The House of Favourite Newspapers

MSIMAMO WA GLOBAL PUBLISHERS SAKATA LA BUNGE LA ULAYA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.

TUMECHAGUA KUSIMAMA NA RAIS WETU

Tumesoma barua ya maazimio 15 ya Bunge la Umoja wa Ulaya (European Union) kwa serikali yetu ya Tanzania. Maazimio hayo yanabeba masharti magumu kwa sababu kwenye barua yao wanazungumzia ushoga. Lakini pia kuna mambo mengine yametajwa kwenye maazimio hayo kama demokrasia na kutetereka kwa Haki za Binadamu.

 

Tayari Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango amesema kama nchi tutapita kwenye wakati mgumu kidogo kwani tutakosa ushirikiano kutoka kwa wahisani kutokana na msimamo wetu.

 

Sisi kama Kampuni ya Global Publishers, tumechagua kusimama na rais wetu, Dk. John Pombe Magufuli kuyapinga maazimio hayo kwani inaonesha wazi yamekuja kutokana na msimamo wake thabiti juu ya usimamizi wa rasilimali zetu.

 

Ndiyo, ni kutokana na msimamo wake juu ya rasilimali zetu kuanzia rais wetu alipozuia mchanga wa dhahabu (makinikia) na kudhibiti Tanzanite, lakini kamwe hatutakubali kuburuzwa na tutaendelea kusimamia mila na desturi zetu.

 

Tunajua hii ni vita ya kiuchumi na kama taifa tunatakiwa kutumia akili nyingi na siyo nguvu, tupo tayari kuungana na rais wetu kwa kutumia akili zetu nyingi tulizonazo. Tuamini kwamba tunaweza bila hata kuwategemea baadhi ya hao wahisani wenye masharti magumu na yasiyotekelezeka.

 

Tunawaomba Watanzania wengine pia kusimama na rais wetu katika kutetea maslahi ya nchi.

Comments are closed.