Msimu Mpya wa The Playlist Usipime!
BAADHI ya mastaa wa muziki wa Bongo Fleva akiwemo Ben Pol na Joh Makini mwishoni mwa wiki iliyopita waliweka shangwe za kutosha ndani ya Studio za Times FM katika uzinduzi wa msimu mpya wa Kipindi cha The Playlist kinachorushwa na Redio Times FM (100.5).
Akizungumza na mtandao huu mtangazaji wa kipindi hicho, Omary Tambwe ‘Lil Ommy’ alisema kuwa msimu huo ambao ni wa nne kufanyika katika redio hiyo, mashabiki mbalimbali walipata nafasi ya kutuma SMS na kuchagua nyimbo wanazozipenda na kupigiwa.
“Lilikuwa ni tukio kubwa ambalo hakuna redio ambayo imewahi kuzindua hivi kama Times FM, mastaa waliandaliwa mazaga kibao kama vile Snacks, Champagne, Soft Drink na mengine kibao na kizuri zaidi kulikuwa na live interviews,” alisema Lil Ommy.
Kipindi cha The Playlist huwa kinawakaribisha mastaa live redioni kuchagua nyimbo tano wanazopenda na kufanya nao mahojiano. Huruka hewani kila Jumamosi Saa 6 hadi Saa 8 mchana kupitia masafa ya 100.5 Times FM.