The House of Favourite Newspapers

Msolla Afungukia Mwambusi Kuondoka Yanga

0

MWENYEKITI wa Klabu ya Yanga, Dk Mshindo Msolla, amefungukia sababu ya aliyekuwa kocha msaidizi wa timu hiyo, Juma Mwambusi kujiweka pembeni kuendelea kukinoa kikosi hicho kinachowania ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe FA.

 

Mwambusi alijiunga na Yanga katikati ya msimu huu baada ya kocha mkuu wa timu hiyo, Mrundi Cedric Kaze kumpendekeza kocha huyo ili awe msaidizi wake mara baada ya kukabidhiwa kikosi hicho.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa, Msolla alisema kocha huyo mwenyewe ameomba kuondoka kwa ajili ya kwenda kupatiwa matibabu kutokana na kuumwa.

Msolla alisema kuwa kocha huyo aliandika barua ya kuomba kukaa nje ya timu kwa ajili ya matibabu tangu wakiwa Zanzibar wakishiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi ambalo wao walilichukua.

 

Aliongeza kuwa madaktari ndio waliomshauri kocha huyo kumpumzika kutokana na aina ya ugonjwa anaoumwa ambao hatakiwi kuongea kwa sauti kubwa, hivyo hivi sasa amepumzika kwa ajili ya kupata muda wa kufanyiwa vipimo hospitalini.

 

“Kama ulikuwa unafuatilia kwa karibu michuano ya Kombe la Mapinduzi utagundua kitu, kwani alikuwa muda wote amekaa kwenye benchi na kocha wa makipa Niyonkuru (Vladimir) ambaye kocha wa makipa na bosi wake Kaze ndiyo waliokuwa wakitoa maelekezo kwa wachezaji.

 

“Mwambusi ameachana na Yanga kwa muda baada ya kuandika barua tangu timu ikiwa Zanzibar na hii ni kutokana na maagizo na ushauri wa daktari kwa maana haruhusiwi kuongea kwa nguvu, sasa ukiangalia kazi ya makocha ni lazima waongee.“

 

Hivyo, kwa maelezo pia tumempa nafasi Kocha Kaze atafute msaidizi wake atakayefaa kuwa naye hadi Mwambusi atakaporudi tena katika timu,” alisema Msolla na kuongeza:

 

“Wapo baadhi ya wachezaji wetu wa zamani waliowahi kuichezea Yanga kutajwa kuchukua nafasi yake kati ya hao ni Nizar (Khalfani) ambaye bado hajapitishwa, lakini wapo wachezaji wengi wa zamani waliopita katika timu yetu watakaouchukua nafasi yake, lakini kwa sasa suala hilo tumemuachia kocha Kaze atupatie pendekezo lake la kocha atakayemhitaji.”

Stori: Wilbert Molandi, Dar es Salaam

 

⚫️ Kwa UPDATES za Michezo, Download GLOBAL APP: ⚫️ ANDROID:http://bit.ly/38Lluc8 ⚫️ iOS:https://apple.co/38HjiCx

Leave A Reply