ILIPOISHIA
Hisia tulivu humsaidia mtu kukabiliana na vikwazo maishani mwake ambavyo wengine wasingeweza. Huwa na uwezo mkubwa wa kupitia shida na raha bila ya mwili wake kupata madhara yoyote.
Endelea……
NINI CHA KUFANYA UNAPOGUNDUA UKO KWENYE MSONGO?
Bila shaka baada ya kusoma mada hii umeanza kuwa na mwanga juu ya msongo na unaweza kujigundua au kumgundua mtu wako wa jirani anayesumbuliwa na msongo hivyo kuwa katika nafasi nzuri ya kuondokana na tatizo hili.
Zifuatazo ni mbinu ambazo zitakusaidia namna ya kujitibu mwenyewe na kumaliza kabisa tatizo la msongo.
-Baada ya kugundua kuwa umesongeka, kaa chini tuliza akili yako na jiulize ni kitu gani unachodhani ndicho kilichosababisha ukawa katika hali hiyo.
-Badili namna unavyofikiri. Badala ya kufikiria kushindwa, kukata tama na kupoteza matumaini maishani mwako, jiambie kuwa unaweza kufanikiwa na una uhakika wa kufika pale unapopataka.
-Acha kuhesabu mabaya yaliyokutokea hata kama ni mengi na makubwa kiasi gani na badala yake utazame upande mzuri wa maisha yako hata kama kuna mambo machache na madogo uliyoyafanya vizuri. Endelea kufikiri vizuri kwa kadiri uwezavyo. Tazama upya na rudia kujifunza namna ya kufikiri vizuri.
-Usiruhusu mwili wako ukakaa bila shughuli yoyote. Fanya kazi za mikono kadiri uwezavyo, fanya mazoezi na shiriki kwenye michezo unayoipenda zaidi. Utafiti umeonesha kuwa mazoezi ya mwili yana umuhimu mkubwa sana wa kupunguza au kumaliza kabisa tatizo la msongo.
– Fanya mazoezi ya kupumua vizuri na kupumzisha mawazo yako. Kupumua kwa kuvuta pumzi ndefu puani taratibu na kuitoa kupitia mdomoni kunaelezwa kuwa husaidia sana kutuliza mawazo.
-Sali kila siku kwa imani ya dini yako. Inaelezwa kuwa sala hasa zile za usiku husaidia sana kupunguza au kumaliza kabisa tatizo la msongo. Tahajudi (Meditations) nayo husaidia kwa kiwango kikubwa sana kumaliza msongo.
-Fanya yale mambo ambayo huwa unayafurahia sana maishani mwako. Jilazimishe kufurahi hata kama bado unajihisi kuelemewa na huzuni. Kwa kufanya mambo yanayotufurahisha , tunakuwa tunalazimisha akili zetu kuingiza kitu kipya, furaha, ambayo huchukua nafasi ya hisia chungu zilizotuletea msongo.
-Matumizi ya vidonge kwa ajili ya kuondoa msongo yanapaswa kuzuiwa kwani hutoa nafuu ya muda mfupi na baada ya nguvu ya dawa kuisha mwilini, tatizo huwa kubwa mara dufu.
-Jenga mazoea ya kutembelea sehemu zenye mandhari tulivu yatakayokufanya ufarijike na kujisikia amani ya nafsi. Tembelea sehemu kama fukwe za bahari, bustani nzuri za maua au sehemu nyingine tulivu.
Comments are closed.