya kutulia naye. Jiridhishe kwa muda kabla ya kumkabidhi moyo wako. Mfanye mtu awe rafiki kwa muda kisha ufanye maamuzi.

Wengi wetu tumekuwa tukikosea sana katika eneo hili, tunawapenda watu haraka kabla hata hatujawajua vizuri. Baadaye unakuja kugundua si mtu sahihi wakati tayari moyo wako ulishazama na unakuta ni vigumu kutoka. Nasisitiza, jiridhishe vya kutosha. Ukishajiridhisha basi fanya maamuzi sahihi. Mkabidhi mtu moyo wako hata kama atakuwa na upungufu fulani. Utamsaidia kutoka kwenye huo upungufu alionao.

Jitoe kweli kwa yule ambaye tayari umempa moyo wako. Acha kuyumbishwa tena na watu wengine. Umeamua kuwa na fulani basi asitokee mtu mwingine wa kukuyumbisha na kukuambia sijui anakuhitaji halafu na wewe unalainika na kuanzisha naye uhusiano. Kuwa na msimamo, heshimu pia hisia za mwenzako. Kama kweli amekupenda, amekuthamini basi nawe muweke moyoni. Wengine wote waweke pembeni. Tamaa za fedha, uzuri wa sura na mambo mengine yote unapaswa kuyaweka kando. Muone yule wa kwako ndio bora kuliko wengine.

Ukiwa na msimamo utampenda hata kama mtu hana kitu. Ukiwa na msimamo utakuwa huru na mwenzako. Mtaishi maisha yenu, mtapanga namna gani mnataka kufanikiwa pamoja na hata katika shida mtakuwa pamoja. Ni matumaini yangu mtakuwa mmenielewa, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri. Unaweza kunifuata kwenye mitandao ya kijamii, Instagram na Facebook natumia Erick Evarist, Twitter natumia ENangale.

Comments are closed.